Dodoma. Sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni
katika akaunti ya Tegeta Escrow limeendelea kuibuka kwa sura mbalimbali
bungeni. Safari hii, Bunge limetakiwa kueleza ni kwa nini Ripoti ya Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) isifikishwe katika chombo hicho cha
kutunga sheria sambamba na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Hayo yalijitokeza bungeni jana baada ya wabunge kadhaa
kusimamia wakitaka mwongozo wa Spika
kuhusu uchunguzi huo, hasa kutokana na
kuwapo taarifa kuwa ripoti ya CAG itawasilishwa bungeni mwishoni mwa mwezi huu,
lakini ile ya Takukuru ambayo pia inachunguza suala hilo, haitapelekwa bungeni
wala kujadiliwa.
Uchunguzi wa Akaunti ya Escrow uliamuliwa na Serikali baada
ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kulipua ufisadi
uliotokana na utata katika uchotaji wa fedha kwenye akaunti hiyo katika Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia kiwango cha
fedha ilichokuwa inalipa kwa gharama za uwekezaji kwa IPTL, ndipo ikaamuliwa na
Mahakama ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa inalipa ziendelee kuwekwa
huko hadi mgogoro utakapokwisha. Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira
yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na IPTL.
Jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge kadhaa
walisimama wengi wakiwa wa upinzani wakitaka mwongozo kuhusu lini ripoti hizo
mbili zitawasilishwa bungeni hasa baada ya ile ya Takukuru kuelezwa na Mkurugenzi
Mkuu wake, Dk Edward Hoseah kuwa imekamilika na kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ndiye
aliyefungua mlango wa kuomba mwongozo wa Spika akitaka kujua ni lini ripoti
hiyo itawasilishwa na kwa nini isiambatane na ile ya CAG kwa kuwa zote
zinatokana na maazimio ya Bunge kutaka uchunguzi huo ufanyike.
Pia Nassari alihoji kwa nini mjadala wa ripoti ya CAG
umepangwa siku mbili za mwisho kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge.
“Naomba maelezo kwa nini hii ya Takukuru haitaletwa wakati
imeelezwa kuwa Waziri Mkuu ameshakabidhiwa?” alihoji Nassari.
Akijibu, Naibu Spika, Job Ndugai alisema Kamati ya Uongozi
imeshajadili suala hilo na kuamua kwamba ripoti ya CAG itapitia kwenye Kamati
ya PAC inayoongozwa na Zitto Kabwe na kuwasilishwa bungeni.
“Ripoti ya CAG itawasilishwa kwenye Kamati ya PAC na wabunge
mtakabidhiwa nakala kama tulivyokubaliana kwenye Kamati ya Uongozi,” alisema
Ndugai na kuongeza:
“Ripoti itawasilishwa tarehe 26 mwezi huu kama
ilivyorekebishwa kwenye ratiba. Kuhusu suala la kupangwa mwishoni ni suala la
kanuni kwa kuwa huwa tunaanza na shughuli za Serikali kwanza halafu ripoti
zinafuata.”
Kuhusu ripoti ya Takukuru, Ndugai alisema haiwezi
kuwasilishwa bungeni kwa kuwa taasisi hiyo ikishamaliza shughuli zake inaweza
kuchukua hatua kwa kupeleka taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili
ya hatua zaidi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment