Watu wanne wameuawa kwa kudungwa visu na vijana waliokuwa
wamejihami mjini Mombasa Pwani ya Kenya.
Watu kadhaa pia walijeruhiwa katika shambulio hilo la usiku
wa kuamkia leo kwenye vituo vya basi Kisauni. Bado haijajulikana waliouawa ila
inaaminika walikuwa raia wa kawaida waliokuwa kwenye shughuli zao.
Mwandishi wa BBC mjini humo Emmanuel Igunza anasema hali ya
wasiwasi imetanda Mombasa huku maafisa wa polisi wakipiga doria mitaani.
Walioshuhudia mashambulio hayo wanasema vijana
waliokuwa
wamejihami kwa mapanga na silaha nyingine butu, waliwavamia watu katika vituo
vya magari ya abiria.
Aidha inadaiwa vijana hao walikuwa wameziba nyuso zao,
wakipeperusha bendera nyeusi sawa na ile iliyopatikana katika msako wa jana
kwenye miskiti ya Musa na Sakinah, jijini Mombasa.
Awali Polisi walionya kuwa wako tayari kukabiliana na
chochote kitakachotokea kufuatia msako huo.
Zaidi ya vijana mia mbili hamsini walikamatwa na silaha
kadhaa ikiwemo magurunedi na bastola kupatikana katika misikiti hiyo.
Hata hivyo viongozi wa Kiislamu na mashirika ya kutetea haki
za kibinadamu wamelaani msako huo, ambao wanasema utaenndeleza dhana kuwa
polisi wanailenga jamii nzima ya waislamu.
Mwezi Februari, msako sawa na huo uliotekelezwa katika
msikiti wa Musa ulisababisha ghasia na kifo cha afisa mmoja wa Polisi.
No comments:
Post a Comment