Mshambuliaji kutoka nchini Uingereza na klabu ya Man Utd, Wayne Mark Rooney amewataka radhi wachezaji wenzake kufuatia adhabu ya kadi nyekundu iliyomuangukia mwishoni mwa juma wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya West Ham Utd kwenye uwanja wa Old Trafford.Rooney ambaye pia ni nahodha wa kikosi cha Man Utd, amesema hana budi kuwataka radhi wachezaji wenzake kutokana na kufahamu kwamba aliwapa wakati mgumu mara baada ya kuonyeshwa kadi nyekundi zikiwa zimesalia dakika 30 mchezo huo kumalizika.
Amesema kwa hakika muamuzi Lee Mason alikuwa sahihi kumuonyesha kadi nyekundu kutokana na kosa la kumchezea ndivyo sivyo kiungo wa West Ham Utd, Stewart Downing, hivyo hana budi kujutia na kukubali makosa aliyoyafanya.
Kuadhibiwa kwa mshambuliaji huyo kwa kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kunaashiria ataikosa michezo mitatu ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza inayofuata ambayo itashuhudia Man Utd wakipambana dhidi ya Everton, West Bromwich Albion pamoja na Chelsea.
Rooney atarejea kwenye kikosi cha Man Utd wakati wa mchezo dhidi ya mabingwa watetezi Man city ambao pia ni mahasimu wakubwa wa Man Utd mchezoa mbao utachezwa mwishoni mwa mwezi ujao.
Kadi nyekundu aliyoonyeshwa Wayne Rooney mwishoni mwa juma ni ya kwanza tangu alivyokumbana na adhabu kama hiyo mwezi Machi mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment