Pages

Thursday, July 31, 2014

WAZIRI WA AFYA ABANWA KISA VIUNGO VYA BINADAMU




Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod  Slaa, amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif  Rashid, kuwajibika kutokana na uzembe uliofanywa na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU).
Slaa ameitaka pia serikali kutoa kauli kuhusu hatima ya wanafunzi wa chuo hicho kufungiwa wakati makosa yametokana na serikali yenyewe kutokiwajibisha chuo hicho kwa sababu kimekuwa kikifanya makosa mengi na kwa muda mrefu sasa.



Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua tawi la Jumuiya ya Wanafunzi wa Chadema (Chaso) tawi la Muhimbili, Dk. Slaa alisema ni jambo la kushangaza kuona taratibu za kitaaluma zikikiukwa halafu waziri mwenye dhamana ya afya akiendelea kukaa madarakani.

 “Nilitegemea Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Rashid atajiuzuru. Yaani viungo vya binadamu vinatupwa kama takataka (jalalani) halafu kiongozi mwenye dhamana amenyamaza... haiwezekani,” alisema.

Aliongeza: “Ninamtaka Rais (Jakaya Kikwete) amwajibishe Waziri wake juu ya kashfa hiyo, lakini pia atoe kauli juu ya wanafunzi baada ya chuo kufungiwa.”

Dk. Slaa alisema serikali imefanya uzembe kwa kutokuiwajibisha hospitali hiyo kwa kuwa ni siku nyingi imekuwa ikilalamikiwa kuwa na matatizo.

Alisema siyo haki kuwaadhibu wanafunzi kutokana na makosa ambayo yamefanywa na serikali ya kushindwa kuichukulia hatua hospitali hiyo.

Alisema ni vema rais atoe tamko juu ya hatima ya wanafunzi hao na ikiwezekana wapelekwe katika vyuo vingine  ili waendelee na masomo.

Jitihada za kumpata Waziri wa Afya ili aelezee suala hilo zilishindikana jana baada ya kutopatikana kupitia simu yake ya mkononi.

Serikali iliifungia hospitali ya IMTU kwa muda usiojulikana kuanzia Julai 25 mwaka huu kutokana na kukutwa na makosa mbalimbali.

Kati ya makosa hayo ni pamoja na kutokuwa na watumishi wa kutosha, tanuri la kuchomea taka na kutokuwa na kibali cha maabara kwa kipindi cha miaka mitatu.

Wiki iliyopita, vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kutupwa kwa viungo vya binadamu katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusika na tukio hilo huku Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kikitoa tamko la kulaani kitendo hicho na kutaka hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya IMTU.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment