WAZIRI MKUU Mizengo Pinda atatuma
wataalamu wa sekta ya kilimo ili waje kufuatilia suala la mahitaji ya trekta
ili kuziba pengo la mahitaji yake nchini Tanzania.
Alisema lengo la Serikali la
kuanzisha sera ya Kilimo Kwanza lilikuwa ni kuwasaidia wakulima kupata ruzuku
ya pembejeo, mbegu bora, na dawa za mifugo ili waweze kuongeza ushalishaji.
“Kutokana na mkopo wa Serikali ya
India, tulipata matrekta 1,846 ambayo hayakuchukua muda kuisha. Sasa hivi
tunatafuta wabia wengine wa kutupatia zana za kisasa za kilimo kwa sababu
matunda yake mazuri tumeyaona, tunataka kilimo cha Mtanzania,” alisema.
Jana asubuhi (Ijumaa, Oktoba 24, 2014), Waziri Mkuu alitembelea kampuni ya Farmers inayotengeneza
vipuri pamoja na matrekta ya kulimia na kuvuna yenye ukubwa wa Horse Power 80 na 72 ambayo alielezwa
kwamba yanavumilia hali ya udongo mgumu wa Afrika.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu,
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Farmer, Bw. ZDZISLAW ZUKIEWICZ alisema vifaa
vinavyotengenezwa na kampuni hiyo vina waranti ya miaka saba na vinaweza
kuhimili udongo wa miamba na mawe wa ardhi ya Tanzania.
Kampuni hiyo
inatengeneza matrekta, mashine za kuvuna mazao shambani (combined harvester),
mashine za kukata nyasi za malisho ya mifugo pamoja na vipuri vyake. Alisema
bei ya trekta ni wastani wa Euro 22,000 na wako tayari kuleta vifaa hivyo
Tanzania kama watapewa oda.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya
siku tatu nchini Poland jana mchana ambapo asubuhi alikutana na Watanzania
waishio Poland na baadaye kufanya vikao na baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la
Warsaw.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 26, 2014
No comments:
Post a Comment