Dira ni kuwa na katiba bora itakayojenga Tanzania yenye
demokrasia ya kweli, uhuru wa kweli na maendeleo endelevu kwa watu wake wote.
Lakini uharamia katika mchakato wa katiba mpya umelipasua taifa. Mpasuko huu
unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au mgogoro chanya utakaoleta
mabadiliko nchini.
Maharamia wanashangilia kilevi katika Bunge Maalum baada ya
kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata theluthi
mbili kwa
njia za kiharamia. Katiba iliyopendekezwa kiharamia na kudharau maoni
ya wananchi ni katiba haramu iliyokosa maridhiano na muafaka wa kitaifa.
Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi,
katiba ya CCM wahafidhiana na mawakala wake inapaswa kupingwa mtaani na
mahakamani kwa mbinu mbalimbali.
Iwe ni kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika
sanduku la kura. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya
katiba ni mwanya wa mabadiliko katika taifa letu.
Theluthi mbili ilianza kutafutwa tangu wakati wa kutungwa
kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, tulipinga muundo wa Bunge Maalum na uteuzi
wake; madhara yake yamedhihirika sasa.
Rais Kikwete akaongezea udhaifu huo kwa kutumia madaraka
vibaya kuteua wanaCCM mahafidhina na mawakala wao kwa wingi katika uteuzi wa
wajumbe wa kundi la 201 kuongezea katika hodhi haramu ya wabunge na wawakilishi
wa chama chake.
Sitta akakamilisha uharamia huo kwa marekebisho haramu ya
kanuni za Bunge Maalum ambayo yaliruhusu kura kupigwa nje ya Bunge hilo na
mianya mingine ya wizi wa kura.
Jana Oktoba Mosi Sitta alilalamikia hatua yangu ya kumtaja
yeye, Chenge na wenzake kuwa ni ‘maharamia’ dhidi ya rasimu iliyotokana na
maoni ya wananchi. Kwa kuwaita maharamia Sitta amelieleza Bunge Maalum kuwa ni
“siasa za kichuo chuo” na kwamba “hatuwezi kushika madaraka kwa mbinu za kitoto”.
Nimkumbushe Sitta na maharamia wenzake kwamba mwaka 1958
Mwalimu Julius Nyerere alishtakiwa kwa kuwaita ‘mashetani na maharamia’ wakuu
wa wilaya wa Serikali ya mkoloni. Ninapolitazama Bunge Maalum nakumbuka utetezi
wake mahakamani wa kukiri kutamka maneno hayo kwa lengo la kuitaka serikali ya
kikoloni itupie macho malalamiko ya watu.
Sitta na maharamia wenzake kama wameshindwa hata kuelewa
waraka wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa
kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Leo Sitta, Samia Suluhu na maharamia wengine wanasherehekea
kama walevi ushindi wa muda mfupi walioupata kwa njia za kiharamia ikiwemo kwa
kuwashinikiza na kuwarubuni baadhi ya wajumbe kuhalalisha rasimu haramu. Andrew
Chenge aliyetajwa kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) ndiye aliyeongoza
kazi hiyo kuanzia katika Kamati ya Uandishi.
Uharamia huu dhidi ya rasimu ya tume ya mabadiliko ya katiba
na maoni ya wananchi unapaswa kuwa kiunganishi kwa umma kutambua kwamba umoja
wa ukweli na uadilifu unapaswa kuvuka mipaka ya vyama, dini, pande mbili za
Muungano na tofauti zingine.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeonyesha msimamo wake,
Mwenyekiti na Wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wameonyesha
msimamo wao, baadhi ya viongozi wa dini wameonyesha msimamo wao, baadhi ya
wanaharakati wameonyesha msimamo wao, baadhi ya wajumbe ndani ya Bunge Maalum
wameonyesha msimamo wao; wewe je?
Namna pekee ya kuirejesha rasimu ya katiba ya wananchi
katika hali iliyofikia ni kuikataa katiba haramu na kuwakataa wote waliofanya
uharamia kuwezesha rasimu hiyo kupendekezwa na wote watakao itetea katiba hiyo.
Muasisi wa CCM alikiambia chama hicho mwaka 1995 kwamba
“watanzania wanataka mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya
CCM”. CCM imepoteza mwanya wa kuwapa watanzania mabadiliko kutoka ndani ya
chama hicho.
Uharamia uliofanywa katika Bunge Maalum una baraka za Katibu
Mkuu wa CCM Kinana na Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete. Uharamia huo ulilenga
kuwezesha Maoni ya CCM yaliyopitishwa na vikao vya juu vya CCM kinyume na maoni
ya wananchi. Hatimaye kwa njia za kiharamia wajumbe wanaojiita walio wengi wa
CCM wamepitisha katiba haramu iliyopendekezwa.
Mwalimu Nyerere aliandika katika kitabu cha Uongozi Wetu na
Hatma ya Tanzania kwamba Rais wa wakati huo Mwinyi alikuwa mtu mwema na mpole
lakini “kiongozi dhaifu”. Akamtakia heri na kuomba asaidiwe amalize kipindi
chake salama. Akatabiri kwamba chini ya CCM na uongozi wake mbele ni giza
tororo.
Rais Kikwete alithubutu kwa kukubali mchakato wa mabadiliko
ya katiba kuanza lakini ameshindwa. Na kwa udhaifu alio uonyesha, kwa vyovyote
vile mchakato huu hauwezi kusonga mbele na kukamilika chini yake.
Udhaifu pekee anao weza kuupunguza kwa sasa ni kusimamia
marekebisho ya 15 ya Katiba ya mwaka 1977 kuwezesha uchaguzi huru na haki
katika uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais mwaka 2015 na kuendelea kwa
mchakato wa katiba mpya mwaka 2016 kwa kuzingatia maoni ya wananchi. Tumtakie
heri Rais Kikwete amalize kipindi chake salama; matokeo ya kura ya katiba
haramu iliyopendezwa yatafutwa kwa kupingwa mahakamani ama kwa njia nyingine.
Mahakama kwa kukosa uhuru wa kikatiba isipotimiza wajibu huo
wa kusimamia haki kwa wakati; katiba haramu iliyopendekezwa itafutwa kwa sheria
maalum itayotungwa na Bunge litakaloongoza nchi baada ya uchaguzi 2015. Ikiwa
watawala wa sasa au wa wakati huo watalazimisha katiba haramu kwenda kupigiwa
kura ya maoni, ni wazi itapigiwa kura ya hapana na wananchi iwe ni mwaka 2015
au 2016.
Mabadiliko yatafutwe kwa kuwakataa watetezi wote wa katiba
haramu kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka
2014. Mabadiliko yatafutwe kwa kutaka Tume itangaze ratiba ya uandikishaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2014 ili kila mwenye umri wa kupiga kura
ashiriki kufanya mabadiliko kupitia uchaguzi 2015 na kura ya maoni.
Kwa wajumbe mlioshiriki kuandika katiba haramu, naheshimu na
nakubaliana na maneno ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba kwamba tutakutana mtaani. Dhima ni kuwa na katiba
mpya itayoleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na Muungano na Muundo
wa Utawala thabiti kwa maendeleo endelevu. Nyinyi mkiwa na katiba haramu sisi
tutakuwa na rasimu ya wananchi; sauti ya watu, ni sauti ya Mungu hivyo umma
utaamua na historia itatoa hukumu kwa maharamia na walevi wa madaraka.
No comments:
Post a Comment