Moja ya nyumba zilizoteketezwa katika Kijiji cha Murufiti
ambapo watu saba waliuawa kwa kuchomwa moto. Picha na Diana Rubanguka.
Na Diana Rubanguka na Antony Kayanda, Mwananchi
Kigoma. Watu saba wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba
katika tukio ambalo nyumba 18 ziliteketezwa na mbili kubomolewa na wananchi
waliodai wanawaua wachawi katika Kijiji cha Murufiti, Kasulu, mkoani Kigoma.
Polisi wameeleza kuwa tayari watu 17 wamekamatwa kwa
kuhusika kwenye tukio hilo.
Miongoni mwa waliouawa katika tukio hilo lililotokea
Jumatatu iliyopita ni John Mavumba (68) na mkewe Elizabeth Kaje 55 ambao pamoja
na wenzao walikuwa wakituhumiwa kuwa ni washirikina.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Josephat John
ambaye ni mtoto wa Mavumba, alisema wazazi wake walichomwa moto na kundi la
vijana waliokuwa wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Alisema vijana walikuwa wamebeba mapanga, marungu na kupita
katika nyumba mbalimbali wakifanya mauaji wakisema maneno kwa kurudiarudia
kwamba watawamaliza wachawi kwa kuwaua, ndipo yeye na wenzake walikimbia usiku
huo wakihofia kuuawa.
“Niliporudi alfajiri niliukuta mwili wa mama ukiwa umbali wa
mita 10 kutoka ilipo nyumba yetu ukiwa umeungua na mwili wa baba ukiwa umeungua
ndani ya nyumba,” alisema John.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed alisema
mauaji hayo yalitokea Oktoba 6 kuanzia saa 4:00 usiku katika kijiji hicho.
John alisema baada ya tukio hilo wanaume wengi wameyakimbia
makazi yao wakihofia kuuawa na kundi la vijana hao. “Kijiji kimebaki na
wanawake tu, wanaume wamezikimbia nyumba zao wanahofia kuuawa,” alisema.
Mohamed alisema mauaji hayo yametokana na imani za
kishirikina.
Aliwataja waliouawa kuwa ni John Muvumba (68), Elizabeth
Kaje (55), Dyaba Kitwe (55), Vincent Ntiyaba (42), Herman Ndabiloye (78),
Redempta Mdogo (60) na Ramadhan Kalaliza (70) wote wakazi wa kijiji hicho.
Alisema nyumba zilizochomwa moto ni 18, mbili zilibomolewa
na kufanya jumla ya nyumba 20 zilizoharibika kabisa.
Wakazi wa kijiji hicho, Zablon Andrew na Eveline Enock
walisema kwa nyakati tofauti kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mganga wa jadi
aliyefika kijijini hapo na kupiga ramli akiwataja watu waliouawa kuwa ni
wachawi.
Andrew alisema baada ya mganga huyo kuwataja, vijana
walikusanyana na kuanza kuwateketeza watu bila huruma.
“Kitendo hiki kimeturudisha nyuma kimaendeleo kwa sababu
nyumba zetu zimechomwa moto na mazao yetu yameharibiwa,” alisema Andrew.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watu aliyechomewa nyumba, Evelyne Msilu alisema
sasa kijiji hicho kina askari wengi wanaofanya doria.
“Hali inasikitisha, tumepoteza ndugu zetu waliouawa, wanaume
wengi wamekikimbia kijiji kwa hofu ya kuuawa na vijana wengine wamekimbia
wakiogopa kukamatwa,” alisema.
Kwa nini ipigwe ramli?
Akisimulia, Enock alisema kuna kijana mmoja katika kijiji
hicho ambaye kazi yake ni kufyatua matofali aliwaomba vijana wanzake kuwa siku
inayofuata wamsaidie kuyapanga katika tanuru.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba walipoamka asubuhi walikuta
matofali yamekwishapangwa na haikujulikana aliyefanya kazi hiyo.
Alisema kijana huyo na wenzake waliamini kwamba waliofanya
kazi hiyo ni wachawi.
Akisimulia kisa kingine, Enock alisema siku chache
zilizopita kuna msiba ulitokea kijijini hapo na baada ya mazishi, siku
iliyofuata walikuta msalaba umeng’olewa na haujulikani ulipo, jambo ambalo pia
lilihusishwa na ushirikina.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ogen Gasper aliyeomba
Serikali kujenga kituo cha polisi kijijini hapo, alisema baada ya kupata
taarifa za tukio hilo alifanya jitihada kubwa kuwapata askari, lakini hawakufika
kwa kilichodaiwa ni kukosa usafiri.
Gasper alisema hilo ni tukio la tatu kwa watu kuuawa kwa
kutuhumiwa kuwa ni wachawi, la kwanza likiwa limetokea mwaka 1996.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment