Mwenyekiti wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu Kenya, David
Sankok akionyesha hali halisi ya maisha ya mtoto huyo kabla ya kuokolewa. Picha
na Ndaya Mgoyo
Juni 21 ilikuwa ni siku ya kawaida kwa Mama Nancy mkazi wa
Narok nchini Kenya, lakini ilifichua siri nzito ya mtoto aliyefichwa kwa miaka
kumi katika banda la mbuzi.Akiwa katika shughuli zake za nyumbani, mara
akatokea mtoto mdogo wa jirani yake aitwaye Jane. Binti huyo akaanza kucheza na wenzake
kwa dakika kadhaa na mara akaacha michezo na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani
kwao.Wenzake wakamuuliza “mbona unakimbia wakati bado tunacheza”. Akajibu,
“nakwenda kwenye banda la mifugo kumpa chakula Ben. Muda umekimbia na hakuna
mtu nyumbani”.Kwa kauli hiyo, mwanamke huyo alitaka kujua iwapo Ben anaishi
kwenye nyumba ya jirani yake kwani ni miaka 10 imepita tangu amtie machoni.“Ben
yupo na anaishi kwenye banda la mifugo. Huwa anahudumiwa na mama, lakini kwa
sasa mama hayupo na baba amekwenda kazini. Mimi nina jukumu la kumpa chakula,”
alijibu Jane.
Mama huyo akapata shauku ya kumtembelea mtoto huyo kuona
kinachoendelea kwa jirani zake, Lo! anachokiona haamini macho yake; Mtoto Ben
amefungwa kwa kamba kwenye kigodoro chembamba akiwa hajiwezi kwa njaa.
Hivyo ndivyo alivyoibuliwa mtoto Ben baada ya kukaa katika
banda la mbuzi kwa muda wa miaka 10 bila majirani kufahamu.
Ben, ambaye kwa sasa ana miaka miaka 14 alizaliwa akiwa kiziwi, bubu na ulemavu. Aibu ya kuzaa mtoto kama huyo
ndiyo ilifanya wazazi wake wamfungie kwenye zizi la wanyama kwa muda wa miaka
10 na wakihakikisha hakuna jirani wala
ndugu wa karibu anayefahamu juu ya tukio hilo.
Historia ya mtoto huyo
Kwa mujibu wa baba mlezi Mr Jeremiah Mbusia, ambaye ni askari katika Wizara ya Mali Asili,
Narok Kenya, mtoto huyo siyo wake wa
kuzaa bali alifika katika nyumba hiyo miaka 12 iliyopita akiwa na mama yake
wakati huo mtoto huyo alikuwa na miaka minne.
Alilelewa katika nyumba hiyo kwa miaka miwili na ndipo
wazazi wake, yaani baba yake wa kambo na mama yake mzazi wakaamua kumuweka
katika kibanda kidogo nje ya nyumba yao
na hutumiwa kama zizi la mbuzi na kondoo.
Maisha ndani ya zizi
Akiwa kwenye zizi mtoto huyo aliwekewa godoro ukutani na
mkono wake mmoja ulifungwa kwa kamba ukutani.
Ilikuwa ni vigumu kuvumilia harufu kali kutoka katika zizi
hilo kwani kulikuwa na mchanganyiko wa kinyesi na mikojo ya binadamu na
wanyama.
Wadogo zake Ben walisema kuwa wazazi wao huwa wanamsafisha
mtoto huyo wakati wowote wanaotaka na kuwa anaweza kushinda na kinyesi au
kulala nacho.
“Ni mara chache kukuta akisafishwa mara mbili kwa siku. Kwa kawaida husafishwa
mara moja tu na wakati mwingine hasafishwi kabisa,” alisema mtoto huyo.
Kwa nini ilikuwa rahisi kujulikana?
Ugunduzi wa mtoto huyo ulitokana na ukweli kwamba mama yake
aliamua kuondoka nyumbani na kuacha familia nzima kutokana na ugomvi na mume
wake.
Mama huyo alikuwa akifanya siri ya kulinda mtoto huyo
asijulikane hapo nyumbani na alipoondoka watoto wenzake ndiyo walikuwa na
jukumu la kumlisha mwezao.
Kauli ya baba mlezi
Kwa kujibu wa baba wa kambo, mama wa mtoto huyo alikuwa
hamtaki mwanaye kwani aliamini kwamba kuishi naye ni kuongeza mikosi.
Baada ya kuishi pamoja walijikuta wakiwa wamezaa watoto
watatu na mama huyo aliona kuwa watoto hao ndio walikuwa muhimu katika maisha
yake kuliko Ben, ambaye alimzaa na mwanaume mwingine kabla ya kuolewa katika
ndoa rasmi.
“Mama yake alikuwa hampendi na hata wazo la kumweka katika
banda lilitoka kwake. Aliamini kuwa kukaa naye ndani kama watoto wa kawaida ilikuwa
ni usumbufu na akitoa visingizio kwamba akikaa ndani anaweza kuvunja vitu na
kuwa anaweza kushika vitu vya hatari kama vile moto,” alijitetea baba mlezi wa
Ben.
“Tulikosana na mama watoto kwa ugomvi wa kawaida tu katika
familia, hiyo ilikuwa ni miezi minne iliyopita, ajabu ni kwamba amenikimbia na
kuniachia familia akiwamo mtoto mlemavu.” “Nashindwa kumlea vizuri kwa kuwa
natakiwa kwenda katika mihangaiko yangu ndiyo maana wadogo zake walikuwa
wakimhudumia wakati sipo.”
Imefahamika kuwa mwanamke huyo amekimbilia kwao eneo la
Rimuru, Kenya ambapo ni kwa wazazi wake na akiwaambia jamaa zake wa karibu kuwa
hawezi kurudi katika nyumba ya mume wake kwani hawapatani.
Kauli za majirani
Majirani wanasema walikuwa wakifahamu kuwa nyumbani kwa
jirani yao kuna mtoto mwenye ulemavu wa akili lakini hawakumwona kwa muda
mrefu.
“Tulikuwa tukifahamu kwamba kuna mtoto mlemavu wa akili
lakini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita hatukumwona. Tulidhani wamemhamishia sehemu nyingine. Ilikuwani
vigumu kusikia sauti kwa kuwa mtoto mwenyewe ni bubu na kiziwi,” alisema jirani
mmoja.
Kumuokoa Ben
Baada ya majirani kupata taarifa za kuwepo kwa mtoto huyo,
walimuita mwandishi wa habari mmoja ili kushuhudia hali halisi.
Mwandishi huyo alitoa taarifa polisi na pia kwa Mwenyekiti wa
Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Kenya, Dk David Ole Sankok na kwa pamoja walivamia katika nyumba hiyo
iliyopo Fanaka Estate, Narok na kumwokoa mtoto huyo katika mateso.
Baada ya kumtoa kwenye kibanda hicho waligundua kuwa hali ya
mtoto huyo haikuwa nzuri kwani alikuwa
amepooza upande mmoja wa kushoto kutokana na kulala kwa muda mrefu, viungo
vyake vilikuwa vimejikunja kutokana na kukosa lishe kwa siku nyingi na nywele
zake zilibadilika rangi kutokana na kutokaa kwenye mwanga wa jua kwa muda mrefu.
“Alikuwa akitoa harufu kali, ilikuwa ni vigumu hata
kumsogelea, lakini kwa kuwa tulikuwa tumedhamiria kumwokoa ilibidi tufanye
hivyo,” akasema Dk Ole Sankok. “Tulimkuta katika mateso makubwa sana, eneo
alilokuwa amelala lilikuwa na kunguni, chawa na viroboto wengi,” anasema.
Anaongeza kuwa wadudu hao walipokuwa wakimsogelea kinywani
alikuwa akiwatafuna na kuwameza kwani alikuwa na njaa muda wote.
“Nilipoona hali hiyo nilijaribu kuondoa viroboto waliokuwa
karibu na mdomo wake, kwa kuwa alikuwa amewazoea sana na aliona ni kama kitoweo
chake alitoa sauti ya ukali kuashiria kwamba nisiwatoe, nilipojaribu kuwatoa
kwa nguvu alitaka kuniuma kwa meno,” alisema daktari huyo.
Wazazi wa kijana huyo walikuwa hawaaniki godoro nje kwani
hawakua na jingine la kumtandikia pia walihofia majirani huenda wangehoji.
Huduma ya kwanza
Baada ya kugunduliwa, Ben alipelekwa katika Hospitali ya Mji
wa Narok kwa ajili ya matibabu. Alipewa huduma za haraka ikiwa ni pamoja na
huduma za kurudisha afya mwilini kwa vyakula vya protini na vitamini.
Vilevile alikuwa akianikwa juani mara kwa mara kwa lengo la
kumrudishai vitamini. Kwa kuwa mgongo wa mtoto huyo ulianza kutoa vidonda
alipewa matibabu ya vidonda.
“Mtoto huyo alikuwa
amepungua mwili kwa kiasi kikubwa
ilikuwa unaweza kumbeba kama mtoto mdogo. Hata rangi yake ya ngozi ilibadilika,” alisema Dk
Sankok, ambaye pia anaendesha kliniki binafsi katika mji wa Narok.
“Licha ya kuwa na umri wa miaka 14 alikuwa na kilo 15
pekee,” aliongeza.
Sankok
aliwahakikishia watu waliomzunguka mtoto huyo kwamba atamfikisha katika kituo
cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo na atampa mazoezi ya
kutosha kuhakikisha anarudi katika hali ya kawaida.
“Unajua kuna wazazi ambao wana kawaida ya kuwaficha watoto
wao kwa sababu wana matatizo ya viungo ama
ya akili. Hilo siyo jambo zuri hata kidogo, watoto kama hao ni binadamu
wa kawaida na wanatakiwa kulelewa kwa misingi yote ya kibinadamu,” anasema.
Anasema kama mzazi anaona hawezi kumhudumia mtoto kama huyo
ni bora amfikishe katika vituo vya kulea watu wa aina hiyo kuliko kumficha
ndani na kumpa mateso makubwa.
via>>mwananchi
No comments:
Post a Comment