Pages

Friday, August 8, 2014

OPERESHENI BODABODA HATARI DAR

OPERESHENI ya kukamata pikipiki maarufu kama bodaboda zinazoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam, imedaiwa kuhatarisha maisha ya watu kutokana na polisi kutozingatia usalama wa wapanda pikipiki hao wanapowakamata na kuwasababishia ajali.






Baadhi ya waandishi wa habari walishuhudia kamata kamata hiyo iliyolalamikiwa na baadhi ya wananchi katika makutano ya Mtaa wa Garden na Azikiwe, Manispaa ya Ilala jana, huku ikisimamiwa na Kamanda C.N Maro.
Ajali hizo zimekuwa zikitokea kutokana na polisi kuwakimbiza wapanda pikipiki hao na kuwavuta kwa nguvu kutoka kwenye pikipiki huku wakiwa kwenye mwendo kasi pindi inapotokea mhusika amekataa kusimama.
Baada ya kukamatwa, mhusika hufungwa pingu kwa kuunganishwa na pikipiki yake na kuamriwa akae chini, kitendo kilicholalamikiwa, kwamba ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katika eneo hilo, zilikamatwa zaidi ya pikipiki 50, kati ya hizo zikiwemo za baadhi ya kampuni na raia wa kawaida, ambazo zilikuwa na vibali vya kuingia katikati ya jiji.
Hata hivyo, polisi hao walikataa kuwasikiliza kwa madai hawana taarifa kuwa kuna vibali vinavyoruhusu pikipiki kuingia katikati ya jiji.
Polisi hao, pia walimkamata na kumfunga pingu mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, kutokana na kuhoji utaratibu uliokuwa ukitumika kuwa haukuzingatia usalama wa wahusika ambao ungeweza kuwaletea madhara.
Katika hali isiyotarajiwa, polisi hao walimgeuzia kibao mtu huyo kuwa alimpiga askari na kumfanya ashindwe kufanya kazi yake wakati haikuwa kweli.
Waandishi walipofika katika eneo hilo kutaka kupatiwa ufafanuzi kuhusu askari hao kuendesha operesheni hiyo kikatili huku wakiwa peke yao bila mgambo wa jiji, Kamanda Maro alikataa kujibu na kuwaamuru kuondoka.
“Ondokeni tufanye kazi yetu, haiwahusu,” alisema.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe, alisema kuhusu operesheni hiyo, mkoa umekubaliana iendelee na hilo la kufungwa pingu inategemea mhusika alivyokuwa akitii sheria.
Pia, alishangaa kusikia kukamatwa kwa mtu aliyekuwa akihoji ukiukwaji wa taratibu za ukamataji, na kusema hata hivyo atawasiliana na Kamanda wa Kanda Maalum, Kamishna Seleman Kova, ili kupata ufafanuzi kuhusu tukio hilo
chanzo:sophie

No comments:

Post a Comment