Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 7, 2014

UNESCO YAAHIDI KUVIENDELEZA VYOMBO VYA HABARI JAMII KUKUZA DEMOKRASIA‏

DSC_0120
Mwalikishi wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii, Bi. Rose Haji Mwalimu akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Zulmira Rodrigues kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo hicho cha redio jamii Uvinza FM uliofanyika wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Kutoka kushoto ni Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya, Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo.
Na Mwandishi wetu, Uvinza


Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini.
Mwalikishi wa shirika hilo ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii Bi Rose Haji Mwalimu aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Redio Jamii cha Uvinza FM kilichozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.
Bi Haji alisema kwamba jitihada hizo ni kutokana na ukweli kwamba watu wengi wanaishi vijijini ambako hawapati fursa ya kupata habari kwa wepesi kwa ajili ya maendeleo yao kwa sababu wanaishi katika sehemu ambazo hazifikiki kwa urahisi kutokana ya miundombinu duni ya mawasiliano.
“Takwimu zinaonyesha kwamba nchini Tanzania watu wenye uwezo wa kuangalia telelvisheni ni asilimia 7 tu, kwa hiyo redio bado inachukua nafasi kubwa zaidi ya upatikanaji wa taarifa kwa haraka, wepesi, urahisi na kwa mapana zaidi,” alisema Bi. Rose Haji.
UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitoa msaada kwa redio jamii Tanzania katika kuzianzisha, kuzipatia vifaa na kuzijengea uwezo kiufundi na mafunzo ili zijiendeshe zenyewe.
Redio zilizoanzishwa na UNESCO ziko chini ya mtandao maalum ujulikanao kama Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA).
DSC_0285
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio hiyo.
Mtandao huo, hutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuharakisha maendeleo ya wananchi na ushirikishwaji wa wananchi kupitia redio jamii hususan matumizi ya Tehama, mchakato wa Rasimu ya Katiba, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Takribani Redio za Jamii zipatazo 30, ikiwemo ya Uvinza zinatekeleza mradi maalum wa Uchaguzi unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la (UNDP) kwa kushirikiana na UNESCO, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bara na Unguja (NEC na ZEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini (RPP).
“Redio zipatazo 30 zimeshapatiwa mafunzo yanayohusu maadili ya vyombo vya habari, jinsia, na masuala ya jinsi ya kuandika habari za migogoro kwa mtazamo chanya.
Viongozi wa serikali za mitaa pia watashiriki katika mradi huu kuhakikisha uhalali wa mradi huo, wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi maalum pia katika kuhakikisha mwendelezo wa utamaduni wa kuvumiliana, kujadiliana bila kugombana ili kuwezesha uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa amani na utulivu.
“Nina uhakika kuwa ushirikiano huu utaendelea baada ya mafunzo haya na kwamba redio jamii zitaleta mabadiliko makubwa kuhakikisha kuwa migogoro haina nafasi katika jamii zetu. Vyombo vya habari vina wajibu wa kuhakikisha kuwa vinaelimisha jamii juu ya athari za migogoro na kuhamasisha utulivu, amani na uvumilivu katika jamii, ” alisema Bi. Rose Haji Mwalimu.
Wakati huo huo mwakilishi huyo wa UNESCO Bi Mwalimu ameuomba uongozi wa halmashauri na wanajamii wa Uvinza kushirikiana na Redio Jamii Uvinza FM katika mradi huu ambao utawanufaisha sana wanajamii wa Uvinza na Kigoma kwa ujumla katika kuharakisha maendeleo.
DSC_0308
Mtangazaji wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, Kadisilaus Simon akitekeleza majukumu yake kwa furaha kabisa mara baada ya kupewa baraka na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.
“Redio hii ni yenu sio ya Kalufya, yeye ameianzisha kwa ajili ya maendeleo ya Uvinza, kitumieni, kitunzeni na mshiriki kikamilifu ili mpaze sauti zenu kwa maendeleo yenu na kudumisha Amani, upendo na utulivu kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” alisema Bi Mwalimu.
Nae Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Bi. Hawa Bayumi alisema kwamba Kampuni hiyo kwa kushirikiana na UNESCO bila kujali biashara, imejikuta inalazimika kujihusisha na masuala ya kijamii katika maendeleo kama shukrani za pekee kwa jamii kuruhusu minara ya kampuni kujengwa sehemu zao.
“Ikiwa ni njia ya kuishukuru jamii kwa kuiruhusu kampuni kujenga minara yake sehemu zao za kuishi, njia pekee ni kutoa msaada kwa wanajamii hao kuleta mabadiliko katika changamoto zilizopo ambazo ni umaskini, unyanyasaji wa kijinsia, na imani potofu za kishirikina kwa kuboresha miundombinu na mawasiliano”, alisema Bi. Bayumi.
Kwa kupitia redio jamii Bi. Bayumi amesema changamoto hizo zitaisha kwa kuhakikisha vipindi bora vinatayarishwa na kuhamasisha elimu kwa watoto, afya masuala ambayo yanaipa kampuni ya Airtel alama kuwa ilichangia maendeleo katika halmashauri ya Uvinza.
Kampuni ya simu ya Airtel imeahidi kuendelea kushirikiana na asasi husika hususan redio za kijamii kwa lengo la kukuza majadiliano ya kidemodrasia nchini.

No comments:

Post a Comment