Askofu Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria anayehusishwa na
biashara ya madawa ya kulevya.
|
KIMENUKA! Vigogo wa madawa ya kulevya wakiwemo viongozi wa
dini sasa wanaanza kupukutika kutoka kwenye mstari wa siri huku baadhi yao
wakikimbilia nje ya nchi kufuatia oparesheni kali inayofanywa na Kikosi cha
Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulenya Tanzania kuwanasa kila kukicha,
Uwazi lina mchoro kamili.
Hivi karibuni kikosi hicho kimemkamata askofu (mwangalizi
mkuu wa kanisa) aliyetambulika kwa jina la Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria
ambaye ana kanisa la kiroho maeneo ya Sinza jijini Dar.
Jina la kanisa hilo limedhibitiwa na vyombo husika kwa
sababu ya uchunguzi zaidi na uhalali wake wa kuwepo nchini.
SIKU YA TUKIO
Vyanzo vyetu makini ndani ya kikosi kazi vinaeleza kwamba,
mchungaji huyo alikamatwa Oktoba 31, mwaka huu saa kumi usiku Tegeta wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya heroine kilo
35.
KAMA UNGEINGIA SOKONI
Habari za ndani
kutoka kwenye oparesheni hiyo zinasema kuwa, endapo unga huo ungeingia sokoni
na kununuliwa, basi mtumishi huyo wa Mungu angevuna kitita cha zaidi ya
shilingi bilioni mbili.
NYUMBA ALIYONASIWA YA PROFESA
Mchungaji huyo ambaye serikali imeanza kazi ya kulichunguza
kanisa lake, alidakwa na mzigo huo haramu kwenye makazi aliyopanga ambayo ni
nyumba ya profesa mmoja wa chuo kikuu, Mbezi jijini Dar es Salaam.
Askofu akiwa chini ya ulinzi.
WASHIRIKA NAO WADAKWA
Kwa mujibu wa chanzo, kamatakamata ya mchungaji huyo pia
iliwakumba watuhumiwa wengine ambao ni Walyat Khan raia wa Pakistani, Chuksi
Sylvester Agbazuo na Tony Olafor wote raia wa Nigeria na inadaiwa kwamba
walikuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali na kutoroka.
HABARI NYETI
Habari za siri ambazo Uwazi ilizinasa zinadai kuwa, watumishi wa Mungu waliokuwa kwenye orodha ya
kunaswa walikuwa wengi lakini
wamekimbilia nje ya nchi na kikosi hicho kimeshawasiliana na Polisi wa
Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kuwasaka na kuwatia nguvuni.
MAJINA MAPYA MEZAN KWA NZOWA
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, Kamanda wa Polisi Kitengo
cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa
amekabidhiwa majina ya vigogo wakiwemo viongozi wa dini ambao ni sugu katika
biashara hiyo. Mbali na majina hayo, pia
amepewa ratiba zao za safari za kibiashara hivyo kilichobaki ni kuwafuatilia na
kuwakamata na ushahidi ili kuhakikisha kwamba hawawezi kupona mahakamani.
MTANDAO HATARI
Habari zaidi zinadai kuwa, siku za hivi karibuni, Kamanda Nzowa amekuwa akifumua mtandao wa watu wazito
katika biashara hiyo na imebainika kuwa vigogo hao wana mtandao mkubwa
serikalini ikiwemo wizara ya mambo ya ndani ambao wanawalinda kwa kupewa
mamilioni ya pesa kwa ajili ya usimamizi wa upitishwaji wa biashara hiyo haramu
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar.
“Unajua zamani viongozi hao serikalini walikuwa wakimsumbua
Kamanda Nzowa ili awaachie watuhumiwa waliokamatwa na unga bila mafanikio,
lakini sasa wameshamsoma kiasi kwamba hata wakikamatwa hawampigii simu tena,”
kilisema chanzo kingine.
Dawa za kulevya alizokutwa nazo askofu huyo.
WATOTO WA VIGOGO
Habari nyingine zinadai kuwa, Kamanda Nzowa pia ana majina
ya watoto wa vigogo wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo na anayafanyia
kazi.
KUMBUKUMBU
Kukamatwa kwa askofu huyo kumekuja baada ya kukamatwa kwa
vigogo ambao ni viongozi wa dini katika makanisa ya kilokole.
Januari 11, mwaka huu, Askofu Moris Charles alidaiwa
kukamatwa na polisi maeneo ya Chinga Mbili mkoani Lindi akiwa na kilo 210 za
madawa ya kulevya aina ya heroine yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4, kesi
yake bado inaendelea mahakamani mkoani humo.
Juni 8, 2011 polisi walifanikiwa kumkamata Mchungaji Kapupu
Denis Okechuku wa kanisa la kilokole lililopo Kinondoni Biafra akiwa na kilo 81
za cocaine, kesi yao bado ipo Mahakama ya Kisutu, Dar.
Nyumba aliyokutwa askofu huyo.
KAMANDA NZOWA
Uwazi lilipomtafuta Kamanda Nzowa ofisini kwake juzi,
alisema kuna watu wanne waliokamatwa Tegeta wakiwa na kilo 35 za madawa ya
kulevya aina ya heroin na kuna wengine wanatafutwa kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa nisingependa kuzungumzia sakata hilo kutokana na
sababu za kiupelelezi kwani kuna wengine tunawatafuta na nitahakikisha
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, nawashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao,” alisema Nzowa.
No comments:
Post a Comment