Dirisha la usajili katika ligi ya Tanzania linatarajiwa kufunguliwa hivi karibu, na baadhi ya vilabu vimeanza harakati za kuimarisha vikosi vyao.
Wakati kukiwa na taarifa kwamba klabu ya Yanga imemtema mshambuliaji
Jaja kutoka Brazil, leo hii klabu hiyo imesema kwamba kiungo mkabaji
Mbrazil, Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili
siku ya Jumanne mchana Dar es salaam kwa ajili ya majaribio na Klabu
Yanga na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa hao mara 24
wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC
iliyopo ligi daraja la pili Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza
soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC
iliyopo Ligi Daraja la pili.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos “Jaja”
kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa
kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya
kifamilia.
Awali ilikuwa familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha
mapumziko, lakini waliomba yeye aende Brazil na baada ya kufika huko
matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurudi
kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua
matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Yanga kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo
katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu
kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya
kimataifa.
Aidha kikosi cha Yanga baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani
wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja
wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa ‘Nani Mtani
Jembe’ pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara
No comments:
Post a Comment