Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini IGP Ernest Mangu
akisalimiana na masheikh wa mikoa na maimamu wa misikiti katika ukumbi
wa bwalo la maafisa wa Polisi wakati wa
kikao cha muendelezo wa kampeni
ya familia yetu haina mhalifu kilichoratibiwa na taasisi ya kiislamu ya
Mwinyi Baraka. Picha na Hassan Mdeme- wa
Jeshi la Polisi
Na Tamimu Adam – Jeshi la Polisi
Viongozi wa dini
wametakiwa kuendelea kufanya doria za kimwili na kiroho katika kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya
jamii ikiwa ni pamoja na kuwajenga
vijana katika maadili mema na kuacha
kutenda dhambi ya kujihusisha na vitendo
vya uhalifu.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu alipokutana na viongozi wa dini
ya kiislam katika ukumbi wa Bwalo la maafisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es
salaam. Kikao hicho kiliratibiwa na taasisi ya kiislamu ya Mwinyi Baraka
inayoongozwa na Sheikh Issa othuman.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mufti wa Tanzania Shabani
Simba, Katibu mkuu wa Bakwata, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Masheikh wa mikoa ya
Tanzania bara pamoja Maimamu wa Miskiti.
IGP Mangu alisema
kuwa haijawahi kutokea kokote duniani kwa Polisi kula njama na viongozi wa dini
katika kupambana na wahalifu na watenda
dhambi, hivyo aliwaomba viongozi hao wa dini waongeze mahubiri yenye kuwataka
waumini kutenda mema pamoja na kuongeza nguvu ya kuimarisha kamati za ulinzi na
usalama katika nyumba za kuabudia.
Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Shaban
Simba alisema kuwa dini zote zinahimiza waumini wake kutenda mema na
kujiepusha kushiriki katika vitendo viovu, hivyo ameliomba Jeshi la Polisi
kuendelea kuwakamata wale wote watakaobainika kutenda uhalifu kwani hivi sasa
uhalifu upo hata kwenye taasisi za dini.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa mkoa wa Arusha Shabani Juma,
wakati akitoa salamu za mkoa huo, alisema kuwa mkoa wa Arusha
kwa sasa hivi upo shwari na wa amani, hivyo ni wajibu wetu kulinda amani
tuliyonayo kwani ndio msingi wa kila kitu.
Kikao hicho ni muendelezo wa mkakati wa Jeshi la Polisi katika
kuwajengea uwezo viongozi wa dini, ambapo viongozi hao wa dini waliazimia kwa pamoja kuendelea kushirikiana na Jeshi la
Polisi katika kampeni ya kutengeneza familia zisizo na wahalifu kupitia
mahubili yao pamoja na kuendelea kuimarisha kamati za ulinzi na usalama katika
nyumba za ibada kwa rahisi ya mawasiliano katika kuwadhibiti wahalifu.
No comments:
Post a Comment