Na Felix Mwagara
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amewataka Wakimbizi wa Kambi ya Nyarugusu kuacha mara
moja tabia ya kuwaozesha watoto wao wenye umri mdogo kwani tabia hiyo
inawaletea matatizo makubwa watoto wao wakati wanapojifungua.Akizungumza na
mamia ya wakimbizi hao katika Ukumbi wa Mikutano katika kambi hiyo iliyopo wilayani Kasulu,
Mkoa wa Kigoma, Waziri Chikawe alisema katika maisha yake, yeye ni
mpambanaji
wa kupinga ndoa za utotoni ambazo zinawaletea madhara makubwa watoto.Chikawe
alifafanua kuwa, tabia hiyo inayofanywa na wakimbizi hao dhidi ya watoto wao
inawasababishia watoto hao kupatwa na matatizo makubwa kipindi wanapojifungua
kwani viungo vyao vya uzazi havipo tayari kwa ajili ya kuzaa hivyo aliwataka
familia za wakimbizi hao kuacha tabia hiyo ya kikatili dhidi ya watoto wao na
pia inawakosesha haki zingine za msingi watoto hao.
“Wapeni haki zao watoto wenu, utamaduni huu sio mzuri wa
kuwaozesha watoto wadogo, mnatakiwa kuuacha na kuulaani kwani mkifanya hivyo
mtakuwa mnawaletea matatizo makubwa watoto wenu hasa wanapojifungua,” alisema
Chikawe.
Aidha, Waziri Chikawe aliwataka wakimbizi katika kambi hiyo
kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi kwani ugonjwa huo unaendelea kuua maelfu ya
watu duniani na pia bado hauna dawa, na kuwataka wakimbizi hao kuacha tabia ya
ufuska na endapo watashindwa basi watumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na
ugonjwa huo hatari.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole, aliwaonya wakimbizi
hao kuacha tabia hiyo ya kuwaoza watoto wao ambao wapo chini ya miaka 18 kwani
kwa kufanya hivyo Wakimbizi hao watashindwa kupata nafasi ya kwenda nchini
Marekani.
“Si mnajua tunawaandaa kwenda Marekani?, kama mnalijua hilo
basi endapo mkimbizi yeyote akimpa mimba mtoto mdogo basi hataweza kupata
nafasi ya kwenda nchini humo, hivyo kuweni makini ili muweze kwenda nchini
Marekani,” alisema Joyce.
Zaidi ya wakimbizi 30,000 wa Kambi ya Nyarugusu wanatarajiwa
kuhamishiwa katika nchi ya Marekani kuanzia mwaka 2015.
Waziri Chikawe ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa
Idara ya Wakimbizi nchini, Harrison Mseke pamoja na maafisa wengine wa wizara
yake, amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Kigoma ambapo katika siku
hizo alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma.
Pia alikitembelea Kituo cha Mpito cha Wakimbizi (NMC)
kilichopo mjini Kigoma na baadaye akamalizia ziara yake katika Wilaya ya Kasulu
mkoani humo kwa kuitembelea Kambi kubwa ya wakimbizi ya Nyarugusu
inayowahifadhi wakimbizi zaidi ya 60,000 ambapo wengi wao wakiwa ni kutoka
nchini Kongo, Burundi na wachache kutoka
mataifa mengine.
No comments:
Post a Comment