Dar es Salaam. Jukwaa la Change Tanzania, limekusanya saini
4,000 za wananchi mikoa mbalimbali, wanaopinga tozo ya kodi kwenye laini ya
simu.
Taarifa ya Mratibu wa Jukwaa hilo, Maria Sarungi, ilisema
saini hizo
ni fursa kwa mbunge au wabunge wataokuwa tayari kuitika wito
wa wapigakura wao na kupeleka hoja bungeni kwa ajili ya kufuta tozo hiyo.
Ilisema saini hizo zimekusanywa kutoka kwa
wananchi Mikoa ya
Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara, Mwanza,
Shinyanga, Singida, Ruvuma pamoja na Zanzibar.
Ilisema wananchi wanataka tozo hiyo iondolewe kwa sababu
inamkandamiza mwananchi wa hali ya kawaida na chini.
“Hawa ni asilimia 67 ya wananchi wanaoishi chini ya kipato
cha dola 1.25 (Sh2,000) kwa siku. Takwimu zinaonyesha kati ya wamiliki wa laini
za simu milioni 22, milioni nane wanatumia chini ya Sh 1,000 kwa mwezi. Huku ni
kuwaongezea mzigo wananchi hawa,” ilisema taarifa ya Sarungi.
Pia, Ilisema tozo hiyo itawanyima kabisa wananchi hao, fursa
ya kutumia huduma muhimu ya mawasiliano ya simu.
“Lakini kodi hii haifuati misingi ya kulipa kwa kadiri ya
matumizi, ni kodi kandamizi inayotozwa kwa wamiliki wa laini za simu wote kwa
kiasi kimoja bila kuzingatia kiwango cha matumizi,” ilisisitiza.
Ilisema kodi hiyo ni juu ya ongezeko la kodi mbalimbali kwa
huduma za simu za mkononi ikiwamo kuongezeka kwa ushuru kutoka asilimia 12 hadi
14.5.
No comments:
Post a Comment