Nyumba hiyo ikiwa imeteketea kabisa.
Nyuma inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu mjini
Zanzibar, Noushad Mohammed Suleiman, iliyopo mtaa wa Kwa Kisasi barabara ya
Bububu, imeteketea kwa moto.
Nyumba hiyo yenye vyumba vitatu na msikiti, iliungua jana
jioni kutokana na hitilafu ya umeme.
Mfanyabiashara Noushad Mohamed Suleiman akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na tukio la kuungua nyumba yake.
Moto huo umeathiri vibaya nyumba hiyo, pamoja na samani zote
zilizomo ndani. Akizungumza na waandishi wa habari hizi, mmiliki wa nyumba hiyo
alisema, chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme, ambao ulianzia katika chumba
cha kushonea na baadae kuenea sehemu nyengine.
Vitu vingine vilivyoungua ni nyaraka muhimu, hati za
kusafiria za watoto wake, televisheni seti sita, friji mbili, kuka, viyoyozi
sita na samani za vyumba vyote na kumbi. Alisema thamani ya vitu vilivyoungua
bado haijajulikana.
Gari za vikosi vya zimamoto zikiwa katika eneo la tukio.
Hata hivyo, alikishukuru Kikosi cha Zima Moto na Uokozi
(KZU) pamojana wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha kuudhibiti moto huo.
Noushad ambae ni mfanyabiashara mkubwa, alisema ingawa nyumba hiyo haijakatiwa
bima, hana wasi wasi na kwamba katika kipindi kifupi atajenga tena nyumba hiyo.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto mkoa wa mjini, Ame Ali
Suleiman, alisema walipata taarifa ya moto huo kupitia simu ya mkononi majira
ya saa 10:07 za jioni na walifanikiwa eneo la tukio saa 10:17.
Vikosi vya zimamoto vya ZKU vikijitahidi kupambana na moto
huo.
Alisema waliudhibiti moto huo uliokuwa ukiwana kwa kasi
kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma. Akizungumzia changamoto walizokumbana
nazo wakati wa uzimaji moto huo, alisema hawakuwa na maji ya kutosha hali
iliyowalazimu kurudi tena mjini kufuata maji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa mjini magharibi Unguja, Mkadam
Khamis Mkadam, alisema hakuna mtu alieathirika na moto huo wala hakukua na
uhalifu wa aina yoyote ulioripotiwa. Aliwataka wanachi kuwa na tahadhari
wanapotumia vitu vya umeme, pamoja na kuhakikisha wanazima vitu vyote
wanapomaliza kutumia.
No comments:
Post a Comment