Pages

Friday, August 22, 2014

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA WA TABORA KUFUATIA AJALI ILIYOTOKEA HIVI KARIBUNI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.  Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa  Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Fatma Mwasa kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 19 Agosti, 2014 katika Kijiji cha Mlogolo, Wilaya ya


Sikonge Mkoani Tabora. 
Ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Mlogolo Wilayani Sikonge,  ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Sabena lililokuwa likitokea Mbeya  kwenda Mwanza ambalo lililogongana uso kwa uso na basi lingine la  Kampuni ya AM Coach lililokuwa likitokea Mwanza na kusababisha vifo  vya watu 19 na kujeruhi wengine 81.  “Nimeshtushwa na kusikitishwa na ajali hii iliyogharimu maisha ya  watu 19 na wengine 81 kujeruhiwa” amesema Rais. “Pokea Salamu zangu za Rambirambi kutokana na ajali hiyo, na  kupitia kwako naomba unifikishie Salamu za Rambirambi na pole kwa  wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba  Mwenye Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za  Marehemu wote mahala pema peponi, Amina”. Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu  na ujasiri wakati huu ambao ni mgumu sana kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.

Aidha amesema anawaombea kwa Mola majeruhi wote wa ajali hiyo  waweze kupona haraka na kurejea tena katika hali zao za kawaida na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao.  Kwa mara nyingine Rais Kikwete ameendelea kusisitiza umakini na usimamizi mzuri wa Sheria ya Usalama Barabarani kutoka kwa mamlaka zinazohusika, ili maisha ya wananchi wasio na hatia yasiendelee kupotea na kusababisha simanzi kwa familia, na kupotea kwa nguvu kazi muhimu ya Taifa.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Agosti,2014

No comments:

Post a Comment