Muungano wa Ukawa dhidi ya CCM, ni matokeo ya misuguano
iliyojiri wakati wa mchakato wa Katiba. Hatua ya kwanza ilianza kwa Mbowe
kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli, likiwashirikisha wabunge kutoka vyama hivyo
isipokuwa NLD ambacho hakina mwakilishi bungeni.
Wakosoaji
Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), Kapteni John Komba alisema
ushirikiano huo ni feki na unalenga katika masilahi binafsi na kwamba hauwezi
kukiyumbisha chama chake. Pia alisema kukosekana kwa wanawake wa kutosha kwenye
mkutano huo wa juzi ni dalili tosha ya anguko la Ukawa.
“Ukiona wapinzani wanaungana ujue wamegundua nguvu ya kila
mmoja wao haitoshi kuing’oa CCM, lakini swali la msingi kujiuliza ni je,
muungano huo utaleta tija inayokusudiwa? Watasambaratika baada ya muda mfupi na
masilahi binafsi pamoja na itikadi tofauti ndizo zitakazochangia,” alisema
Komba.
Komba alisema aliangalia mkutano huo kupitia runinga lakini
alishangazwa na idadi ndogo ya wanawake waliohudhuria na kusema kuwa hiyo ni
ishara kuwa kinamama hawaukubali umoja huo.
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Hili si
jambo jipya kwa kuwa lilishawahi kutokea lakini baada ya kuona halina maana
wengine tuliamua kujitoa… tumekaa pembeni tuone watakapofika.
“Huko mbele ni lazima watakorofishana hasa litakapokuja
suala la masilahi. Inaeleweka wazi kuwa chama chenye wawakilishi wengi ndicho
kinapata ruzuku. Kusimamisha mgombea wa urais pekee ina maana kubwa kwa kila
chama, sijui kama wameweka wazi utaratibu wa kugawana ruzuku itakayopatikana
kwa chama kitakachostahili.”
Mziray alibainisha kuwa anakumbuka vizuri ushirikiano
uliokuwapo kati ya Chadema na Mchungaji Christopher Mtikila ambaye baada ya
kukiunga mkono chama hicho hakuambulia chochote.
Kwa upande wake, Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa DP
aliuponda muungano huo akisema: “Nililetewa mwaliko wa kuhudhuria mkutano
uliofanyika juzi kutoka kwa mratibu wa Ukawa, ambaye simjui. Siwezi kwenda huko
kwa sababu wakati wanaanzisha Ukawa ilikuwa ni Umoja wa Katiba ya Watanganyika
na si kama wanavyoieleza.”
Alidai kwamba ndiye aliyeanzisha mchakato wa kudai Katiba ya
Watanganyika baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge Maalumu la Katiba
lakini baada ya Chadema kuchukua hatamu za kuongoza harakati hizo alijiweka
pembeni.
Wabunge wa upinzani
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema
nafasi za uongozi katika ushirikiano wa Ukawa zipo wazi kwa kila mwanachama,
hivyo ushindani utahusisha wote walio tayari kushindana.
“Jimbo si mali ya mbunge aliyepo, kitakachoendelea kumweka
madarakani ni uchapakazi wake licha ya kuungwa mkono na Ukawa. Yapo maeneo
yanatambulika kuwa ni ngome za vyama fulani vya upinzani huko, tutaunga mkono
ili kupata ushindi mkubwa zaidi. Katika maeneo ambayo CCM wanaongoza juhudi
binafsi ndizo zitakazotumika kumpata mpinzani atakayeungwa mkono na wote.”
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Barwan Salum alisema historia
inaonyesha kuwa vyama vya upinzani vinaongoza katika maeneo tofauti na kwamba
juhudi hizi zinalenga kuwanufaisha wananchi.
“Chadema ina nguvu kubwa Kaskazini mwa nchi wakati
NCCR-Mageuzi ikiongoza Magharibi na CUF wanafanya vizuri Visiwani. Katika
chaguzi zilizopita, takwimu zinaonyesha kuwa vyama vya upinzani kwa jumla wake
vilikuwa vinapata asilimia 40 ya nafasi zote. Umoja huu unamaanisha makubwa
katika siasa za nchi hii.”
Wananchi
Mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam, Hamis Suleiman (72),
alisema muungano huo ni mwamko mpya wa siasa nchini kwani hakuwahi kufikiria
kuwa kuna siku wapinzani watakuja kuonyesha mshikamano mkubwa kiasi hicho
katika kupigania masilahi ya taifa.
“Ni kitu kipya katika historia ya Taifa letu. Wakati tunadai
uhuru iliwezekana kuona mambo haya lakini kwa sasa naona harakati hizo
zinafanywa kudai utawala bora na usawa kwa wananchi wote,” alisema Suleiman.
Mkazi mwingine, Deogratius Bikongoro alisema hakuamini kama
wapinzani wanaweza wakafanya kitu kikubwa kama hicho, tena hadharani na kwamba
alishawishika kwenda kwenye mkutano huo ili aweze kujiridhisha.
“Nimejifunza elimu ya uraia katika tukio hili. Kumsikiliza
Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu wakifafanua Katiba Inayopendekezwa pamoja na
sheria za nchi kwa jumla, imenipa ufahamu wa mambo mengi niliyokuwa siyajui
lakini nimeona dhamira ya wapinzani sambamba na mwitikio wa wananchi. Mkutano
huu unatoa picha kuwa hata huko mikoani kuna watu ambao hawajaridhika na jinsi
mchakato wa Katiba ulivyokwenda,” alisema.
Mmoja wa waasisi wa Chadema, Victor Kimesela alisema
mchakato wa kuunganisha vyama vya upinzani ulianza siku nyingi kutokana na
mahitaji ya wananchi… “Wananchi watanufaika kutokana na muungano huu ambao
unaunganisha juhudi tofauti zinazoletwa na itikadi mtambuka.”
Alisema juhudi za kuunganisha vyama zimepitia hatua nyingi
na kuzitaja kuwa ni pamoja na kuundwa kwa Umoja wa Demokrasia Tanzania (Udata)
na Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (Kamaka) na kusisitiza kuwa Ukawa ndiyo
hitimisho la juhudi hizo.
Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alisema:
“Masilahi ya Taifa ndiyo kitu cha msingi kinachotuunganisha
pamoja na tunawaomba wote walio tayari kushirikiana nasi watuunge mkono katika
kutekeleza azma hii muhimu kwa wananchi na nchi kwa ujumla. Masilahi binafsi
siyo hoja yetu kwa kuwa wapo watu wengi wasio wafuasi wa siasa hapa nchini
lakini wanaovutiwa na haja ya kuwa na maendeleo sawa kulingana na rasilimali
zilizopo.”
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa NCCR-Mageuzi, Mohamed
Tibanyendera alisema kitendo cha CCM kutunga Katiba yenye mapendekezo yake
pekee na kuyatupia kisogo maoni ya wananchi, kimepokewa vibaya na Watanzania
wengi ambao wanataka mabadiliko kupitia umoja huu.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa alisema:
“Historia inaonyesha kuwa ni vigumu kwa vyama vya upinzani kukiondoa madarakani
chama tawala pasipo ushirikiano wa vyama hivyo. Tuliona yaliyotokea Afrika
Kusini na hata jirani zetu Kenya… muungano huu utaleta mapinduzi kama
yaliyotokea Kenya.”
No comments:
Post a Comment