Maazimio ya Bunge yalimtaka Rais kuwawajibisha wote
waliotajwa kuhusika na kashfa ya escrow, uamuzi ambao upo mikononi mwa Rais
Kikwete
Mamlaka ya Bunge.
Baada ya wabunge kutoa maoni yao katika Taarifa
iliyowasilishwa na Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC) na majibu ya Serikali
kama yalivyowasilishwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ilikuwa ni wazi kwamba Serikali ilikuwa imelemewa na hoja za PAC.
Kulemewa kwa hoja za Serikali kulikuja kuwa wazi zaidi baada
ya Kamati ya PAC kujibu kwa umakini mkubwa hoja za Serikali na wabunge
waliokuwa wanaegemea upande wa Serikali.
Baada ya mjadala kuhitimishwa mambo matatu yalikuwa dhahiri
kwa wabunge wengi. Mosi, sehemu ya fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta
Escrow ilikuwa ni ya umma.
Pili, kuna baadhi ya viongozi wa Serikali na watu wengine
wenye mamlaka katika jamii walikuwa wamejipatia fedha ya Escrow katika
mazingira yanayotia shaka kuhusu maadili yao kama viongozi.
Tatu, Serikali haikutekeleza wajibu wake kikamilifu katika
kusimamia masilahi ya umma katika uendeshaji wa akaunti ya Tegeta Escrow na
mikataba ya nishati kwa jumla.
Kutokana na makosa haya ilikuwa lazima kwa Bunge kuchukua
hatua kadhaa katika kuiwajibisha Serikali na hapa ndipo hoja ya mamlaka ya
Bunge inapokuja.
Kutokana na mjadala wa Bunge usiku wa Ijumaa 28 Novemba 2014
ilikuwa wazi kwamba Bunge letu limewekewa mipaka mikubwa sana kikatiba katika
kuiwajibisha Serikali.
Pamoja na kwamba wabunge wengi walitamani kwa usahihi kabisa
kuwajibisha mara moja waliohusika na kadhia hii, lakini walikuwa hawana uwezo
wa kikatiba wa kutekeleza matamanio yao.
No comments:
Post a Comment