CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Simanjiro mkoani Manyara,
kimepata viongozi 223 kati ya 281 wa vitongoji na wengine 48 kati ya 55 wa
vijiji waliopita bila kupingwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa,
unaotarajia kufanyika Jumapili.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Bakari Mwacha
alithibitisha hayo jana wakati Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Brown ole Suya
akizindua kampeni ya CCM ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye mji mdogo wa
Mirerani.
Mwacha alisema hadi sasa kabla ya uchaguzi huo,
CCM imepata
ushindi wa asilimia 87 kwenye uchaguzi wa ngazi ya vijiji na asilimia 88 katika
vitongoji vya wilaya hiyo, baada ya wagombea wao kupita bila kupingwa.
Katibu Uchumi na Fedha wa CCM mkoani Manyara, Lucas Zacharia
aliitaka Chadema kutoeneza maneno ya chuki, fitina na uongo kuwa yeye alitoa
rushwa ili wagombea wao waondolewe ilhali walikosea kujaza fomu zao.
Zacharia ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Endiamtu, alisema
wagombea wa Chadema walikosea kwa kuandika majina yao, hivyo wajilaumu wao
wenyewe na siyo kuchafua majina ya watu kuwa rushwa ilitumika ili waondolewe.
“Kama ni uchawi watafutane wao wenyewe na kama ni uzembe
walifanya wao wenyewe na siyo kudanganya wananchi kuwa eti nilitoa rushwa kwa
wasimamizi wa uchaguzi huo ili CCM tupite bila kupingwa,” alisema Zacharia.
Alisema kwenye vitongoji vyote 12 vya Kata yake ya Endiamtu,
wagombea wote wa CCM walipita bila kupingwa, baada ya wagombea wa Chadema
kukosea kujaza fomu na kujidhamini wao wenyewe badala ya chama chao.
Chanzo;Habari Leo
No comments:
Post a Comment