Idadi ya watu waliolazwa hospitalini kwa kunywa togwa
inayosadikiwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi mkoani
Ruvuma imeongezeka kutoka 270 hadi 340.Tukio hilo lilitokea Jumapili baada ya
watu kushiriki sherehe ya Kipaimara ambako walikula, kunywa pombe na togwa na
baadaye wale waliokunywa togwa walianza kuumwa matumbo, kuhara na kutapika.Hadi
jana, watu 102 walikuwa bado wamelazwa katika Zahanati ya Lyangweni, Hospitali
ya St. Joseph Peramiho na
Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.Tayari watu watano
wanashikiliwa na Polisi kwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo, akiwamo Baba
Mzazi wa mtoto Dickson aliyepata kipaimara, Enes Nungu (47).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela aliwataja
watu wengine wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea kwa mahojiano
kuwa ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki Masodi (65) na John
Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa ufunguo chumba cha vinywaji kabla ya
kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji vilichukuliwa
juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda Mskhiela alitoa wito kwa wananchi wanaoandaa sherehe
kuhakikisha wanafanya hivyo katika mazingira mazuri na yenye usalama ili
kuepuka athari kama hizo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace Mushi
alisema hadi jana, watu waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walikuwa 34
na hakukuwa na mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Majuto
Mlawa alisema wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na kupatiwa matibabu huku hali
zao zikiwa mbaya.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu alisema: “Jambo hili limenisikitisha sana, nimeumizwa sana nawapa
pole wote waliopatwa na tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu atawasaidia na
watapona na kurejea katika hali zao za kawaida.”
Hata hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama nyingine,
hivyo anaviachia vyombo vya usalama na wataalamu wa afya kupata ukweli. Pia
aliwataka wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa vyakula na pombe za kienyeji
katika sherehe mbalimbali.
No comments:
Post a Comment