Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta
amewahakikishia Watu wenye Ulemavu nchini kuwa wanatendewa haki katika Katiba
Mpya itakayopatikana.
Mhe. Sitta ameyasema hayo leo Septemba Mosi, 2014 katika
mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ambalo lilikuja katika Bunge Maalum kwa lengo la
kuwasilisha hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika
mchakato Katiba Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kazi wanayoifanya ya kuyapokea
makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la kuja na hoja mpya na
kuziwasilisha katika Bunge hilo, bali ni mawasiliano ya kawaida yanayohusu
safari kutoka Rasimu Mpya ya Katiba mpaka kufikia katika Katiba Mpya
inayopendekezwa ipatikane.
“Jambo lolote lililoandikwa na binadamu halikosi kasoro,
katika Rasimu hii ya Katiba tumegundua inayomapungufu kadha wa kadha, kuna
baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo
katika Katiba Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe. Sitta.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inclusive Development
Promoters and Consultants kutoka Dar es Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo
ambaye pia ni mwanachama wa Shirikisho hilo,amesema kuwa Kikosi cha Ushauri
kuhusu masuala ya watu wenye Ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao
ambao unajielekeza katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano ambapo
wamependekeza kuwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kuongezewe suala moja
zaidi la Nane kwa mujibu wa Rasimu ya Pili ya Katiba ambalo ni uratibu wa
masuala ya haki, usawa na fursa na uwajibikaji kwa watu wenye ulemavu kama
jambo la Muungano.
Bw. Rutachwamagyo ameongeza kuwa hoja nyingine ya msisitizo
inahusiana na suala la uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa
fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu ambayo hii ni kwa mujibu wa
Ibara ya 33 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba
mwenza wa nyongeza iliyoridhiwa kwa pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na amesema kuwa wanataka chombo hiko kijulikane kama Tume ya Kitaifa Juu ya
Haki, Usawa wa Fursa na Uwajibikaji kwa Watu wenye Ulemavu.
No comments:
Post a Comment