Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali
za upashanaji habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya
kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.
Chama kupitia Idara ya Habari kingependa kutoa ufafanuzi
kama ifuatavyo;
1.
Uamuzi wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba wanaotokana na CHADEMA kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA), kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi
mchakato wa Katiba Mpya, ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu
iliyoketi Julai 18-19 na kuazimia kwamba;
§ Wajumbe
wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye
vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka ya Bunge hilo yatafafanuliwa kuwa ni
ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta, misingi mikuu (basic features) ya
Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi na kuandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais kwa ajili hiyo;
§ Wajumbe
wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye
vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na baada ya, ufafanuzi uliotajwa katika aya
ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge Maalum, pamoja na Kanuni husika
za Bunge Maalum;
§ Wajumbe
wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum hawatashiriki katika kikao chochote cha
Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum
uliotajwa katika aya za 2 na 3 utakapofanyika kwa mujibu wa maazimjo ya Kamati
Kuu;
Hadi wakati huu, hakuna jambo hata moja
kati ya hayo lililofanyika, huku mazungumzo yaliyotarajiwa kuokoa mchakato yakiwa
yamevunjika, kwa sababu CCM na Serikali yake wameamua kudharau na kupuuza maoni
ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba badala yake kuweka maslahi ya
chama hicho kwenye katiba.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
2.
Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba wanaotokana na CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya kuhudhuria
vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au watashiriki
vikao vya bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya kujieleza kisha
chama kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake kupitia vikao.
3.
Tunapenda
pia kuwakumbusha wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa Watanzania kuwa, mji wa
Dodoma mbali ya kuwa Makao Makuu ya Nchi pia inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba ambako
hakujaridhiwa na Watanzania wengi, hakujazuia shughuli za Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kufanyika ikiwemo kutoa huduma kwa watu mbalimbali ikiwa
ni pamoja na wabunge. Suala hilo linakwenda sambamba na ukweli kwamba sehemu kubwa
ya watumishi wa Bunge Maalum la Katiba ni wale wale ambao wanatakiwa
kuwahudumia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba.
Hivyo kuonekana kwa mbunge yeyote wa
CHADEMA mjini Dodoma au kwenye viwanja au Ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mbunge husika amehudhuria
vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kinyume na msimamo wa UKAWA.
Imetolewa
leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini
Makene
Mkuu wa
Idara ya Habari- CHADEMA
No comments:
Post a Comment