DIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kigogo,
Kinondoni jijini Dar es Salaam, Richard Chengula wiki iliyopita alipata wakati
mgumu, baada ya kunusurika kupigwa na wananchi wake, kwa kile kilichodaiwa
kuzuia shughuli za maendeleo.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita saa tatu na nusu
asubuhi wakati zoezi la upigaji kura wa serikali za mitaa likiendelea. Inadaiwa
kuwa baada ya mafuriko ya mara kwa mara ya mto Tenge uliopo katika mtaa wa
Mkwajuni, wananchi hao walichangishana fedha na kukodi katapila kwa ajili ya
kusafisha na kuzibua maji.
Wakati shughuli hiyo ikiendelea, kwa mshangao wa wengi,
diwani huyo alijitokeza na kuwakataza kuendelea na shughuli hiyo, jambo
lililopingwa kwa nguvu zote na wananchi hao, ambao walimgeuzia kibao na kutaka
kumshushia kipigo.
Polisi akiwazuia wananchi wasimpige Diwani, Richard
Chengula.
Inadaiwa kuwa baada ya kuona anazidiwa nguvu, diwani huyo
alikimbilia katika jengo la kiwanda cha kununua na kusaga mifupa cha Ferner
Center Limited ambako aliomba hifadhi na kuwapigia simu polisi ili waje
kumuokoa. Baada ya dakika chache, askari waliwasili eneo la tukio walikokuta watu
wengi wakipiga kelele nje ya kiwanda hicho.
“Tumeamua kumtukana na kutaka kumpiga kwa sababu siyo mtu wa
kuleta maendeleo kabisa. Yeye hata siku moja hajawahi kuleta katapila la
serikali kwa ajili ya kazi hii, sasa sisi wenyewe wananchi tumechangishana
halafu yeye anakuja kutuletea upuuzi, ndiye amefanya Kata yetu kuwa nyuma
kimaendeleo,” alisema mwananchi mmoja kwa jazba kubwa.
Gari la Polisi likiwa eneo la tukio.
Inadaiwa kuwa kutokana na kadhia hiyo, wananchi hao kwa
pamoja waliungana na kuhamasishana kupiga kura za hasira na kuwapa wapinzani,
ambapo mitaa miwili kati ya mitatu ya kata hiyo, ilichukuliwa na Chama Cha
Wananchi (CUF) huku mtaa mmoja uchaguzi wake ukiahirishwa hadi ulipofanyika
juzi Jumapili.
“Huyu diwani pamoja na kwamba ni bosi wangu kichama, lakini
ametuudhi sana na yeye ndiyo kikwazo kikubwa cha kusababisha mitaa kuchukuliwa
na vyama vya upinzani kwa sababu baada ya kutuingilia wananchi walimweleza wazi
kuwa mitaa yote wanaipa upinzani na ndivyo ilivyokuwa, yaani hata wanaccm
wamekasirishwa sana na kuipa kura CUF,” alisema mjumbe mmoja wa nyumba kumi
ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Wananchi wenye hasira wakiwa eneo la tukio.
Diwani Chengula alikiri kukutana na mtafaruku huo akidai
kuwa alikwenda eneo hilo ili kutoa ushauri wa kitaalamu lakini cha ajabu,
akajikuta mambo yakimbadilikia.
No comments:
Post a Comment