Na Baraka Mpenja
MBRAZIL Marcio Maximo amepoteza mechi yake ya kwanza
akiiongoza Yanga baada ya kukubali kipigo ‘swaafi’ kabisa cha mabao 2-0 kutoka
kwa Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro jioni hii.
Katika mechi hiyo ya kukata na shoka, Mbrazil mwingine,
Geilson Santos Santana ‘Jaja’ naye ameweka rekodi ya kukosa mkwaju wa kwanza wa
penalti akiichezea Yanga katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu.
Mabingwa hao wa 1999 na 2000 wakiongozwa na
mwanafunzi wa
zamani wa Maximo, Mecky Mexime, waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 15
kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Musa Hassan Mgossi.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifanya makosa
ya kumsindikiza Mgosi katika eneo la hatari akiamini kipa Deogratius Munishi
‘Dida’ ataokoa, lakini hakufanikiwa na kumpa nafasi nyota huyo wa zamani wa
Simba kuandika bao kimiani .
Yondan alishindwa kuosha mpira mrefu wa juu kwa kichwa na
kuangukia eneo ambalo si mabeki wala kipa ambaye angeweza kuokoa kiurahisi.
Licha ya Oscar Joshua kuingia kusaidia kuokoa, Mgosi alimchengua Dida aliyetoka
langoni mwake na kufungwa goli hilo.
Wakati wachezaji wa Mtibwa wakishangilia bao hilo, nyuki
walipita uwanjani hapo na kusababisha baadhi ya wachezaji wa timu zote kulala
chini ili kukwepa madhara.
Dakika ya 32 Jaja almanusura aandike bao safi kwa kichwa
akiunganisha kona iliyopigwa na Haruna Niyonzima, lakini mabeki wa Mtibwa
waliondoa mpira katika mstari wa golini na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwa ujumla dakika 45 za kipindi cha kwanza sola lilianza kwa
presha kubwa, na kushuhudia timu zote zikicheza mpira wa ‘butu-butu’.
Hata hivyo, Yanga walionekana kufika mara nyingine golini na
kupiga mashuti 5 yaliyolenga goli wakati Mtibwa walipiga 2 tu.
Yanga walionekana kutofanya vizuri sehemu ya kiungo mpaka
pale kocha Marcio Maximo alipoamua kumtoa Oscar Joshua na kumuingiza Omega
Seme.
Mabadiliko hayo yalimlazimisha Mbuyu Twite arudi sehemu ya
ulinzi wa kushoto na kumpisha Seme sehemu ya kiungo. Mabadiliko hayo yaliwapa
nguvu Yanga na kutawala sehemu ya kiungo.
Hata hivyo licha ya kutawala sehemu ya kati na kumiliki
mpira kwa asilimia 52 kwa 48 katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga walikosa mipango sehemu ya mwisho na
kukosa nafasi za kufunga.
Sehemu ya ulinzi ya Yanga haikucheza vizuri katika dakika za
kipindi cha kwanza na hii ilichangiwa na sehemu ya kiungo kushindwa kufanya
kazi yake vizuri.
Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga hawakuonekana kucheza
mpira wao uliozoeleka na walitawaliwa na viungo wa Mtibwa akiwemo Mkongwe
Shaban Nditi.
Kutokana na Yanga kufa sehemu ya kiungo, Cannavaro na
Yondani walishindwa kutimiza majukumu yao na mara kadhaa kulitokea presha kubwa
langoni mwao.
Yondani alionekana kukosa utulivu na kufanya baadhi ya faulo
ambazo kwa bahati nzuri mwamuzi hakuziona.
Kipindi cha pili, Yanga walianza mpira kwa kasi
wakishambulia kutoka upande wa kulia ambako Mrisho Ngassa alionekana kuwa
hatari zaidi.
Dakika ya 45 Ngassa alipiga krosi kutoka winga hiyo ya kulia
na ukagonga katika mkono wa nahodha wa Mtibwa, Nditi na mpira kumpata Jaja
aliyetia nyavuni, lakini mwamuzi alikataa goli hilo na badala yake kutoa
penalti.
Jaja katika dakika 46 alipewa penalti yake ya kwanza
akiichezea Yanga, lakini alikosa baada ya kipa Said Mohamed kuokoa kwa mguu
wake wa kushoto.
Dakika moja baadaye, Yanga walishambulia kwa kasi na Saimon
Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya Hamis Kiiza alitia nyavuni mpira, lakini
mwamuzi msaidizi alikataa bao hilo akidai winga huyo aliotea.
Dakika ya 51 Niyonzima alipiga mpira wa adhabu ndogo na
kuunganishwa kwa njia ya kichwa na Cannavaro, lakini ‘Mchawi’ wa Yanga leo hii,
Kipa Mohamed aliudaka mpira huo.
Dakika ya 61, Niyonzima alipiga mpira mwingine wa adhabu
ndogo uliotua kichwani kwa Jaja , lakini kipa aliokoa kwa mara nyingine.
Jaja aliyepata mipira minne mizuri, alitia kambani mmoja
lakini goli lilikataliwa na mitatu alipiga vichwa vya hatari. Hii inaonesha
mshambuliaji huyo kutoka Brazil ni mtu wa kuchungwa.
Dakika ya 69, Msuva alienda golini kwa Mtibwa na kutoa mfuko
wa ‘Gloves’ za kipa Said Mohamed ingawa haikujulikani ni kwanini.
Kwa tamaduni za soka la Tanzania, inawezekana Msuva amehisi
mfuko ule ndio unawazuia kufunga magoli. Kifupi ni kama imani za kishirikina.
Dakika ya 82 Amel Ally alipata mpira mrefu na kusumbuana na
Cannavaro akiwa na mwenzake Yondani, akatishia akapiga mpira wa juu ambapo kipa Dida alipaa juu na kujaribu kuokoa,
lakini ukazama nyavuni na kuiandikia Mtibwa bao la pili.
Goli hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambapo kwa
muda mrefu timu yao ilikuwa ikishambulia na mpira ulipopigwa hawakuwa tayari
kukuabiliana na shambulizi hilo la kushitukiza
Kwa ujumla kipindi cha pili Yanga walitawala mpira na kufika
langoni kwa Mtibwa mara nyingi zaidi, lakini mambo yalikuwa magumu.
Katika kipindi hicho, Yanga walimiliki mpira kwa asilimia 54
kwa 46, lakini haikuwasaidia kukwepa kipigo hicho kutoka kwa wakata miwa wa
Manungu Turiani
No comments:
Post a Comment