Moja kati ya wajumbe wa mkutano huo profesa SAFARI na mh MABERE MARANDO wakiwa hapa katika uchaguzi wa baraza la wazee,uchaguzi huo unafanyiaka jijini Dar es salaam ukumbi wa mlimani city |
Chama cha democrasia na maendeleo CHADEMA leo kimeingia katika siku yake ya kwanza ya chaguizi ndani ya chama hicho ambapo leo watafanya chaguzi ndani ya baraza la wazee la chama hicho uchaguzi unaofanyika jijini Dar es salaam.
Akizungumza na mtandao huu mwenyekiti wa baraza la wazee wa chama hicho nje ya ukumbi wa mkutano MZEE NYANGAKI SHILUNGUSHELA amesema kuwa muitikio wa wajumbe ndani ya uchaguzi huo ni mzuri ambapo wajumbe zaidi ya 90 wanatarajiwa kucshiriki katika uchaguzi huo.
Mtandao huu utakuletea yote yatakatokuwa yanajiri ndani ya chaguzi hizi za ndani za chama cha democrasia na maendeleo CHADEMA
Picha zikionyesha wajumbe mbalimbali wakiwa katika mkutano huo ambao umeanza leo jijini Dar es salaam |
Mwnyekiti wa baraza la wazee la chama cha democrasia na maendeleo CHADEMA MZEE NYANGAKI SHILUNGUSHELA akizungumza na wanahabari muda huu nje ya ukumbi wa mkutano huo wa uchaguzi.UNAWEZA KUPATA HOTUBA YAKE YOTE YA UFUNGUZI WA UCHAGUZI HUO HAPO CHINI
HOTUBA
YA MWENYEKITI WA TAIFA WA BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA MZEE NYANGAKI
SHILUNGUSHELA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA
TAREHE 6 SEPTEMBA 2014 KATIKA UKUMBI WA MLIMANI CITY DAR ES SALAAM
Waheshimiwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa,
Waheshimiwa Waasisi wa
CHADEMA mliohudhuria mkutano wa leo,
Waheshimiwa Wasimamizi
wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa,
Waheshimiwa Wawakilishi
wa Chama Taifa na Makao Makuu,
Waheshimiwa Wageni waalikwa; mabibi na mabwana:
Waheshimiwa
Wazee;
Niungane nanyi
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutukutanisha siku ya leo katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA
Taifa. Niwasalimu kwa kauli mbiu ya Baraza letu: Wazee, Hazina ya Hekima na
Busara.
Tumekutana katika
Mkutano Mkuu huu tukiongozwa na dhumuni kuu la Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa
mujibu wa kipengele cha 1.1 cha kuwa
chombo kikuu cha ushauri wa busara na hekima kinachowezesha CHADEMA kufikia na
kuendeleza madhumuni ya CHADEMA kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mkutano huu mara baada
ya ufunguzi utajadili ajenda kuu nne: Mosi, Taarifa ya Utendaji wa Baraza la
Wazee wa CHADEMA, Pili, Marekebisho ya Mwongozo wa Baraza la Wazee wa CHADEMA,
Tatu, Mpango Kazi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa mwaka 2014-2016 na Nne,
Uchaguzi wa Viongozi wa Taifa wa Baraza la Wazee wa CHADEMA.
Wajibu wangu katika
hatua ya sasa ni kufungua mkutano huu rasmi na nimeona nichukue fursa hii
kuzungumza machache kabla ya Taarifa ya Sekretariati ya Wazee ambayo itatoa
maelezo juu ya Utendaji wa Baraza la Wazee katika kipindi cha kati ya mwaka
2009 mpaka 2014 na ajenda nyingine ambazo zitatoa mwelekeo wa 2014 mpaka 2016.
Kabla ya kuendelea na
hatua hiyo, niwaomba tusimame kwa dakika moja ya ukimya kuwakumbuka Wazee
wenzetu viongozi na wanachama wa Baraza la Wazee waliotangulia mbele ya haki
katika kipindi cha tangu tulipokutana katika Mkutano Mkuu wa Wazee.
Wazee hao ni pamoja na
Hayati Mzee Mohamed Bob Makani aliyekuwa muasisi, Katibu Mkuu wa kwanza na
Mwenyekiti wa Pili wa CHADEMA, marehemu Wazee Balozi Pastor Ngaiza, Philip
Shilembi na Shida Salum waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama, viongozi na
wanachama wengine; Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema.
Waheshimiwa
Wazee;
Niwapongeze kwa
kuchaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee kwa mujibu Taratibu
za Kuongoza Baraza la Wazee wa CHADEMA kipengele 4.7.4.
Nitumie nafasi hii pia
kuwaomba mfikishe salamu zangu za pongezi kwa viongozi wote wa Baraza la Wazee
wa CHADEMA walioshinda katika ngazi mbalimbali kuanzia misingi, matawi,
kata/wadi, wilaya na Mikoa.
Hakika ushindani katika
chaguzi hizo na kiwango cha wagombea waliojitokeza kwenye uchaguzi wa ngazi ya
taifa ni ushahidi wa ukuaji wa CHADEMA na namna ambavyo wazee wanazidi kujiunga
na CHADEMA na kuwa mstari wa mbele kuwezesha mabadiliko nchini.
Hali hii inapaswa
kuendelezwa na viongozi wa kitaifa watakaochaguliwa katika Mkutano Mkuu huu.
Hali hii ni matokeo pia ya msukumo ulioongezwa na muundo wa Kanda na Programu
ya CHADEMA ni Msingi.
Hivyo, ni muhimu katika
maeneo ambayo hayajakamilisha uchaguzi ngazi ya chini, mara baada ya Mkutano
huu; nyinyi, viongozi wa kitaifa watakaochaguliwa na kwa kushirikiana na
viongozi wa ngazi mbalimbali kwenda kukamilisha chaguzi katika maeneo machache
yaliyobaki hususan katika vitongoji, vijiji na mitaa kupitia mwendelezo wa
Programu ya CHADEMA ni msingi.
Kwa mafanikio haya ya
ujenzi wa CHADEMA, napendekeza kwamba Mkutano Mkuu huu wa Wazee upitishe azimio
la kutaka Serikali kutangaza haraka uchaguzi wa Vitongoji, vijiji na Mitaa wa
mwaka 2014 kwa kuwa kuchelewa kutangazwa kwa uchaguzi huo mpaka hivi sasa
sababu mojawapo ni hofu ya CCM kushindwa katika maeneo mengi nchini.
Aidha, mafanikio haya
ni dalili njema ya CHADEMA kwa kushirikiana na
vyama vingine vya upinzani hususan vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) vya kuiondoa CCM madarakani kupitia chaguzi za udiwani, ubunge
na urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika muktadha huo,
katika kujadili Mpango Kazi wa Baraza la Wazee kwa mwaka 2014 mpaka 2016,
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee mtoe mapendekezo yatakayowezesha
kukamilisha chaguzi za wazee katika maeneo machache yaliyobaki kwenye ngazi za
misingi, matawi, kata/wadi, wilaya na mikoa ili kuwezesha ushindi katika maeneo
yote muhimu.
Pamoja na kazi hii,
anzeni kujiandaa kuhamasisha wazee kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapiga kura. Napendekeza pia Mkutano
Mkuu huu upitishe azimio la kuitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza mara moja
ratiba ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kuwa iliahidi kwamba zoezi hilo
lingeanza maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka
2014.
Kampeni za uchaguzi
zitakapoanza Mpango Kazi wa Wazee uwezeshwe uwepo wa wazee kwenye kamati za
kampeni katika vituo vya kupigia kura kuwezesha ushindi wa CHADEMA na washirika
wake katika chaguzi zote zinazofuata.
Waheshimiwa
Wazee;
Muongozo wa baraza la
Wazee wa CHADEMA kipengele 1.2 (f) unatoa jukumu kwa baraza letu kubuni mipango
na mikakati ya kuhusisha kundi la wazee ndani ya jamii kukagua, kusimika na
kuchagua viongozi bora kwenye chaguzi za ndani na nje ya chama.
Nimeweka kipaumbele
suala la uchaguzi kwa kuwa tupo katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa ndani ya
CHADEMA unaofanyika ikiwa ni takribani mwezi mmoja kutoka kuanza kwa kampeni
za uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na
Mitaa wa mwaka 2014 na mwaka mmoja kutoka katika kampeni za uchaguzi mkuu wa
udiwani, ubunge na urais wa mwaka 2015. Nimeweka kipaumbele suala la uchaguzi
kwa kuwa nchi yetu ipo kwenye mkwamo wa mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Wakati sisi tunapokutana
hapa, Bunge Maalum linaendelea kupokea taarifa za Kamati mbalimbali huku
wanaojiita walio wengi katika Bunge hilo wa CCM na vibaraka wao wakiendelea
kupuuza maoni ya wananchi na kubomoa misingi ya rasimu iliyowasilishwa na tume
ya mabadiliko ya katiba.
Natambua kwamba rasimu
ya katiba itayopendekezwa hatimaye itakuja kupigiwa kura ya maoni ambao hao
wanaojiita walio wengi wa CCM katika Bunge Maalum watakutana na wananchi walio
wengi waliotoa maoni yao.
Hata hivyo, Baraza la
Wazee wa CHADEMA ni muhimu kupitia mkutano mkuu huu lipitishe azimio la kulaani
hatua ya Wazee wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum Samuel Sitta na
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutoa uongozi wa kunusuru fedha
za umma kuendelea kutumika huku kukiwa hakuna muafaka wa kitaifa kwenye
mchakato.
Kwa upande mwingine, nashauri
Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA upitishe azimio la kuwapongeza Wazee
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti
Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba na wajumbe wake akiwemo mzee mwenzetu mteule
kupitia CHADEMA Prof. Mwesiga Baregu kwa kuheshimu maoni ya wananchi na
kuzingatia sehemu kubwa ya maoni hayo katika rasimu ya pili ya katiba
iliyowasilishwa.
Waheshimiwa
Wazee;
Muongozo wa Baraza la
Wazee kipengele cha 1.2 (a) kimetoa jukumu kwa Baraza la Wazee wa CHADEMA kuwa
chombo cha ushauri ngazi mbalimbali za chama. Wajibu huu ni wa baraza na wazee
wanachama wa baraza letu. Kwa kuzingatia wajibu huo, nimeshiriki kwa niaba yetu
katika vikao vya kamati kuu kwa nyakati mbalimbali na katika vikao vya kupanga
mikakati ya chama kwa miaka kadhaa.
Kati ya masuala ambayo
vikao hivyo vimekuwa vikiyapa kipaumbele ni mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Wazee ni hazina ya
hekima na busara. Hivyo, ushauri wangu mara nyingi umekuwa ni kwa CHADEMA
kuwezesha maridhiano, usuluhishi na utatuzi wa migogoro inayojitokeza kwenye
mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Hata hivyo, katika hali
ambayo imefikia ya mgogoro baina ya CCM kwa upande mmoja na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wananchi walio
wengi waliotoa maoni yao kwa upande mwingine; na kuvunjika kwa mazungumzo
yaliyoongozwa msajili wa vyama vya siasa nashauri viongozi wa CHADEMA na UKAWA
nashauri wachukue tahadhari kubwa katika mazungumzo na Rais.
Waheshimiwa
Wazee;
Kitendo cha Bunge
Maalum kuendelea mpaka hivi sasa hata baada ya kuanza mazungumzo ya Rais na
vyama yanayoratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) inaweza kuwa ni
mchezo wa CCM na Serikali kuchelewesha maridhiano huku wajumbe wake wakiendelea
‘kuchakachua’ rasimu ya katiba kinyume
na maoni ya wananchi.
Hivyo, tarehe 8
Septemba 2014 iliyotangazwa na Ikulu kuwa ni mwendelezo wa mazungumzo na Rais
inapaswa kuwa nafasi ya mwisho iwapo Bunge Maalum halitasitishwa au kuahirishwa
ni muhimu viongozi wa taifa wa CHADEMA wakashauriana wenzao wengine wa UKAWA kufanya maamuzi ya
kuwaunganisha wananchi kwa nguvu ya umma kuchukua hatua kwa CCM na Serikali.
Mwelekeo unaonyesha
kwamba wazee wa CCM ndani ya chama hicho, Bunge Maalum, Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Serikali za pande zote
mbili za Muungano wameamua kusaliti maoni ya wananchi na matakwa ya kikatiba
kwamba mamlaka na madaraka ni ya wananchi.
Katika muktadha huo,
ufumbuzi endelevu ni kuiondoa CCM madarakani na kuweka uongozi bora na chama
kitakachokuwa na dhima ya kuleta sera
sahihi, mikakati makini na oganaizesheni
makini katika mchakato wa mabadiliko ya katiba na maendeleo ya nchi.
Mabadiliko ya Katiba
sio mchakato wa kuchukuliwa kwa mzaha.
Ni mchakato unaohusu maisha ya wananchi na mustakabali wa nchi. Pamoja na CCM
kukataa maoni ya msingi ya wananchi juu ya muundo wa muungano wa Shirikisho la
Serikali tatu, chama hicho kupitia wajumbe wake wanaojiita walio wengi kinapinga
maoni ya wananchi yaliyoingizwa kwenye rasimu ya katiba ikiwemo uadilifu, uwazi
na uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za taifa.
Kwa kuzingatia maoni
hayo, CCM na wajumbe wake wanaojiita walio wengi hawana uadilifu, uwazi na
uwajibikaji wa kuweza kusimamia masuala ya msingi yanayohusu wazee katika
rasimu ya katiba ikiwemo ya kuhakikisha kwamba hifadhi ya jamii hususan
pensheni inatolewa kwa wote (universal social security particularly pension).
Waheshimiwa
Wazee;
Masuala na maslahi ya
wazee chini ya chama kinachotawala sasa yamekuwa yakipewa kipaumbele kwenye
ahadi badala ya kuwekwa katika utekelezaji. Matokeo yake ni migogoro ya wazee
kama ambavyo inajitokeza kwa nyakati mbalimbali kwa wazee wanaodai mafao yao.
Taarifa ya utendaji ya
sekretariati itaeleza namna ambavyo Baraza la Wazee wa CHADEMA limekaa na wazee
wenye madai mbalimbali ikiwemo wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Katika maboresho ya Mpango Kazi 2014 mpaka 2016 natarajia wazee
wajumbe wa mkutano huu mtatoa mapendekezo ya namna ya kuwezesha Baraza letu
kuongeza msukumo katika kuwawakilisha na kuwatetea wazee nchini.
Kilio cha wazee wengi
kimekuwa ni umaskini na hali ngumu ya maisha kutokana na wenye kupata pensheni
kupata kiwango kidogo kwa waliokuwa waajiriwa katika sekta rasmi na wengi zaidi
kutokuwa kabisa na pensheni baada ya kustaafu kwao hasa wakulima na wazee
waliotumikia taifa katika sekta isiyo rasmi.
Kwa nyakati mbalimbali
katika siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi kati ya mwaka 2009, 2010, 2011, 2012
na 2013 Serikali imekuwa ikiahidi kutoa pensheni kwa wazee wote nchini; hata
hivyo hakuna mwaka mpaka sasa ambao bajeti imetengwa kuwezesha utekelezaji.
Wanachama wa Baraza la Wazee wa CHADEMA wamekuwa wakifuatilia suala hili
ikiwemo kupitia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Ahadi za uongo zimekuwa
zikitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mawaziri wengine kuhusu suala hili.
Nitoe mwito kwa viongozi wa wazee kutoka mikoa mbalimbali mlioshiriki mkutano
huu kuanza maandalizi mara baada ya kurejea katika maeneo yenu ili kuziunganisha
ngazi zenu na za chini yenu katika maadhimisho ya siku ya wazee kwa mwaka huu
Oktoba Mosi, 2014 ujumbe ufike kwa watawala kwamba wazee wamechoka kudanganywa
na wako tayari kuunga mkono mabadiliko kuchangua uongozi ambao utatekeleza
ahadi kwa vitendo.
Wazee wanaweza
kuendelea na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi wakiwa na mazingira
bora. Hivyo, katika Mkutano huu Taarifa
ya Sekretariati ya Baraza la Wazee itawajulisha hatua iliyofikiwa katika
mchakato wa kuboresha Sera ya Wazee ya CHADEMA. Nawahimiza kushiriki katika
kushiriki michakato yote ya sera mbalimbali zenye kuwagusa wazee kwa namna au
nyingine zitakazotekelezwa na CHADEMA kitakapoongoza Serikali.
Waheshimiwa Wazee;
Nimalizie kwa
kuwakumbusha majukumu ya msingi ya Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa mujibu wa
muongozo kipengele 1.2 (b), (c) na (j) ya kuwa chombo cha utatuzi na usuluhishi
wa migogoro ndani ya chama ama baina ya viongozi, kuwa chombo cha kupatanisha
na kuunganisha viongozi na kushauri viongozi wa CHADEMA katika ngazi mbalimbali.
Katika mkutano huu
mtapokea mapendekezo ya maboresho na marekebisho ya muongozo wa Baraza la Wazee
wa CHADEMA katika maeneo na masuala mbalimbali. Pendekezo langu jipya ni kuhusu
jina la Baraza letu; kumekuwa na changamoto ya kutafuta kifupi cha Baraza hili
kuweza kutofautiana na Baraza la Wanawake wa
CHADEMA (BAWACHA). Kumekuwepo pia na ombwe la kutokuwa na Baraza la
Wazee katika taifa letu.
Hivyo, pendekezo langu
ni kuwa tujitambulishe kama Baraza la Wazee tu. Baraza la Wazee (BAWA) litabeba
sura ya utaifa litaendelea kuwa la kitaifa. Jumuiya ya Wazazi ya CCM imeendelea
kujitambulisha kama JUWATA ikighilibu wazazi nchini. Umoja wa Wanawake wa CCM,
umeendelea kujitambulisha kama UWT ukihadaa wanawake kuwa ni chombo cha wote.
Baraza la Wazee (BAWA) sio tu libebe taswira ya wazee nchini, bali lionyeshe
kwa vitendo kuwakilisha na kutetea wazee nchini mpaka pale wazee watakapokuwa
na chombo chao cha kuwaunganisha wote bila kujadili tofauti mbalimbali.
Katika kujadili
mapendekezo hayo, na katika kutekeleza muongozo huo kumbukeni kuwa pamoja na
kuwa wanachama na vikao vya kawaida vya ngazi mbalimbali. Mkazo uwekwe katika
kuunda “Caucus ya Wazee” katika ngazi zote. Hili ni kundi maalum la kushauri
viongozi wa kuanzia ngazi za msingi hadi taifa. Hili ni kundi la wazee wateule
wenye busara na hekima lukuki, wanaokubalika na kuheshimika katika jamii na wenye kupatikana mara kwa mara kutoa
ushauri. Kwa kufanya hayo mtakuwa mnatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Baraza
la Wazee wa CHADEMA: Wazee; Hazina ya Hekima na Busara. Na kwa kauli mbiu hiyo,
natangaza kwamba Mkutano Mkuu huu umefunguliwa rasmi.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki CHADEMA,
Mungu wabariki Wazee.
No comments:
Post a Comment