Pages

Thursday, November 20, 2014

IJUE SHERIA::JICHO LA BIASHARA LEO

Jicho kama kiuongo cha mwili linaona mbali, linakufanya kuweza kuangalia na kumulika biashara yako, uwezo kupata hali halisi na kufanya mabadiliko. Watu wengi Tanzania hususani wafanyabiashara wanafanya biashara kiholela bila kufuata utaratibu wa kisheria  au kufanya biashara kwenye taasisi inayokubalika na inayotambulika kisheria, kuna umuhimu mkubwa sana wa mfanyabiashara au mtoa huduma yoyote kuwa katika taasisi inayoeleweka kisheria na kutambulika bila kujali aina au ukubwa wa biashara husika.
Katika makala ya leo, JICHO LA BIASHARA limemulika kwenye usajili wa makampuni, Kampuni ni muunganiko wa watu zaidi ya mmoja walisajiliwa kisheria wenge lengo mmoja. Kampuni kisheria inatambulika kama mtu mwingine ambaye hausiani na wanahisa au washirika.
SHERIA
Usajili wa uendeshwaji wa kampuni unasimamiwa na sheria nyingi, Sheria kuu ni Sheria ya Makampuni sura ya 212, pia sheria nyingine ni sheria ya kodi, 

sheria ya viwango, Sheria ya Leseni, na sheria zingine zote za nchi ikiwa ni pamoja na katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
AINA ZA MAKAMPUNI,
Makampuni unaweza kuyatofautisha kulingana na mambo mbalimbali, unaweza kuyatofautisha kwa utaifa, uwepo wa hisa, umiliki au uwepo wa ukomo. Kisheria kuna makampuni ya aina mbalimbali, tukianza kwa kuangalia utaifa.
Tuna makampuni ya kigeni (Foreign Companies) , haya kimsingi yameundwa nchi za nje na hapa yamesajiliwa pia na yanamilikiwa kwa asilimia kubwa na wageni, kuna makampuni ya wazawa (Local Companies) Haya ni makampuni yaliyosajiliwa nchini na yanamilikiwa kwa asilimia kubwa na wazawa.
Pia kuna makampuni yenye ukomo wa hisa na yasiyo na ukomo wa hisa, Makampuni yenye ukomo wa hisa (Companies limited by Shares) Kimsingi ni makampuni ambayo yana malengo ya kibiashara, pia wanahisa wake wanatakiwa kuchangia endapo kampuni ikifirisiki kiasi kile ambacho hawajalipia kwenye hisa zao. Makampuni yasiyo na ukomo wa hisa (Companies limited by Guarantee) ni makampuni yasiyo na mlengo wa kufanya biashara, yenyewe yanategemea fedha kutoka kwa wa hisani, mara nyingine yana sura ya Taasisi zisizo za kiserikali (NGO’S) washirika(Members) kama kampuni itafirisika watachangia kile walicho ahidi kwenye katiba za makampuni husika mfano LHRC (Legal and Human Right Center).
Makampuni mengine ni kutokana na umiliki, hapa tuna makampuni ya umma (Public companies) haya ni makampuni ambayo wanahisa wake ni wengi sana, na kampuni inauwezo wa kuuza hisa zake kwa umma wote wa Tanzania, Haya ni makampuni ambayo hisa zake zinauzwa kwenye soko la hisa na haina ukomo wa idadi ya wanahisa lakini lazima waanzie wawili. Aina nyingine ni  makampuni binafsi (private companies) haya ni makampuni ya watu wachache ambao hisa zao haziuzwi kwenye soko la hisa, na uuzaji wake wa hisa sio rahisi sana, mara nyingi wahusika wenyewe hununua kwanza kabla ya kumuuzia mgeni lakini pia idadi ya wanahisa ya chini ni lazima wawe watu wawili, kwa idadi ya kwenda juu lazima wasiwe zaidi ya hamsini.
Pia kuna makampuni yenye ukomo (Limited Companies) ambayo haya makampuni kipindi cha kufirisika au yanapokufa mtu anapaswa kuchangia kile ambapo hakulipia kwenye hisa  ( limited to unpaid up shares) au kile ambacho amekubali kuchangia. Makampuni mengine ni makampuni yasiyo na ukomo (Unlimited Companies) haya ni makampuni ambayo wakati wa kufirisika au kufa mtu anapaswa kulipa madeni yote ya kampuni, hata mali binafsi zinaweza kuchukuliwa.
Nimeeleza aina za makampuni ili ndugu msomaji uelewe kuwa kuna aina mbalimbali za makampuni hapa Tanzania kwa mujibu wa sheria yetu ya makampuni sura ya 212.
Watu wengi wanafikiri kuwa na kampuni ni lazima uwe na fedha nyingi sana au biashara yako iwe kubwa sana sio kweli, acha uoga. Hata hao wenye makampuni makubwa hawakuanza na makampuni makubwa, walianza na wazo kama lako baadae wakasajili kampuni, ikawa kampuni mpya ndo baadae ikaanza kukua. Uoga ni dhambi na uoga ni umaskini thubutu na fungua kampuni yako isimamie pambana nayo baadae hata ukifariki watoto watajua baba au mama alifanya kitu. Mtu akifariki kampuni haifa, kampuni inadumu milele na milele labda ifirisike.
JINSI YA KUSAJILI KAMPUNI
Kuna hatua kadhaa za kupitia ili kufanya usajili wa kampuni, hatua hizo ni zifuatazo;
Moja, Uchunguzi wa jina, hapa mtu mwenye nia ya kusajili kampuni au kwa kupitia wakili huandika barua na kutaka majina pendekezwa yaangaliwe kama yanafaa kwa maadili ya kitanzania na haya fanani na kampuni nyingine yoyote. Hapo barua hupelekwa kwa msajili baada ya siku mbili au tatu utaambiwa kama jina limepita au hapana.
Kuandaa katiba na kanuni za kampuni (memorandum and articles of association ) hii huandaliwa kitaalamu na wanasheria, inaeleza kazi, malengo, majukumu, mgawanyo wa hisa,mwenendo na jinsi ya kuendesha kampuni. Katiba na kanuni zinapaswa kuandikwa kisheria ikiwa kinyume na sheria kampuni haita sajiliwa.
Kujaza fomu namba 14A, baada ya kuandaa katiba, inajazwa fomu namba 14A ambayo kimsingi inajazwa kitaalamu ikielezea mahali ofisi ya kampuni itakuwa, wakurugenzi na anwani zao, tarehe zao za kuzaliwa lengo ni kuwa mkurugenzi lazima awe na miaka zaidi ya 21, pia utaifa wao ili kujua utaifa wa kampuni. Ikikosewa kujazwa vizuri kampuni haitasajiliwa.
Kujaza fomu namba 14B, hii ni fomu ya kiapo kwamba mtu aliyehusika kusajili kampuni hii amefuata utaratibu wote wa kisheria, hii fomu lazima kiapo chake kiwe mbele ya wakili au kamishina yoyote wa viapo, hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Makampuni Sura ya 212.
Baada ya kuandaa nyaraka husika basi nyaraka hizo huwasilishwa kwa msajili wa makampuni na  kulipa gharama kwa kulingana na mtaji wa kampuni na aina ya kampuni,
Baada ya siku kadhaa mhusika au kupitia wakili huenda kuchukua cheti cha usajili wa kampuni yako, , basi baada ya hapo mtu huwa na kampuni yake na kuanza taratibu zingine, kama kuchukua leseni na vibali mbalimbali kulingana na aina ya biashara yake.
SIFA ZA KAMPUNI
Kampuni ina sifa kadhaa tofauti na taasisi nyingine, sifa hizo ni kama zifuatazo;
Moja, kampuni kisheria ni mtu tofauti kabisa na wanahisa au washirika wake, maana yake ina sifa za mtu ndani yake (legal personallity ) ina maana kampuni inauwezo wa kufanya shughuli zote za kibiashara kwa jina lake yenyewe, wakurugenzi ni ubongo wa kampuni lakini wao sio kampuni.
Kampuni inaweza kuingia kwenye mkataba kwa jina lake yenyewe, kwa kuwa ina sifa kama mtu, basi inaweza kuingia kwenye mkataba kwa kutumia mhuri wa moto (Common seal) au kupitia wakurugenzi kwa niaba ya kampuni.
Kampuni inaweza kushitaki au kushitakiwa, kampuni inaweza kufungua kesi na kushitaki au kusishitakiwa kwa lolote itakayofanya katika shughuli zake.
Kampuni ina dumu milele (perpetual succession), pia kampuni ina sifa ya kudumu, yani wanahisa au walioifungua na kuisajili wakifariki kampuni yenyewe haifi, inaendelea kudumu ina utaratibu wake wa kufa au kufirisika.
Lakini sheria inazuia watu kusajili kampuni kwa nia ya kuiba au kukwepa kodi au kudhurumu, makama haitaweza kuvumilia watu kufanya uhuni kwa kupitia kampuni. Mahakama au Sheria inaweza kutoa kivuli cha kampuni na mtu kushitakiwa binafsi (Lift the corporate vail).
FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI
Kuna faida nyingi sana za kuwa na kampuni, kisheria, kiuchumi na kijamii, kwanza mtu mwenye kampuni yake, jamii ina mheshimu sana na anaonekana ni mtu makini sana hata kama atakuwa hajasoma kabisa. Faida za kuwa na kampuni ni hizi zifuatazo,
Moja utaongeza uwezo wako wa kibiashara kitaifa na kimataifa, watu wengi sana kwa sasa wanapenda kufanyakazi na makampuni na sio mtu binafsi, kuna kazi nyingi unaweza kukosa kwa kuwa hauna kampuni, kampuni inaweza ikawa ya kufanya usafi, kuuza na kununua biadhaa, kampuni ya kilimo, kampuni ya uvuvi, ulinzi, kukusanya madeni, kutoa huduma ya hospitali, michezo,mtandao,shule, mawasaliniano n.k
Ukiwa na kampuni ni rahisi kupata zabuni za aina mbalimbali (Tender), ukipitia magazeti mbalimbali zabuni wanataka mtu ambaye yupo na kampuni sio mtu binafsi, watu wanaamini ni salama zaidi kufanya kazi na kampuni na sio mtu binafsi,unapaswa kwenda na wakati.
Lakini pia kampuni inakufanya uweze kufanya biashara kwa uhuru zaidi na kuheshimika sana, ndani na nje ya nchi.
Ukiwa na kampuni, hata kama kampuni ikiyumba sio lazima na wewe utayumba, zitayumba mali za kampuni sio zako binafsi, kama kuna hasara mnagawana wanahisa wote, kwa hiyo unaweza kupata hasara kidogo.
Ukiwa na kampuni ni rahisi kukopesheka kwa mabenki na taasisi mablimbali za kifedha, kampuni inaweza kutoa na kupokea mkopo.
Ni watanzania tu, ambao bado akili haijafunguka na kutambua fursa mbalimbali ukiwa na kampuni, ni muda muafaka wa kufikilia kuwa na kampuni yako inayojitegemea kwa kulingana na biashara yako au huduma yako.

Mwandishi wa Makala hii ni Jebra Kambole Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates wa Jijini Dar-es-salaam.
JICHO LA BIASHARA kwa maswali na maoni 0717334032  Email jebrakambole@gmail.com

No comments:

Post a Comment