Sewa Haji Paroo alijenga jengo la kutoa huduma za afya kwa
watu mbalimbali. Picha na Charles Kayoka.
KWA UFUPI
Alipokutana na Stanley alikuwa na miaka 20 tu, alizaliwa
mwaka 1851.
Wasomaji kadhaa walitaka kujua zaidi kuhusu Sewa Haji Paroo
anayetambulika kama mtu wa kwanza aliyejitolea kuanzisha huduma za afya na
elimu kwa faida ya watu wote bila kujali rangi, daraja la kiuchumi wala dini ya
mtu yoyote.
Ikumbukwe kwamba Bagamoyo kabla ya 1900 ulikuwa mji maarufu
sana na makao makuu ya kwanza ya Serikali ya kikoloni yalikuwa katika mji huo
chini ya Deutch Ost Africa. Watu wengi wakiwamo wazazi wa Sewa Haji walifika
Bagamoyo kutoka pande mbalimbali za dunia kutafuta maisha.
Sewa Haji Paroo anatajwa na Henry Morton Stanley mpelelezi
na mwandishi wa habari kutoka Marekani mwenye asili ya Uingereza kama Soor
Hadji Paloo katika kitabu chake kuhusu safari ya Kumtafuta Dk David
Livingstone.
Stanley alifika Bagamoyo akitokea Unguja Machi 1871 akiwa
njiani kwenda Ujiji kumtafuta Livingstone na alielekezwa kumwona Soor Hadji
(Sewa Haji) kwa ajili ya msaada wa kumtafutia wapagazi wa kumbebea mizigo hadi
Ujiji; kumtafutia nguo, majora, vitenge na kaniki na sari na khaki tetroni.
Pia alikusanya shanga za aina mbalimbali ambazo zilikuwa
zikitumika kama malipo kwa ajili ya kununulia mbuzi, mtama na vyakula vingine
kwa ajili ya kuwalisha wapagazi. Soor Hadji, alitambulika pia kama mchuuzi
mashuhuri wa biashara ya silaha ambazo alikuwa akiziagiza kutoka India. Wakati
alipokutana na Stanley alikuwa na miaka 20 tu, alizaliwa 1851.
Wakati huo wamisionari na wapelelezi kama kina Livingstone,
Burton, Speke na Stanley walikuwa wakihitaji bunduki kwa ajili ya ulinzi na
kuwindia wanyama. Stanley anamweleza Soor Haji kama kijana mwenye unyenyekevu
sana wa dini, lakini katika biashara alikuwa mwerevu sana na mwenye akili
iliyokuwa ikifikiri kwa kasi sana.
Anamlaumu kuwa, katika kufanya biashara alikuwa mjanja kwa
kupata zaidi ya Dola 1,300 za Marekani kutoka kwa Stanley peke yake. Soor Haji
alinunua majengo Bagamoyo na Dar es Salaam na huko Mombasa kwa ajili ya
kutumika kwa watu maskini.
Chanzo:Mwananchi
===================
Sewa Haji, soma historia ya mtu alietukuka. Ndie alietajwa
katika moja ya wodi ama majengo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili...
Inasadikiwa Hospitali ya Muhimbili ndie alieijenga kabla ya Waingereza
kuichukua na kuiendeleza.
SEWA HAJI PAROO, ALITOA MCHANGO MUHIMU KATIKA MAENDELEO YA
AFRIKA.
Ingawa alikuwa mfanyabiashara maarufu na tajiri sana, Bw.
Sewa Haji Paroo anatajwa alikuwa mcha Mungu na alijulikana zaidi kwa kusaidia
wasio na uwezo na wagonjwa, a
mbapo alisaidia Wahindi, Waarabu na Waswahili bili kuchagua
wala kubagua kwa Dini au Rangi zao.
Ndie alietajwa katika moja ya wodi za Hospitali kuu ya Taifa
Muhimbili Jijini Dar es salaam, ambapo kuna wodi ama jingo linaloitwa Sewa
Haji.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini na
kutambua mchango wake kwa Jamii ikaamua kuipa moja ya wodi za Hospitali hiyo ya
Taifa jina la Sewa Haji kwa heshima yake.
Sewa Haji Paroo alifariki dunia mnamo mwezi wa February
mwaka 1897 akiwa na umri wa miaka 46 na kuacha Simanzi kubwa na huzuni
isiyomithilika kwa Wakazi wenzie wa Bagamoyo hasa Wanyonge, Wagonjwa na
Wahitaji ambao aliwasaidia sana.
DUKAWALLA.
Historia ya Afrika ina mengi sana, moja kati ya Maandiko ya
Historia ya Afrika juu ya Usuli wa ujio wa Jamii ya Waasia wengi katika Afrika
Mashariki yameitaja sana Zanzibar na Bagamoyo. Maandiko hayo yameainisha kuwa
watu wengi wa Jamii hiyo walikuja Afrika Mashariki kwa Sababu ya
Kufanyabiashara na walitambulika zaidi kama "DUKAWALLAS"
(MADUKAWALLA), Ukoo wa kina Sewa Haji Paroo ni sehemu ya Maandiko hayo.
Haji Paroo Pradhan alihama kutoka Bhuj, Kutchh mpaka
Zanzibar akiwa pamoja na kaka yake Jaffer Paroo Pradhan, hawa wanatajwa kuwa
miongoni mwa Madukawalla wa awali kabisa. Mwaka 1852 walianzisha Duka dogo la
Bidhaa mbalimbali ambapo mpaka Mwaka 1860 biashara yao ilikuwa imekuwa zaidi na
hivyo kuamua kuanzisha Tawi Mjini Bagamoyo.
Mmoja kati ya Watoto wanne wa Bwana Haji Paroo Pradhan
alikuwa ni bwana Sewa Haji Paroo, ambaye alizaliwa mwaka 1851 ikiwa ni mwaka
mmoja tu tokea wazazi wake wahamie Zanzibar. Sewa alilelewa katika makkuzi ya
Kidini na kufunzwa biashara na baba yake katika umri mdogo tu.
Mwaka 1869 Mzee Haji Paroo alipata msiba mzito sana wa
kuwapoteza vijana wake wawili kati ya wanne aliobarikiwa kupata, hivyo basi
kumtaka Sewa Haji Paroo kuchukua nafasi ya kaka zake katika usimamizi wa
biashara za Familia ambazo zilikuwa chini ya Kampuni iitwayo Haji Kanji &
Co.
MISAFARA YA WAPAGAZI NA KILELE CHA MAFANIKIO.
Mwaka 1870 mara baada ya kijana mdogo Sewa haji Paroo
kukabidhiwa Mamlaka ya uendeshaji wa biashara za Familia yao alifanya
mabadiliko mengi ya kimsingi ambayo yaliiongezea mapato mno kampuni yao. Akiwa
na umri wa miaka 18 tu Sewa Haji Paroo alivivuka vizingiti vyote na kufuta
dhana ya umri katika utafutaji kwa kuifikisha biashara yao katika kilele
ambacho hata baba yake hakuota kukifikia.
Msingi Mkuu wa mafanikio ya Biashara yao ni ubunifu wake wa
kutumia misafara ya Wapagazi katika kueneza bidhaa zake na kusaka bidhaa mpya,
misafara hiyo aliieneza nchini kote ikipita Unyanyembe, Mwanza mpaka Ujiji. Kwa
kuwa Makao yake yalikuwa Bagamoyo alieneza misafara ya Wapagazi mpaka Zanzibar
ambako ndiko yalipokuwa Makao yao ya mwanzoni.
Mwanzoni Wafanyabiashara wengi wa Kizungu waliipinga dhana
yake ya kueneza biashara kwa kutumia Misafara ya Wapagazi lakini mara baada ya
kuliteka soko lote la Biashara kwa Misafara yake watu wengi walianza kumuiga na
kuikubali mbinu yake hiyo.
Sewa alijishughulisha zaidi na Uuuzaji wa Nguo, Vitambaa,
Vitanda, Sufuria za Bati na Chuma huku naye akinunua bidhaa kama Pembe za Ndovu
na meno ya Tembo kwa ajili ya kuuza kwa Wazungu. Pia Sewa Haji alipata kibali
cha kufanya Biashara ya Silaha ambapo kwa eneo hili alikuwa ndiye
mfanyabiashara mkubwa sana wa Silaha.
Mafanikio yake kwenye Biashara yalimzalishia Faida kubwa
sana ambayo iliongeza Maradufu utajiri wa Familia yao.
MSAADA KWA WAHITAJI.
Waneni hunena kuwa Mali na utajiri mwingu humbadili mtu na
kumfanya awe na kiburi, ajinate na kujiona tabu. Ajabu kwa Bwana Sewa Haji
Paroo ni kuwa Mali na Utajiri mwingi ambao alibarikiwa na Mungu ulimfanya awe
karibu zaidi na watu na wala haukumpa Kiburi na Majinaki.
Mafungamano na Ubaramaki wake na Wapagazi viliwashangaza
wengi katika wakati ule, haikuwa Mazoea kuonekana Matajiri wakila au hata
kujichanganya na Masikini namna ile. Sewa Haji alipituka mipaka kwa kufikia
hatua ya kununua Eneo na kujenga Makazi Maalum kwa ajili ya Wapagazi ili
kuwapunguzia adha ya Makazi waliyokuwa nayo.
Kwa Bwana Sewa Haji Rangi au Dini ya Mtu haikuwa na Thamani
zaidi kuliko Utu wake, alijenga Makazi Maalum kwa ajili ya Makazi ya Wakoma na
pia Akanunua Baadhi ya Majengo kwa ajili ya kuanzisha Hospitali ambayo
aliikabidhi kwa Kanisa La Bagamoyo na akaainisha katika Wosia wake Theluthi
moja ya Mali zake itumike kusaidia Gharama za Uendeshaji wa Hospitali hiyo.
Katika Mji wa Mzizima (sasa Dar es salaam) bwana Sewa Haji
Paroo alijenga Hospitali ambayo ilijulikana kama Sewa Haji Hospital, Hospitali
ambayo Wakoloni wa Kiingereza waliibadili Jina na kuiita Princess Margaret
Hospital kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Muhumbili mwaka 1961 baada ya Uhuru
wa Tanganyika.
SKULI YA SEWAHAJI/ SKULI YA MWAMBAO - SHULE YA KWANZA ISIYO
YA KIBAGUZI.
Sewa Haji alitambua na kuthamini sana Elimu, lakini pia
alikera mno na namna hiyo elimu ilivyotolewa kibaguzi na kutumika kujenga
Matabaka katika Jamii. Hivyo basi Mwaka 1892 alinunua Jengo la Ghorofa kadhaa
na kuligeuza kuwa Shule ya Kwanza ya Mchanganyiko ambayo haikujali Dini, Rangi,
Kabila au jinsia ya Mwanafunzi, Yeyote aliyekuwa Tayari kujifunza alikuwa huru
tu kwenda kusoma.
Shule hiyo ambayo ilijulikana kama Skuli ya Sewa Haji au
Skuli ya Mwambao ilifanya kazi kwa muda wa miaka mitatu chini ya ufadhili wake
ambapo mwaka 1895 Serikali ilichukua rasmi na kuigeuza Shule ya Serikali ambapo
yeye aliajiri Mkurugenzi mpaya wa Shule na pia kufadhili utafiti wa uanzishaji
wa Mtaala Bora zaidi wa kusomea.
MCHAMUNGU SEWA HAJI, DINI NI KIUNGANISHI.
Sewa Haji alikuwa mchamungu na mtu aliyependa sana dini,
alitumia sehemu kubwa ya mali yake katika kuendeleza Nyumba za Ibada bila
kuleta Ubaguzi wowote wa Kidini, Sera yake kuu ilikuwa ni Upendo kwa kila
mmoja.
Kiongozi wa Jumuia ya Waislam wa Madhehebu ya Ismailia
ambayo ndipo Bwana Sewa Haji Paroo ndo alitokea, Mawlana Sultan Muhammad Shah
alimpachika bwana Sewa Haji Cheo Kikuu cha Alijah kwa kuchamini mchango wake
kwenye Jumuiya Hiyo. Majengo ya Jumuiya Hiyo yalioko Mombasa yalijengwa naye
kama sadaka kwa Jamii yake.
Sewa Haji hakujali Dini ya Mtu katika kutoa misaada yake,
kwa Bagamoyo alijulikana sana kama Mfadhili Mkuu wa Kanisa Katoliki na mara
baada ya kifo chake Gazeti la Kanisa lilimuita "Mja Mwema wa
Kipekee".
Wamishenari wa Bagamoyo walizoea kumuita Sewa Haji
"Rafiki yetu Mtukuka" na Kuonyesha namna Kanisa lilivyoguswa na Kifo
chake siku nane tu baada ya kifo hicho kilibandikwa kibao chenye Picha yake
katika lango la kuingilia Kanisani ambacho kilisomeka “This devoted friend of
the mission will not forget (us) in his last wishes.”
Utu, Kujali na Upendo wake huu kwa watu na Jamii
iliyomzunguka vinaonyesha na kutoa taswira namna Bwana Sewa Haji Paroo
alivyokuwa kiumbe wa namna yake, Jamii ya sasa inapaswa kuiga mema yake haya.
No comments:
Post a Comment