Kwa mtu anayejali, lazima atakuwa akipata vitu vinavyoweza
kumsaidia katika maisha yake ya kimapenzi anayoishi.Tunajua changamoto nyingi
zilizopo katika mambo yetu haya ya uhusiano.
Mapenzi, pamoja na utamu wake, lakini hakuna kitu hatari
kama hiki katika maisha kinachoweza kukuharibia ndani ya muda mchache kuliko
unavyofikiri.
Watu wanamwagiana maji ya moto, tindikali, kuchomwa visu na
hata kuuana kwa sababu ya mapenzi.
Na usije ukadhani wanaofanyiana hivi ni wale waliochepuka,
hapana, wakati mwingine mume anamfanyia hivyo mke wake au mke anamfanyia mume
wake.
Na kinachosababisha litokee hivi, siyo mara zote linahusiana
na mapenzi moja kwa moja, ni kitu kingine kabisa. Maana tumezoea mume au mke
kumfanyia mwenzake unyama kwa sababu labda alimfumania na mtu mwingine.
Hii inatokana na jinsi tusivyo huru kimawazo katika
kukabiliana na changamoto zinazokuja mbele yetu. Kuna kitu kimoja ambacho
wanandoa wengi na walio katika uhusiano wanashindwa kukielewa kuwa ni cha
msingi sana katika maisha yao ya kimapenzi.
Kauli ni jambo linaloonekana dogo, lakini lina madhara
makubwa sana, siyo tu katika mapenzi, bali hata katika maisha ya kawaida
tunayoishi uswahilini.
Ndiyo maana unaweza kuwa umeshasikia mara nyingi sana habari
kuwa mtu kachomwa kisu kwa deni la shilingi mia moja au hata elfu moja.
Unajiuliza mara nyingi ni vipi umuue mwenzako kwa deni dogo
kiasi hiki, lakini kumbe nyuma ya pazia ni kauli. Badala ya mdaiwa kutoa majibu
mazuri, anajibu ovyo, mtu anapandisha hasira, ibilisi anafanya kazi.
Katika mapenzi, kauli au kwa maana nyingine lugha ni silaha
kubwa sana inayoweza kuyalinda au kuyaharibu. Siku zote ni lazima uwe mtu
mwenye kuzichunguza sana kauli zako kabla ya kuzitoa kwa mwenza wako.
Katika nyakati mbaya za uhusiano wenu, kauli ndicho kitu
pekee kitakachoweza kuboresha palipoharibika au kuharibu kabisa. Unaweza
kuzungumza na kutuma ujumbe ukafika bila kutoa mapovu.
Unapotaka kukabiliana na mwenza wako, ili uende sawa ni
lazima kwanza upunguze hasira, ujiweke katika nafasi ambayo unaweza ukazungumza
na mwenzako akakuelewa. Tunachokosea sisi, tunatanguliza hasira na kauli
zisizofaa, ndiyo maana moto unazidi kuwaka.
Kwa mfano, umekuta mipira ya kiume katika mfuko wa suruali
ya mpenzi wako. Ni dhahiri kwamba hiyo si kwa ajili yako. Kama ni matumizi atatumia
na mwanamke mwingine. Ingawa hiyo ni dalili iliyo wazi kabisa kuwa mwenzako ni
mchepukaji, lakini haikufanyi kuwa na hasira na kuondoa staha katika kumkabili.
Kwanza mshukuru Mungu kwamba angalau mwenzako anajali.
Hawezi kukuletea maradhi kutoka huko kwenye michepuko yake. Lakini pia,
ukimuendea taratibu, aibu ya kibinadamu itamshika, hata kama hatasema, lakini
atajutia.
Kauli ya ukali kwa jambo kama hili, unaweza kumpa nafasi ya
kukugeuzia kibao. Nikuambie kitu, siku zote watu wakosefu hutafuta udhaifu wa
anayemhusu katika kukabiliana naye. Kama unafoka, anaweza kuondoka nyumbani
akijidai unampigia kelele na pengine akaenda kufanya kweli kabisa, ili
kukukomoa!
Ikitokea hivyo, utakuwa umekosa kujua sababu ya yeye kuja na
kondom nyumbani, ungekwenda taratibu, ungemnyima nafasi ya kuongopa, badala
yake angekuomba msamaha. Kumbuka, KAULI NI SILAHA YAKO NAMBARI ONE!
Source: habarizetu
No comments:
Post a Comment