Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar aliyefukuzwa kazi, Othman
Masoud Othman (mwenye mkoba), siku alipopiga kura ya 'HAPANA' ambayo ndiyo
imemponza.
Dar es Salaam. Kung’olewa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud Othman katika nafasi hiyo ni kama kumewasha moto
visiwani humo huku mwenyewe akisema: ‘Ipo siku ukweli utadhihirika.’
Othman licha ya kutafutwa kutwa nzima ya jana, hakuwa tayari
kuzungumzia kufukuzwa kwake kazi na badala yake alituma ujumbe mfupi kupitia
simu yake ya kiganjani akisema: “Si wakati wake kulizungumza.”
Alipoulizwa kwamba pengine anaweza kuwa tayari
lini
kuzungumzia suala hilo, Mwanasheria huyo aliyepinga baadhi ya Ibara za Katiba
zinazopendekezwa kwa kuzipigia kura za hapana, alijibu pia kwa kifupi: “I have
no idea when (sifahamu ni lini), time will tell (ipo siku ukweli utadhihiri)”.
Kwa upande mwingine, watu wa kada mbalimbali nchini
wameelezea uamuzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kumtimua kazi kuwa
ni uonevu kwa kuwa alitumia haki yake ya kikatiba.
Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms alisema, “Sidhani kama ni matumizi
mazuri ya madaraka. Othman katika maelezo yake alitamka wazi kuwa maoni yake si
msimamo wa Serikali ya Zanzibar. Alichokizungumza ndiyo msimamo wake binafsi na
jinsi anavyoona inafaa.”
Alisema Mwanasheria huyo katika maoni yake alieleza wazi
jinsi Katiba ya Zanzibar inavyokinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano...
“Kilichomtokea ni tatizo la kutokuwapo kwa maridhiano tangu ulipoanza mchakato
wa kuandika Katiba Mpya.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali
linalojihusisha na masuala ya kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza alisema wajumbe
wa Bunge la Katiba walipiga kura kwa utashi wao na si ushawishi kutoka katika
makundi wanayotoka.
“Alichokizungumza Othman si maoni ya Serikali za Zanzibar.
Alipokuwa bungeni alikuwa sawa na wajumbe wengine na si mwakilishi wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar. Hii ni ishara mbaya kwa watendaji wa Serikali. Maana
yake ni kwamba watendaji wa chini wakifichua uovu unaofanywa na walio juu yao
wanaweza kufukuzwa kazi.”
Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei alisema:
“Sasa watu wameanza kuzuiwa kuamua mambo yao wao wenyewe. Othman alipiga kura
kama yeye binafsi na si Serikali ya Zanzibar tena akiwa na mawazo huru kabisa.
Kumfukuza kazi ni kutomtendea haki.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Ubatili siku
zote huzaa ubatili. Nchi yetu sijui inakwenda wapi, maana watu wanazuiwa
kufanya mambo yao ambayo yapo kikatiba. Maandamano hakuna, ukisema ukweli
unafukuzwa kazi?
“Watanzania wataendelea kudai Katiba yenye maoni yao. Hii ni
ishara ya kutaka kuwafumba midomo wengine wanaopenda kueleza ukweli.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alikuwa tofauti na wenzake,
akisema kilichomkuta mwanasheria huyo alikitarajia kwa sababu kitendo chake cha
kupiga kura ya hapana kilimaanisha kuwa amekwenda tofauti na msimamo wa
Serikali ya Zanzibar.
“AG anahudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri la Zanzibar na
ni lazima kuna mambo ambayo wanakubaliana, ambayo unatakiwa uyapinge ukiwa nao
na si nje ya vikao vyenu.
“Alipokuwa bungeni alikuwa amebeba msimamo wa Zanzibar na
kitendo cha kupiga ‘hapana’ ni kinyume na miiko ya uwajibikaji wa pamoja,”
alisema Dk Bana.
Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis
Abubakar (CUF), alisema hafahamu sababu za kigogo huyo kuvuliwa wadhifa wake.
“Aliyemwondoa AG ni Rais wa Zanzibar, yeye ndiye atakuwa
anajua sababu za kufuta uteuzi wake,” alisema Abubakar.
Hata hivyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS),
Awadh Ali Said alisema haikuwa wakati mwafaka kwa Rais Shein kumvua wadhifa
Othman wakati Taifa bado halijakamilisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano
na Zanzibar.
Alisema alikuwa akitetea mambo hayo kwa kuweka mbele manufaa
ya Zanzibar na wananchi wake pamoja na vizazi vijavyo hasa kwa kuzingatia kuwa
SMZ haikuwa na msimamo wa pamoja katika suala la mabadiliko ya Katiba ya
Muungano tangu mwanzo.
Alisema uamuzi wa kumvua wadhifa una madhara makubwa ikiwamo
kuwajengea misingi ya woga watendaji wakuu na kujikuta wakishindwa kujitokeza
kutetea au kupigania mambo ya msingi yenye manufaa kwa Zanzibar na wananchi
wake.
Mwanasheria Mkuu wa zamani, Hamid Mbwezeleni alisema kwamba
Rais hajafanya kosa kwa kumwondoa kwa sababu anatekeleza wajibu wake kwa mujibu
wa Katiba na sheria za nchi kama vile alivyomchagua na Katiba inampa haki ya
kumwondoa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF na Waziri wa Biashara Viwanda na
Masoko Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui, alisema haikuwa busara kufukuzwa kazi
wakati huu nchi ikiwa katika mjadala mkubwa wa kutafuta Katiba Mpya.
Alisema AG hakufanya makosa kutetea msimamo unaokwenda
kinyume na ule wa CCM katika kutafuta Katiba Mpya kwa kuwa alikuwa akitoa maoni
yake kama wajumbe wengine wa Bunge la Katiba.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja, Baraka Shamte
alisema Othman alitakiwa kujiuzulu wadhifa wake kabla ya kutimuliwa kazi
kutokana na kitendo chake cha kutetea mfumo wa Muungano wa Serikali tatu
kinyume na matakwa ya Serikali zote mbili ya Zanzibar na ile ya Muungano.
“AG ni sehemu ya Serikali, hakupaswa kujitokeza hadharani
kupinga mfumo wa muungano wa Serikali mbili kinyume na mtazamo wa bosi wake
anayetetea serikali mbili katika mfumo wa Muungano,” alisema Shamte.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment