Makamu Mkuu wa Chuo cha International Medical and
Technological University (IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la
blue) na viongozi wengine wakisindikizwa
na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya
mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la Mpigi Bunju.
Picha na Rafael Lubava
Dar es Salaam. Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya
binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar
es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia
(IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho
kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa
na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa
awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya
IMTU.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la
Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo
vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi
saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana
na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya
binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi
ya juu kwa ajili ya kutupwa eneo la
Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina
mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya
aina mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote
na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika
hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali
ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua
sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini
wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya
kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa
hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na
kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi,
ninachoweza kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”Chanzo
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment