Spika wa Bunge la
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dkt. Magret Zziwa (wa pili kulia) akipewa
maelezo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya TICS Paul Wallace namna kampuni yake
inavyofanyakazi ya kupakua na kupakia mizigo katika bandari ya Dar es salaam
wakati wa ziara ya Wabunge wa bunge hilo
walipotembelea ofisi za Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) jana jijini Dar es salaam.
Picha na Eleuteri
Mangi-MAELEZO)
…………………………………………………
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
29/08/2014
Jumuiya ya Afrika
Mashariki iko makini katika kutekeleza majukumu yake na iko karibu na watu wake
kwa kuwahudumia kupitia nchi washirika.
Kauli hiyo imetolewa
na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dkt. Magret Zziwa
wakati wa ziara yake alipotembelea ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
pamoja na wabunge wa bunge hilo jana jijini Dar es salaam.
Spika Dkt. Zziwa
alibainisha kuwa lengo la ziara ya wabunge hao ni kujionea shughuli mbalimbali
zinazofanywa na TPA na Bandari ya Dar es salaam kwa ujumla katika kuhudumia
nchi washirka kiuchumi na kujiamii.
“Ni muhimu kuifanya
Jumuiya kuwa imara zaidi kiuchumi na kijamii ili kuwahudumia watu wetu kwa
umahiri na umakini mkubwa katika mahitaji yao” alisema Spika Dkt. Zziwa.
Wabunge hao
walitembelea maeneo mbalimbali bandarini hapo na kujionea shughuli zinazofanywa
ikiwa ni pamoja na kupakia na kupakua mizigo inapoingia au kutoka ili
kusafirishwa kwenda nchi husika.
Spika Dkt. Zziwa
alisisitiza kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanahitaji kuona
jumuiya yao inavyowajali na kuwahudumia wanapotekeleza majukumu yao
ikizingatiwa kuwa kwa sasa hakutakuwa na urasimu wa kusafirisha mizigo kutoka
nchi moja kenda nyingine kwa kukaguliwa mara mbili ambapo kwa sasa utaratibu wa
Himaya Moja ya Forodha umeanza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Akionesha umuhimu wa
uchukuzi na usafirishaji wa mizigo kati ya nchi washirika, Naibu Waziri wa
Wizara ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki, Dkt. Abdala Juma Abdulla Saadalla
amefananisha bandari, reli na barabara katika nchi kuwa ni sawa na “moyo na
mishipa ya damu” ambapo amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea
kuboresha reli zilizopo ili ziweze kutoa huduma kwa wakati.
“Tayari Serikali
kupitia wataalamu wake wa ndani imeboresha vichwa vya treni nane hadi sasa
ambapo vinatarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani pamoja na makasha” alisema
Naibu Waziri Saadalla.
Kwa upange wake
Meneja wa Bandari ya Da es salaam Awadh Massawe alipokuwa akiwaeleza Wabunge wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki namna TPA inavyofanya kazi, amesema kuwa kwa mwaka
2013/2014 mizigo inayosafirishwa kutoka bandarini hapo imeongezeka kutoka tani
milioni 4.05 mwaka 2012/13 hadi tani milioni 4.45 mwaka 2013/2014 ambayo ni
sawa na asilimia 9.8.
Massawe amesema kuwa
mizigo hiyo ilisafirishwa kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda nchi za
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Burundi, Rwanda, Malawi and Uganda kwa
kutumia mifumo ya barabara na reli.
Massawe amesema kuwa
bandari ya Dar es salaam imekuwa ni kiunganishi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kutumia mitandao iliyopo ya njia ya reli na barabara.
Kwa upande wa reli,
Massawe amesema kuwa Bandari ya Dar es salaam inaunganishwa na reli ya kati
kwenda Mwanza na Kigoma hali inayorahisisha nchi za Burundi, Rwanda na Kongo
DRC kufikika kirahisi na TARZARA ambayo inakwenda hadi Zambia.
Kwa njia ya
barabara,Bandari ya Dar es salaam inaunganisha Tanzania na nchi nyingine
kuanzia Dar es salaam kupitia Dodoma/Isaka/Rusumo /Kabanga, Kigali hadi
Bujumbura kwa Rwanda na Burundi, vilevile Dodoma/Mwanza/Mutukula hadi Kampala
Uganda.
Aidha, Massawe
amesema kuwa kwa mwaka 2013/2014 kumekuwa na jumla ya asilimia 30.4 ya mizigo
yote ilihudumiwa na bandari ya Dar es salaam.
Massawe amesema kuwa
ongezeko hilo la usafirishaji wa mizigo linatokana na maboresho yaliyofanywa
bandarini hapo kuhusu namna ya usafirishaji wa mizingo kufuatia mfumo wa Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuboreshwa kwa taratibu za kibiashara nchini na nchi
inapopelekwa mizigo hiyo.
Naye Kaimu Kamishina
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Lusekelo Mwaseba alifafanua faida ya mfumo
wa Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa unatarajiwa kupunguza
gharama za kufanya biashara na kuondoa urasimu wakati wa usafirishaji mizigo,
kupunguza gharama za kiutawala, kuondoa uwezekano wa rushwa na kuimarisha
matumizi ya mifumo ya mawasiliano (ICT) taktika kubadilishana taarifa miongoni
mwa nchi washirika.
Ziara hiyo
ilijumuisha Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makamishina kutoka
Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, mwenyeji Tanzania pamoja na Viongozi na
watumishi wa TPA.
No comments:
Post a Comment