Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 11, 2014

WAKAZI DAR WAASWA KUJITOKEZA KWENYE CHANJO YA MATENDE NA SURUA-RUBELLA.


 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu zoezi la utoaji wa chanjo ya Matende , Mabusha, dawa za Minyoo, matone ya Vitamini A, na Surua  - Rubella,  litakalofanyika  katika mikoa yote ya Tanzania kuanzia  Oktoba 18 hadi 24, 2014.
 Kaimu Mgaga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Hawa Kawawa  akisisitiza umuhimu wa  chanjo ya Surua –Rubella itakayotolewa wakati wa zoezi la chanjo Oktoba 18 hadi 24 na umuhimu wake kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito ambapo huwakinga watoto walio tumboni dhidi ya Virusi ambavyo huleta madhara pindi watoto wanapozaliwa.


Picha na Aron Msigwa - MAELEZO
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
10/10/2014. Dar es salaam.

Wakazi wa jiji la Dar es salaam wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la utoaji wa chanjo ya Matende , Mabusha, dawa za Minyoo, matone ya Vitamini A, na Surua  - Rubella,  litakalofanyika  katika mikoa yote ya Tanzania kuanzia  Oktoba 18 hadi 24, 2014.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendesha zoezi hilo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na  Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) kwa lengo la kudhibiti magonjwa yayoweza kuzuilika ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kuboresha afya za wananchi. 

Amesema zoezi hilo litawahusisha watoto  wenye umri wa miezi 9 hadi miaka 15 ambao watapatiwa chanjo ya Surua-Rubella, watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59  watapatiwa matone ya Vitamini A huku dawa za minyoo zikitolewa kwa wale walio na umri kunzia mwaka 1 hadi miezi 59 . 

 Ameeleza kuwa zoezi la utoaji wa chanjo ya dawa za Matende na Mabusha litawahusisha wananchi wote walio na umri wa kuanzia miaka 5 hadi 100.

Bw. Meck Sadiki amefafanua kuwa  katika jiji la Dar es salaam huduma itatolewa katika vituo vya afya pamoja na vituo vya muda vitakavyochaguliwa na viongozi  wa serikali ngazi ya kata ili kukidhi mahitaji na kusogeza huduma ya chanjo karibu na wananchi.

Aidha, amesema baadhi ya wadau wakiwemo LIONS  CLUB, RED CROSS na viongozi wa dini wamejitolea  kuwahamasisha wananchi katika  maeneo mbalimbali ili waweze kuitikia wito wa kushiriki  katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Ametoa wito kwa wananchi hususan wakazi wa jiji la Dar es salaam kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha zoezi hilo litakalofanywa na wataalam wa afya na kusisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na itatolewa bure na Serikali kwa wananchi wote.

Kwa upande wake Kaimu Mgaga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Hawa Kawawa amesema kuwa zoezi hilo  ni salama na lina umuhimu mkubwa kwa afya na maendeleo ya wananchi na kuongeza kuwa litasimamiwa na wataalam wa afya .

Akizungumzia kuhusu utoaji wa chanjo ya Surua –Rubella amesema kuwa una umuhimu mkubwa kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito ambapo huwakinga watoto walio tumboni dhidi ya Virusi ambavyo huleta madhara pindi watoto wanapozaliwa.

Amesema Virusi hivyo huwa na athari kwa mtoto aliye tumboni kwani humsababishia kuzaliwa akiwa na ngozi yenye vipele, homa, tatizo la mtoto wa jicho, mtindio wa ubongo, ulemavu na tatizo la Moyo.

Ametoa wito kwa wanachi wote hususan wakazi wa jiji la Dar es salaam kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata chanjo zitakazowakinga watu wazima na watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment