Watu wenye silaha wameua watu saba wakiwemo maafisa wanne wa
polisi baada ya kushambulia basi la abiria katika kaunti ya Lamu kwenye mwambao
wa Kenya.
Watu hao walishambulia basi hilo kwa risasi karibu na mji wa
Witu, takriban kilomita 50 kutoka Lamu.
Baadaye walishambulia gari la polisi lililofika katika eneo
la tukio.
Kundi la al-Shabab limesema limefanya shambulio hilo.
Basi hilo lililoshambuliwa siku ya
Ijumaa lilikuwa
likisafiri kutoka Mombasa kwenda Lamu. Watu hao walishambulia basi hilo baada
ya kuziba njia na gari lao.
Dereva wa basi ni miongoni mwa waliouawa, amesema kamishna
Miiri Njenga wa kaunti ya Lamu akizungumza na shirika la habari la Reuters.
Watu wanane wamelazwa hospitali, wengi kwa majeraha ya
risasi.
Shambulio hili limekuja siku moja baada ya jeshi la Kenya
kusema ndege yake imeteketeza kambi zinazotumika na kundi hilo katika eneo
hilo.
Msemaji Wa al-Shabab, Abdulaziz Abu Musab, ameiambia Reuters
kuwa tangazo hilo la Kenya ni "propaganda".
Kuhusu shambulio la Ijumaa, amesema ni "kujibu madai ya
Kenya kuwa imepeleka wanajeshi wengi katika eneo la pwani na kuimarisha
usalama".
Mamia ya familia zimekimbia makazi yao katika maeneo hayo
kutokana na kutetereka kwa hali ya usalama ambayo pia imeathiri sekta ya
utalii.
No comments:
Post a Comment