Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja
Jeshi la Magereza Nchini limeibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Ruvuma), Kanda ya Kasikazini(Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara), Kanda ya Magharibi(Mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam) pamoja na Kanda ya Magharibi(Mikoa ya Tabora, Kigoma na Shinyanga) ambapo Jeshi la Magereza limeibuka Kidedea katika upande wa uzalishaji wa mazao ya Kilimo na Mifugo.
Jeshi la Magereza ni Miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwa na jukumu lake la kuwahifadhi na kuwarekebisha Wafungwa wa aina mbalimbali wawapo Magerezani ili pindi wamalizapo vifungo vyao waweze kuwa raia wema katika jamii. Pia hushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kikanda kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kupitia shughuli zake mbalimbali za uzalishaji katika Sekta za Kilimo na Ufugaji.
Mbali na ushindi huo wa Kikanda, Jeshi la Magereza limeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa(Maarufu kama Nane Nane) katika Mkoa wa Lindi ambapo Jeshi hilo limeibuka Mshindi wa Pili wa jumla katika Kilele cha Maonesho hayo huku Jeshi la Kujenga Taifa likibuka Mshindi wa Kwanza wa jumla na Mgeni rasmi katika Kilele cha Maonesho hayo Kitaifa alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed Ghalib Bilal.
Kutokana na Ushindi huo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amewapongeza Maafisa na Askari wote walioshiriki kikamilifu katika Maonesho hayo hadi kufanikisha ushindi huo na amewapa changamoto ya kuongeza bidii zaidi katika utendaji wao wa majukumu ya kazi ili katika Maonesho yajayo waweze kufanya vizuri zaidi.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Jeshi la Magereza kuibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Taasisi za Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Kikanda hapa nchini ambapo katika Maonesho ya Nane Nane ya Mwaka 2013 Jeshi la Magereza lilibuka Mshindi wa kwanza katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mshindi wa kwanza wa jumla katika Kilele cha Maonesho ya Nane Nane Kitaifa ya Mwaka 2013 yalifanyika Nzuguni, Mkoani Dodoma.
Imetolewa na Mkaguzi wa Magereza, Lucas Mboje,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Agosti 08, 2014.
No comments:
Post a Comment