BARAZA
la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), limelaani mauaji ya wanawake
yanayofanywa na watu wasiofahamika maeneo mbalimbali ya Wilaya za
Butiama na Musoma mkoani Mara huku Jeshi la Polisi likishindwa
kuyadhibiti.
Akiwahutubia wananchi wa Musoma kwenye uwanja wa shule ya Msingi
Mkendo Musoma Mjini, Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao, alisema
inasikitisha kuona wanawake wasio na hatia wanauawa katika mazingira ya
kutatanisha huku viongozi wa Serikali na jeshi la polisi lenye dhamana
ya kulinda usalama wa raia na mali zao wakiwa kimya.
“Wananchi wa Musoma unganeni wafichueni wauaji wa mama zetu, ikibidi
muwakamate muwapeleke kwenye vyombo vya sheria, kwani jeshi la polisi
linaonekana limeshindwa kazi. Haiwezekani wanawake wanauawa hapa lakini
hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wauaji hawa,”
alisema Abwao.
Naye Mwenyekiti wa BAWACHA mkoani Mara, Ester Matiko, alisema kuwa ni
vema polisi ijikite kutafuta wahusika wa mauaji hayo yaliyoshika kasi
kwenye Wilaya za Butiama na Musoma Vijijini.
Alisema kuwa, polisi wameweka nguvu kubwa kuzuia mikutano na
maandamano yanayoandaliwa na CHADEMA ambayo yako sahihi kisheria,
wakasahau wajibu wao wa kulinda raia.
Mwananchi wa Butiama, Costantine Juma, alisema kuwa mauaji ya
wanawake yanasababishwa na imani potofu huku akitoa mfano kuwa, wakati
mvua zilipoanza kunyesha siku inayofuata kuna wanawake waliamua kuwahi
shamba kulima.
Alisema kuwa, mvua hiyo haikuendelea hivyo wanawake wale wakauawa kwa
madai kuwa kitendo chao cha kuwahi kulima kiliwakasirisha mizimu hivyo
mvua ikaacha kunyesha.
Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoani Mara, Philip Karangi,
alisema kuwa ni kweli kulikuwa na matukio ya mauaji, ambako mara ya
mwisho yalifanyika Aprili mwaka huu na tayari wahusika walishafikishwa
kwenye vyombo vya sheria.
Kada wa CCM atimkia CHADEMA
Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM, (UWT), Kata ya Wanyasho, Rehema
Kunderema, alikihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA huku akiishutumu
CCM kuwa, imejaa mafisadi na inakumbatia wafitini na wanafiki wenye
kazi ya kupeleka maneno ya uongo kwa viongozi.
Alisema kuwa, tangu kumalizika uchaguzi mkuu uliopita na jimbo la
Musoma mjini kunyakuliwa na CHADEMA baada ya Vincent Nyerere kushinda,
ndani ya CCM kumekuwa na mtafaruku mkubwa kila mmoja akimnyooshea kidole
mwenzake kuwa ndiye chanzo cha kushindwa kwao.
Kunderema aliyepewa kadi ya CHADEMA na Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA,
Hawa Mwaifunga, alisema kuwa hali hiyo imewafanya kushindwa kutekeleza
mikakati ya ujenzi wa chama, badala yake watu wamejikita kutafutiana
ubaya ili wapeleke kwa viongozi.
“Nimeamua kuhamia CHADEMA kwa hiyari yangu sijalazimishwa na mtu,
CHADEMA wanawaongelea wananchi si majungu. Suala la Nyerere kushinda
uchaguzi wa kulaumiwa ni wanaCCM wote wa Musoma, ingawa kufanya hivyo ni
kuwaonea kwani walimchagua kwa kuwa walijua ana uwezo wa kuwatumikia
kama mnavyoona sasa,” alisema Kunderema.
Mwaifunga awataka wanawake kugombea
Makamu Mwenyekiti BAWACHA, Hawa Mwaifunga, aliwataka wanawake
wajiamini na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye chaguzi
mbalimbali, jambo litakalochangia kupatiwa ufumbuzi wa kero
zinazowakabili kwa kuwa sehemu ya maamuzi ya vikao vya ngazi mbalimbali.
Alisema kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa uongozi na ni wapiga kura
wakubwa, hivyo akawataka wanawake wengine wasisite kuwakampenia na
kuwapigia kura, kwani CHADEMA itahakikisha wagombea wake ni wenye sifa.
Tendega alia na uchakachuaji kwenye chaguzi
Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, amewataka wananchi kujitokeza
kwa wingi Novemba 23 hadi 29 mwaka huu, kujiandikisha kwenye ofisi za
kata, mitaa, vitongoji na vijiji kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za
mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Aliwaambia wananchi kuwa siku ya kupiga kura, wahakikishe
wanaongozana na wanafamilia zao kupiga kura kisha wazilinde
zisichakachuliwe.
Alisema kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni muhimu sana, kwani
ndiyo wenye kuchagua viongozi wa ngazi za chini kabisa ambao ndiyo
uhusika kujadili na kuweka mipango ya maendeleo ya wananchi wa maeneo
husika kabla haijapelekwa ngazi za juu kwenye kata, halmashauri na
bungeni.
Kunti alia kushuka kiwango cha elimu
Naibu Katibu BAWACHA, Kunti Yusuph, alisema kuwa Serikali ya CCM
imeharibu kwa makusudi mfumo wa elimu hapa nchini, ndiyo maana kumekuwa
na ongezeko kubwa la vijana wanaotimu darasa la saba bila kujua kusoma
na kuandika.
Alisema kuwa, serikali imekuwa haitafuti ufumbuzi wa kuikwamua sekta
ya elimu, badala yake inazidi kuididimiza huku akitoa mfano kuwa, kwa
sasa inawakata walimu sehemu mishahara yao ili kujenga maabara jambo
alilodai litazidi kuzorotesha morali ya ufundishaji.
BAWACHA wamefanya ziara kwa wiki nne sasa kwenye mikoa ya Kanda ya
Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara, ambako agenda kuu
zilikuwa ni umuhimu wa wananchi kushiriki chaguzi za Serikali za mitaa
na kuwapa elimu wajue kwa nini wapige kura ya hapana kwa katiba
pendekezwa
- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment