Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, November 12, 2014

BAWACHA walaani mauaji ya wanawake Mara

BAWACHA walaani mauaji ya wanawake Mara 
BARAZA la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), limelaani mauaji ya wanawake yanayofanywa na watu wasiofahamika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Butiama na Musoma mkoani Mara huku Jeshi la Polisi likishindwa kuyadhibiti.
Akiwahutubia wananchi wa Musoma kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mkendo Musoma Mjini, Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao, alisema inasikitisha kuona wanawake wasio na hatia wanauawa katika mazingira ya kutatanisha huku viongozi wa Serikali na jeshi la polisi lenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao wakiwa kimya.


“Wananchi wa Musoma unganeni wafichueni wauaji wa mama zetu, ikibidi muwakamate muwapeleke kwenye vyombo vya sheria, kwani jeshi la polisi linaonekana limeshindwa kazi. Haiwezekani wanawake wanauawa hapa lakini hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wauaji hawa,” alisema Abwao.
Naye Mwenyekiti wa BAWACHA mkoani Mara, Ester Matiko, alisema kuwa ni vema polisi ijikite kutafuta wahusika wa mauaji hayo yaliyoshika kasi kwenye Wilaya za Butiama na Musoma Vijijini.
Alisema kuwa, polisi wameweka nguvu kubwa kuzuia mikutano na maandamano yanayoandaliwa na CHADEMA ambayo yako sahihi kisheria, wakasahau wajibu wao wa kulinda raia.
Mwananchi wa Butiama, Costantine Juma, alisema kuwa mauaji ya wanawake yanasababishwa na imani potofu huku akitoa mfano kuwa, wakati mvua zilipoanza kunyesha siku inayofuata kuna wanawake waliamua kuwahi shamba kulima.
Alisema kuwa, mvua hiyo haikuendelea hivyo wanawake wale wakauawa kwa madai kuwa kitendo chao cha kuwahi kulima kiliwakasirisha mizimu hivyo mvua ikaacha kunyesha.
Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoani Mara, Philip Karangi, alisema kuwa ni kweli kulikuwa na matukio ya mauaji, ambako mara ya mwisho yalifanyika Aprili mwaka huu na tayari wahusika walishafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kada wa CCM atimkia CHADEMA
Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM, (UWT), Kata ya Wanyasho, Rehema Kunderema, alikihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA huku akiishutumu CCM kuwa, imejaa mafisadi na inakumbatia wafitini na wanafiki wenye kazi ya kupeleka maneno ya uongo kwa viongozi.
Alisema kuwa, tangu kumalizika uchaguzi mkuu uliopita na jimbo la Musoma mjini kunyakuliwa na CHADEMA baada ya Vincent Nyerere kushinda, ndani ya CCM kumekuwa na mtafaruku mkubwa kila mmoja akimnyooshea kidole mwenzake kuwa ndiye chanzo cha kushindwa kwao.
Kunderema aliyepewa kadi ya CHADEMA na Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA, Hawa Mwaifunga, alisema kuwa hali hiyo imewafanya kushindwa kutekeleza mikakati ya ujenzi wa chama, badala yake watu wamejikita kutafutiana ubaya ili wapeleke kwa viongozi.
“Nimeamua kuhamia CHADEMA kwa hiyari yangu sijalazimishwa na mtu, CHADEMA wanawaongelea wananchi si majungu. Suala la Nyerere kushinda uchaguzi wa kulaumiwa ni wanaCCM wote wa Musoma, ingawa kufanya hivyo ni kuwaonea kwani walimchagua kwa kuwa walijua ana uwezo wa kuwatumikia kama mnavyoona sasa,” alisema Kunderema.
Mwaifunga awataka wanawake kugombea
Makamu Mwenyekiti BAWACHA, Hawa Mwaifunga, aliwataka wanawake wajiamini na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye chaguzi mbalimbali, jambo litakalochangia kupatiwa ufumbuzi wa kero zinazowakabili kwa kuwa sehemu ya maamuzi ya vikao vya ngazi mbalimbali.
Alisema kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa uongozi na ni wapiga kura wakubwa, hivyo akawataka wanawake wengine wasisite kuwakampenia na kuwapigia kura, kwani CHADEMA itahakikisha wagombea wake ni wenye sifa.
Tendega alia na uchakachuaji kwenye chaguzi
Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Novemba 23 hadi 29 mwaka huu, kujiandikisha kwenye ofisi za kata, mitaa, vitongoji na vijiji kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Aliwaambia wananchi kuwa siku ya kupiga kura, wahakikishe wanaongozana na wanafamilia zao kupiga kura kisha wazilinde zisichakachuliwe.
Alisema kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni muhimu sana, kwani ndiyo wenye kuchagua viongozi wa ngazi za chini kabisa ambao ndiyo uhusika kujadili na kuweka mipango ya maendeleo ya wananchi wa maeneo husika kabla haijapelekwa ngazi za juu kwenye kata, halmashauri na bungeni.
Kunti alia kushuka kiwango cha elimu
Naibu Katibu BAWACHA, Kunti Yusuph, alisema kuwa Serikali ya CCM imeharibu kwa makusudi mfumo wa elimu hapa nchini, ndiyo maana kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana wanaotimu darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.
Alisema kuwa, serikali imekuwa haitafuti ufumbuzi wa kuikwamua sekta ya elimu, badala yake inazidi kuididimiza huku akitoa mfano kuwa, kwa sasa inawakata walimu sehemu mishahara yao ili kujenga maabara jambo alilodai litazidi kuzorotesha morali ya ufundishaji.
BAWACHA wamefanya ziara kwa wiki nne sasa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara, ambako agenda kuu zilikuwa ni umuhimu wa wananchi kushiriki chaguzi za Serikali za mitaa na kuwapa elimu wajue kwa nini wapige kura ya hapana kwa katiba pendekezwa
- Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment