MBUNGE WA VUNJO AMBAYE PIA NI MJUMBE WA BUNGE MAALUM LA
KATIBA, AUGUSTINE MREMA (TLP), AMESEMA KUNA HAJA RAIS JAKAYA KIKWETE AONGEZEWE
MUDA WA KUONGOZA NCHI.
Alisema kama Rais Kikwete ataongezewa muda, atapata muda wa
kukamilisha mchakato wa Katiba ambao ndiye aliyeuanzisha.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria kikao kati ya Rais Kikwete na
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kilichofanyika mwanzoni mwa wiki Ikulu
ndogo ya Kilimani mjini Dodoma, aliiambia kwamba Mrema aliyasema hayo alipokuwa
akichangia wakati wa kikao hicho.
“Wakati mjadala unaendelea, Mrema alipendekeza Rais Kikwete
aongezewe muda wa mwaka mmoja au miwili ili afanikiwe kukamilisha mchakato huu
wa Katiba.“Alipotoa pendekezo hilo, kuna
mjumbe mmoja akamuuliza, ‘sasa Mrema
unataka muda uongezwe ili na wewe upate muda wa kupambana na Mbatia (James
Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) anayekusumbua kule Vunjo au?’
“Huyo mjumbe alipouliza hivyo, Mrema akadakia na kusema,
‘hapo hapo’,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa .
Chanzo hicho kilisema kuwa Mrema aliendelea kumsihi Rais
Kikwete amzuie Mbatia asiende Vunjo kwa kuwa anapokuwa huko anatumia jina lake,
kwamba amemtuma kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Mbatia alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana juu ya
malalamiko hayo, alisema hawezi kuendelea kujibizana na Mrema kwa kuwa ni
mkubwa wake.
“Mimi sikulelewa katika mazingira ya kujibizana na wakubwa
zangu ila ninachosema ni kwamba, wakati wa mkutano wangu wa hadhara
niliohutubia Vunjo wiki iliyopita, wenyeviti 11 wa serikali za vijiji
walioshinda kupitia TLP, wenyeviti 32 wa vitongoni ambao ni wa TLP, msaidizi wa
Mrema pamoja na wanachama wapya 1,564, walihamia NCCR-Mageuzi,” alisema Mbatia.
Naye Mrema alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alikiri
kutaka Rais Kikwete aongezewe muda na kumwomba amzuie Mbatia kwenda Vunjo
akidai kuwa anatumia jina la rais kumsema vibaya kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment