Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamesema wala
rushwa pamoja na wahujumu uchumi adhabu yao iwe ni kunyongwa.
Wametaka Katiba mpya
inayoenda kuandikwa itamke hivyo ili kufanya viongozi wa kisiasa kuogopa kama
ilivyo kwenye nchi nyingine.
Sababu ya wajumbe hao kupendekeza jambo hilo ni kwamba
uhujumu uchumi na rushwa nchini limekuwa tatizo kubwa kwa viongozi.
Kutokana na ukiukwaji huo wa maadili, wamesema
umefika wakati wa kuweka bayana suala hilo
kwenye sheria mama.
Miongoni mwa waliochangia ni Paul Makonda aliyesema suala hilo likiwekwa
bayana, litaokoa fedha nyingi za walipa kodi ambazo kwa sasa baadhi ya viongozi
wanazichota na kwenda kuzihifadhi nje ya nchi.
Pia alipinga kuruhusu viongozi wa nchi kufungua akaunti nje
ya nchi. “Kwa nini viongozi hao washindwe kuhifadhi fedha zao ndani ya nchi,
wanafanya biashara gani hadi wakafungue benki nje ya nchi?
“Tusiruhusu jambo hili na napendekeza kwamba kiongozi
atakayebainika amekula rushwa na kuhujumu uchumi huyo anyongwe,” alisema
Makonda.
Yusuf Singo pia alisema maadili yanazidi kuporomoka kwa
viongozi, jambo linalorudisha nchi
nyuma. Alitaka Katiba isisitize maadili kwa kada hiyo na ambao watakiuka
wanyongwe.
Alitoa mfano wa Japan kuwa kiongozi wa kisiasa
anapochunguzwa kwa kujihusisha na rushwa anatoa machozi kwa sababu hajui hatima
yake. “Tunataka na sisi ifike wakati kiongozi akianza kuchunguzwa atoe machozi,”
alisema.
Dk Mary Mwanjelwa katika mchango wake alisema rushwa imekuwa
adui mkubwa wa maendeleo ya Watanzania. Alisema isipopingwa kuanzia kwenye
Katiba, nchi itakuwa inajichora.
Alisema Bunge halitaeleweka kama halitaweka jambo hilo
kwenye Katiba, kwa sababu wananchi wengi wameteseka ndani ya nchi yao kwa
sababu ya rushwa.
Alisema pia wapo viongozi wengi wasio na maadili na ndiyo maana wanajihusisha na vitendo vya
rushwa.
Kwa upande wake, Profesa Mark Mwandosya alisema tatizo la
rushwa haliwezi kutenganishwa na haki za binadamu kutokana na kukosesha
wananchi maendeleo.
Profesa Mwandosya alisema Katiba lazima itambue adui wa haki
za wananchi ni rushwa.
Alipendekeza suala hilo litambulike kikatiba na serikali
zote mbili zitunge sheria kali za kupambana na rushwa kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za
msingi bila kutoa wala kupokea rushwa.
Naye Gerison Lwenge
alisema Katiba itambue jambo hilo na ikemee vikali kwa wanaotoa na wale
wanaopokea.
Alisema kwa ahli ilivyo, wanaobanwa zaidi ni wale ambao
wanapokea na akapendekeza sheria kali zitungwe kubana pia wanaotoa.
Alishauri Kamisheni isimamie suala hilo la rushwa badala ya
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kwa mujibu wa Lwenge, Kamisheni ni chombo kikubwa zaidi
kuliko ilivyo kwa taasisi. Alisema kazi yake itakuwa ni kuzuia zaidi na si kutibu pekee.
Jesca Msambatavangu alisema Takukuru wanafanya kazi vizuri
na walishindwa kupambana na rushwa kwa vile hawana uhuru wa kutosha.
Alisema kama Takukuru wakipewa meno kupitia Katiba mpya,
watashughulika kwa uhuru zaidi katika kupambana na tatizo la rushwa nchini.
No comments:
Post a Comment