Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete.
BUNGE limeazimia kuwajibishwa kwa mawaziri Profesa Sospeter
Muhongo, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick
Werema, kutokana na sakata la uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT) kwa kutaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi
wao.Mbali na hao, yumo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).Aidha,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuwa Serikali itatekeleza maazimio yote
manane yaliyopitishwa jana jioni na Bunge baada ya mjadala mkali wa siku tatu
na mvutano wa siku moja juzi katika kupitisha maamuzi hayo ambayo yalifikiwa
kwa maridhiano.Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe alisoma maazimio hayo manane jana bungeni baada ya kufikiwa
kwa maridhiano kati ya Kamati yake, Kambi ya Upinzani, Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Serikali.
Maazimio
Katika azimio la pili, Zitto alisema viongozi hao wa umma na
maofisa wa ngazi za juu serikali wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa
na vitendo vya kijinai katika sakata hilo, linalohusisha kampuni ya kufua umeme
ya Independent Power Tanzania (IPTL).
“Kwa kuwa vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi
wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini, vinakiuka pia maadili ya
viongozi wa umma kuwanyima viongozi na maofisa hao uhalali wa kuendelea
kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
“Hivyo, basi Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na
Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco wawajibishwe,
kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi wao kutengua uteuzi wao,” alisema Zitto.
PAC katika mapendekezo yake bungeni, ilitaka Muhongo, Maswi,
Jaji Werema, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele na Waziri Mkuu
Pinda wawajibike kutokana na sakata hilo, lakini wabunge wengi walisema Masele
na Waziri Mkuu Pinda hawakuhusika katika sakata hilo.
Aidha, kwa mujibu wa Zitto, Bunge limeazimia kuwa Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),
Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria
za nchi kwa watu wote waliotajwa kuhusika na vitendo vyote vya jinai,
kuhusu miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow, na watu wengine watakaogundulika
baada ya uchunguzi mbalimbali unaondelea katika vitendo hivyo vya jinai.
Miongoni mwao ni mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Singh
Sethi, James Rugemalira wa VIP Engineering Ltd, Jaji Werema, Profesa Muhongo,
Maswi, wajumbe wa Bodi ya Tanesco, ambao inasemwa kuwa walihusika kwa namna
moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha katika
akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP na VIP Engineering and Marketing Ltd.
*Wabunge
Azimio jingine la Bunge ni kuazimia Kamati za Kudumu za
Bunge
kuwawajibisha viongozi wake kwa kuwavua nyadhifa zao
kutokana na kushiriki kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo.
Hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Andrew
Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, William
Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco.
Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na fedha za mwanahisa
Rugemalira kwa Chenge kupewa Sh bilioni 1.6 na Ngeleja Sh milioni 40.2, kwa
mujibu wa taarifa ya CAG na PAC.
“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Kamati husika za Kudumu
za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi
na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa Kamati husika za
Kudumu za Bunge,” alisema Zitto.
*Majaji
Kuhusu ushiriki wa majaji katika kashfa hiyo, alisema Katiba
ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka
utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya majaji, ambao kwa mujibu wa
Katiba hiyo, unamtaka Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma
za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Alisema kwa kuwa utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya
majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji
husika wakati wa tuhuma dhidi yake unaendelea;
“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji
ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa nidhamu wa maadili dhidi ya
Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya
Tanzania,” alisema Zitto.
Aidha, Bunge limeazimia mamlaka husika za kifedha na za
kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote
itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na
utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi
zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
*Sheria
Katika azimio jingine, Bunge limeazimia kwamba Serikali
iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa
lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti
vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa
Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
Pia Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge kuhusu
mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua
umeme, hivyo basi Serikali imetakiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la
Bajeti.
“Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa
kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la
kuokoa fedha za shirika hilo,” aliongeza Zitto katika maazimio hayo
yaliyoridhiwa na Bunge zima baada ya kuandaliwa na watu 21.
*Pinda
Akiahirisha mkutano huo wa 16 na 17 wa Bunge, Waziri Mkuu
Pinda alisema CAG atapewa kazi mahsusi
ya kufanyika kazi kujua kama fedha za Tegeta Escrow zilikuwa za umma, kwa maana
alisema sehemu inaweza kuwa za Tanesco, IPTL au Serikali.
Source:Habarileo
No comments:
Post a Comment