Pages

Saturday, December 6, 2014

60 wanusurika kufa mtoni

Mkuu wa wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya
Zaidi ya abiria 60 waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Mwanza Coach, kwenda Musoma mjini wamenusurika kufa baada ya tairi la mbele kupasuka na kutumbukia mtoni.
Tukio hilo limetokea juzi na kulihusisha basi lenye namba za usajili T714 BJB  ambalo baada ya tairi kupasula liliacha kuacha njia.
Mkuu wa wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu tisa walipata michubuko kidogo baada ya basi hilo kutumbukia katika daraja la Mto Masanza kata ya Kiloleli wilayani hapa.

Alisema baada ya tairi kupasuka basi hilo lilipoteza mwelekeo hatimaye kutumbukia katika mto huo 




uliokuwa umejaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani hapa. Kwa upande wake dereva wa basi hilo, Edward Juma, alisema baada ya tairi kupasuka alijitahidi kulizuia gari hilo lisitumbukie mtoni lakini ilishindikana.
Naye mmoja wa abiria wa basi hilo, Mary Mwita, aliyekuwa akitoka Musoma kwenda Mwanza, alisema kazi kubwa iliyofanywa na dereva wa basi hilo ilisaidia kuokoa maisha yao.

Abiria mwingine Francis Mongela, alisema iwapo dereva wao asingekuwa makini basi hilo lingesababisha vifo vya abiria wengi.

Askari wa jeshi la polisi, Joseph Christopher wa kituo cha Busega aliyekuwa akipeleka mahabusu wilayani Magu, alisema basi hilo lilikuwa katika mwendo wa kawaida na iwapo mwendo ungekuwa wa kasi ingesababisha maafa makubwa.

Kampuni ya Mwanza Coach na ile ya J4, yalifungiwa na serikali kuendesha huduma za usafishaji abiria kati ya Mwanza na Musoma baada ya kugongana na kusababisha vifo vya abiria zaidi ya 30 eneo la sabasaba wilayani Serengeti Agosti mwaka huu.

Wakati huo huo,  Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema kuwa mvua za vuli zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya mikoa mbalimbali nchini zinatarajia kufikia ukingoni katika maeneo ambayo kwa mwaka hupata misimu miwili ya mvua.

Mkurugenzi wa Utabiri wa mamlaka hiyo,Dk. Hamza Kabelwa, alisema mvua za vuli na msimu zinakaribia kufikia ukingoni ili msimu wa mvua za masika kwa baadhi ya maeneo ambayo hupata mvua kwa misimu miwili kuanza kunyesha.

“Hizi ni mvua za vuli na msimu wala siyo mvua za masika kama ambavyo wananchi wanafikiria, wakati ukifika tutatoa taarifa kuwajuulisha Watanzania,”alisema.
 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment