Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu,Bi. Nikki Clarke akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,katika Jengo lao lililopo Mikocheni.Kushoto ni Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh (wa tatu kulia) akiwapatia maelekezo Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Dkt. Salim Ahmed Salim na Mwenyekiti wa CUF,Prof. Ibrahim Lipumba ya namna Idhaa hiyo inavyoandaa vipindi yake na inavyopeleka hewani wakati wa hafla ya Uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC,jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu,Bi. Nikki Clarke akibadilishana mawazo na aliewahi kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Tiddo Mhando wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,Hassan Mhelela (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo pamoja na kuitambulisha timu yake.
Baadhi ya Wageni waalikwa wakiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wakuu wa BBC waliokuwepo kwenye hafla hiyo,jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa zamani wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Tiddo Mhando (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Ali Saleh pamoja na Mtangazaji Sussani Mongi.
Taswira za Studio za BBC jijini Dar.
Chumba cha Habari cha BBC jijini Dar.
Wadau Salim Kikeke na Nicolas wakipitia habari kabla ya kuipeleka hewani.
BBC Idhaa ya Ulimwengu, imezindua ofisi zake jijini Dar es Salaam. Ofisi za Dar es Salaam zina studio ambazo zinatumika kuandaa matangazo maarufu ya redio ya asubuhi, Amka na BBC, na pia kuendesha tovuti ya bbcswahili.com.
Katika kuadhimisha uzinduzi huo, vipindi vingine viwili vya BBC Idhaa ya Kiswahili, Dira ya Dunia ya redio na ya TV vitaandaliwa kutoka Dar es Salaam katika siku hiyo ya Jumatatu Agosti 11.
Ufunguzi wa ofisi za Dar es Salaam ni matokeo ya mikakati ya BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuhamisha uandaaji wa vipindi vya redio na tovuti kutoka London kwenda Afrika Mashariki.
Ofisi mpya ina vifaa vya kisasa vinavyoweza kutayarisha vipindi vya redio, TV na huduma za habari kwa njia ya simu za mkononi. Amka na BBC, kipindi cha nusu saa ambacho hutangazwa Jumatatu hadi Ijumaa humulika matukio na taarifa zitakazojiri katika siku, sasa kitaandaliwa Dar es Salaam na watayarishaji na watangazaji 15.
Ofisi mpya pia zina watayarishaji wanaoandaa taarifa mbalimbali za kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya vipindi vya TV vya Focus on Africa na Dira ya Dunia. Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu Nikki Clarke amesema:
“Uzinduzi wa ofisi zetu za Dar es Salaam ni hatua kubwa katika safari yetu iliyoanza muda mrefu kidogo, katika kuwapa wanachotaka wasikilizaji katika nchi zinazozungumza Kiswahili, na ambao husikiliza BBC wanapotaka kupata taarifa wanazoziamini na zenye uhakika. Takriban watu milioni 12.4 – ambao ni kama nusu ya idadi ya watu wazima nchini Tanzania, husikiliza matangazo ya redio ya BBC kila wiki.
Na sasa moja ya kipindi maarufu cha BBC, Amka na BBC, kimekuja karibu zaidi na wasikilizaji.” Ofisi ya Dar es Salaam, ina studio mbili za redio ambazo zinaweza kutumika na hadi watu sita kwa wakati mmoja, na hivyo ni muafaka kabisa kwa kipindi kichangamfu cha Amka na BBC kwa ajili ya mijadala na mahojiano ya kuvutia.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh anasema : “Ofisi mpya zinatoa nafasi bora kabisa kwa watayarishaji wa BBC nchini Tanzania kuimarisha ukusanyaji wa habari na kutoa taarifa kutoka katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Amka na BBC itakuwa na uwezo mkubwa zaidi kutoa taarifa na habari mchanganyiko, za Afrika Mashariki na pia za dunia, pamoja na mahojiano ya moja kwa moja na watu mbalimbali, lakini pia makala na habari za kijamii.” Idhaa ya Kiswahili ya BBC imekuwa kitovu cha hatua ya BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuimarisha kuwepo kwake katika sekta ya habari barani Afrika.
Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Nairobi mwaka 1998, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilikuwa shirika la kwanza la habari la kimataifa kuwa na kituo cha uandaaji habari barani Afrika. Mwaka 2006 Amka na BBC ilihamishwa kutoka London kwenda Nairobi, na BBC Idhaa ya Ulimwengu, kwa mara nyingine tena ikawa shirika la kwanza la kimataifa la habari kuandaa na kutangaza vipindi kutoka barani Afrika.
Katika hatua ya kuhamisha utayarisaji wa vipindi na taarifa za kwenye tovuti, kipindi maarufu cha jioni cha redio, Dira ya Dunia sasa kinatayarishwa Nairobi. Mwisho// Kwa taarifa zaidi wasiliana na afisa wa idara ya mawasiliano ya BBC Idhaa ya Ulimwengu – Lala Najafova, lala.najafova@bbc.co.uk.
Kwa wahariri: BBC Idhaa ya Ulimwengu ni shirika la utangazaji la kimataifa lenye idhaa nyingi za lugha mbalimbali zinazotoa huduma ya matangazo ya redio, TV, kwenye mtandao wa internet na pia simu za mkononi. BBC Idhaa ya Ulimwengu hutumia njia mbalimbali kuwafikia wasikilizaji wake wapatao milioni 191 duniani kote. BBC huwafikia watu milioni 265 duniani kote kila wiki kwa huduma zake kutoka BBC Idhaa ya Ulimwengu, BBC News TV na bbc.com.
chanzo:full shangwe
No comments:
Post a Comment