Siri ya kipigo kizito ilichokipata klabu ya Manchester
United kutoka kwa klabu iliyopanda daraja msimu huu ya Leicester City
imefichuka.
Taarifa zilizozagaa nchini Uingereza zinadai kuwa wachezaji
na viongozi wa klabu ya Leicester City walifanyiwa maombi maalumu kutoka kwa
mmoja kati ya viongozi wa dini ya Kibudha waliokuwepo uwanjani King Power
Stadium kwaajili ya kazi hiyo maalumu.
Wachezaji wa timu hiyo walifanyiwa maombi maalumu na kupewa
mikono ya baraka ambayo inaaminika ndio iliyowasaidia kuupata ushindi huo wa
kihistoria dhidi ya Manchester United kutoka kwa makasisi hao wa dini ya
Kibudha waliofanya kazi hiyo kwenye dimba la King Power Stadium.
Taarifa zinadai kuwa wafungaji wa magoli ya Leicester City
David Nugent na Jamie Vardy walivalishwa mavazi maalumu ya Kibudha mara baada
ya ushindi huo wa jumla ya magoli 5-3 wakati meneja wa timu hiyo Nigel Pearson
alishindwa kuzizuia hisia zake mara baada ya mcheazo huo pale alipokwenda
kuwakumbatia viongozi hao wa kidini ikiwa ni ishara ya kutoa shukrani kwao kwa
kuwa sehemu ya ushindi huo na kuwaambia kuwa wanakaribishwa uwanjani hapo kila
mara timu hiyo itakapokuwa inacheza ili waweze kufanya maombi hayo.
Mmiliki wa klabu hiyo ambaye ni raia wa Thailand Vichai
Srivaddhanaprabha alisafiri na viongozi hao wa kidini kutokea mashariki ya
mbali na mara alipofika nao nchini Uingereza walikwenda kwenye kiwanja cha
mazoezi cha timu hiyo na mara moja maombi maalumu yakaanza kwaajili ya mchezo
huo dhidi ya Manchester United.
Wiki moja kabla ya msimu kuanza mahema maalumu yalifungwa
kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo na viongozi hao wa kidini wakafanya
maombi maalumu kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo yenye malengo ya kuwapa
baraka ambapo inasadikika kuwa maombi hayo yameisaidia sana timu hiyo kuto
kupoteza mchezo wowote ule wa nyumbani dhidi ya vilabu vya Everton, Arsenal na
hatimaye Manchester United.
Mara baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wa ligi daraja la
kwanza nchini Uingereza (Championship) wachezaji na viongozi wa timu hiyo
walizuru kwenye eneo la Phra Maha Mondop mahali ambapo majumba ya ibada za
Kibudha kwenye mji wa Bangkok yalipo kwaajili ya kutoa shukrani kwa maombi
waliyofanyiwa mpaka wakaweza kuwa mabingwa na hatimaye kupanda daraja.
No comments:
Post a Comment