Dar es Salaam. Matokeo ya awali ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyika nchi kote hivi karibuni yanaonyesha kuwa wananchi
wamebadilisha mitazamo yao dhidi ya vyama vya siasa na hivyo kutoa picha mpya
kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Uchaguzi huo uligubikwa na malalamiko katika baadhi ya
maeneo nchini kiasi cha Serikali kuwaondoa kazini wakurugenzi wa halmashauri
tano kwa kushindwa kuusimamia vyema, pia umevipa vyama na Serikali nafasi ya
kujitafakari upya.
Kwa upande mmoja, uchaguzi huo umewapa nguvu wapinzani kwa
kuongeza idadi ya viti, lakini umeivuta nyuma CCM baada ya kupoteza zaidi ya
nafasi 2,600 za uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa na
uchaguzi wa
mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12, 042.
Vyama vya upinzani vimefanikiwa kuongeza kibindoni viti
1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2009
ambapo vilipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Matokeo haya yametoa mwelekeo mpya kwa vyama vya siasa nchini,
wapinzani wakiamini huo ndiyo ufunguo wao kuelekea Ikulu mwakani, CCM wakiamini
kuwa huko ni kujikwaa tu na wataendelea kubaki Ikulu mwakani kwani bado
wanakubalika kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza mjini Dodoma hivi karibuni, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda alisema kwamba wakati
CCM ikifanikiwa kupata ushindi wa jumla wa mitaa na vijiji 9,406, vyama vya
upinzani vimepata nafasi 3,211.
Katika matokeo hayo CCM kimepata vijiji 7,290 kikifuatiwa na
Chadema yenye vijiji 1,248. CUF imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na vijiji 946,
ikifuatiwa na UDP yenye vijiji vinne na TLP na NLD vyenye viwili kila kimoja.
Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM kimechukua jumla ya
mitaa 2,116. vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF
(235), ACT (9), NCCR - Mageuzi (8) wakati vyama vya TLP, UMD, UDP na NRA
vimepata mtaa mmoja kila kimoja.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo nchini, wananchi
watapiga kura leo baada ya kushindwa kufanya hivyo Desemba 14 kutokana na
kasoro kadhaa zilizojitokeza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema matokeo hayo ni dalili kuwa
CCM itafanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.
Ingawa waziri huyo alikiri kuwa vyama vya upinzani
vimechukua maeneo mengi kuliko uchaguzi uliopita, alisema vyombo vya habari
vinatumika kupotosha hali halisi na kuifanya CCM kuonekana kuwa imepoteza viti
vingi kuliko uhalisia.
Matokeo hayo yanaonyesha CCM imepoteza viti zaidi katika
mikoa wa Dodoma, Lindi, Mtwara, Iringa, Arusha, Singida na katika baadhi ya
majimbo ya Dar es Salaam.
Nape akiri makosa
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye naye alisema
makosa yanayofanywa kwenye kura za maoni katika chama hicho ndiyo yanayokigharimu
na badala yake kupeleka furaha kwa wapinzani.
Alisema katika baadhi ya maeneo wananchi walipiga kura za
hasira ili kuiadhibu CCM baada ya majina ya watu waliowataka kugombea uongozi
kutopitishwa na chama hicho.
“Tunajua kwamba kuna maeneo mengi ambayo wapinzani
wameshinda. Ukiangalia CCM tulifanya makosa katika kumweka mgombea, hivyo
kusababisha hasira ambazo kwa kweli zimewafurahisha wapinzani lakini sisi
zimetugharimu,” alisema.
Serikali ya mseto yanukia
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika
alisema wananchi wameamua kuvipigia kura vyama vinavyoundwa na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) baada ya kubaini kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi
ya kuwapatia maisha bora.
“Hasira ya wananchi dhidi ya CCM imetokana na mchanganyiko
wa mambo mengi, wananchi wamechoka kupewa ahadi zisizotekelezeka kuhusu kupewa
maisha bora, kupambana na ufisadi na kuchakachuliwa kwa maoni kwenye Rasimu ya
katiba,” alisema Mnyika.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ubungo alisema lengo
la Ukawa ni kuingia Ikulu mwaka 2015 na kwamba iwapo wananchi wataendelea na
imani waliyoionyesha kwenye uchaguzi huo, upinzani wanatarajia kupata viti
vingi zaidi ya CCM bungeni.
“Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu anatoka kwenye
chama chenye wabunge wengi, haiwezekani Waziri Mkuu na Rais watoke vyama
tofauti, CCM italazimika kuunda serikali ya mseto,” alisema.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa wananchi hawapotezi
imani na Ukawa, tayari Chadema kwa upande wao wameandaa mwongozo na mafunzo
maalumu kwa viongozi wa mitaa waliochaguliwa.
Wakati Ukawa wakishangilia idadi kubwa ya viti waliyopata
kwenye uchaguzi huo, baadhi ya wananchi wanaonyesha wasiwasi kuhusu viongozi
waliochaguliwa kwa madai kwamba baadhi yao hawana sifa ila walipigiwa kura ya
ndiyo ili kuiadhibu CCM.
Akizungumzia suala hilo, Mnyika alisema sifa ya kwanza ya
kiongozi ni kuaminiwa na wananchi waliomchagua na kwamba kabla ya kupata nafasi
ya kugombea walipitishwa kwenye mchujo wa ndani ya chama.
“Sifa nyingine ya uongozi ni uadilifu na ushirikishaji
wananchi kwenye uamuzi ndiyo maana tunaamini wataongoza vizuri, mafunzo
tuliyowaandalia ni nyongeza tu,” alisema.
Profesa Safari
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari
anasema Ukawa inaweza kuingia Ikulu kwa njia rahisi kupitia Uchaguzi Mkuu ujao
endapo mambo matatu yatatekelezeka kwa sasa.
Profesa Safari alitaja mambo hayo kuwa ni kukamilika kwa
maboresho ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura, kupatikana Tume Huru ya
Uchaguzi na kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto ya kuwafikia wananchi wengi
vijijini.
Alisema kuhusu Daftari la Wapigakura, idadi kubwa ya vijana
na wafuasi wa Ukawa kwa sasa hawana fursa kwani hawana sifa za kupiga kura
hivyo kukamilika kwa zoezi hilo itakuwa kitanzi kwa CCM.
“Matokeo ya uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa yanaonyesha
kuwa kura za wapinzani zitaongezeka maradufu lakini tutafanikiwa endapo daftari
litawafikia vijana wote wenye sifa kwa asimilia mia moja,” alisema na kuongeza:
“Jambo la pili, ni kufanikisha kuwafikia wananchi wengi
vijijini, kwa sasa tumeshasambaza pikipiki zaidi ya 2,000 katika vijiji
mbalimbali katika kanda kumi tulizofikia.”
Alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kupitia chama
chake amefanikiwa kuwafikia wananchi wengi kutokana na ziara zake kote mikoani
mpaka vijijini, ambako ndiko waliko wapigakura wanaohitaji mabadiliko.
Profesa Safari alitaja kikwazo kingine kuwa ni uwepo wa Tume
ya Uchaguzi isiyokuwa huru tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini.
“Tume ya Uchaguzi tumekuwa tukiipigia kelele mara nyingi
ifanyiwe maboresho lakini hakuna hatua zozote. Tunahitaji kuwa na Tume Huru ya
Uchaguzi ambayo inaweza kusahihisha dosari zilizojitokeza kwenye chaguzi
zilizopita,” alisema Profesa Safari.
Katika hatua nyingine, Profesa Safari alisema matokeo ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamechagizwa zaidi na sakata la uchotwaji wa
fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo liliibuliwa na Gazeti la The
Citizen.
Profesa Lipumba.
Naye Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema endapo umoja huo ungefanikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi
huo, CCM ingeanguka vibaya.
Profesa Lipumba alisema katika maeneo mengi waliyoshindwa na
CCM, kura zilionekana kutofautiana kwa idadi ndogo hali ambayo wangeweza
kushinda endapo wangeunganisha kura zao kwa mgombea mmoja.
Akitoa mfano, Profesa Lipumba alitaja maeneo waliyofanikiwa
kuunganisha nguvu ambayo ni Kimara, Kigamboni, Ubungo na Kijitonyama yaliyopo
Dar es Salaam, Ukawa ilishinda.
“CCM wangeanguka vibaya, lakini ni changamoto iliyojitokeza
kwa wawakilishi wetu kutoelewana, kutofahamu juu ya azimio letu kama Ukawa,”
alisema na kuongeza:
“Kwa hivyo tunaomba imani ya Watanzania iendelee kuwapo,
tutafanya tathmini ya kina ili kuepuka athari hiyo mwakani.”
Kibamba
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus
Kibamba alisema kiburi cha baadhi ya watendaji ndicho kilichoifikisha CCM
mahali ilipo hivi sasa na kwamba endapo Rais Kikwete hatawachukulia hatua
viongozi hao, huenda hali ikawa mbaya zaidi kwenye uchaguzi ujao.
Pia, alisema CCM imefanya vibaya kwenye Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa kutokana na Serikali kusita kuwachukuliwa hatua viongozi waliotajwa
kwenye sakata la uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu.
“Mchakato wa Katiba Mpya utazidi kuathiri uchaguzi ujao, kwa
sababu wapo baadhi ya watendaji wa CCM wanadhani kura ya maoni ipigwe baada ya
uchaguzi mkuu,” alisema.
Hata hivyo, Kibamba alisema CCM inapaswa kumshukuru Katiba
Mkuu wa chama hicho, Kinana ambaye alizunguka nchi nzima akizungumza na
wananchi.
Wasomi
Mdhahiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam,
Danford Kitwana alisema CCM haina jambo jipya la kufanya kwa wananchi ili
iendelee kukaa madarakani zaidi ya kutekeleza ahadi ilizotoa.
Alisema iwapo chama hicho hakitafanya hivyo huenda hali
ikawa mbaya zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwani inaweza kupata kura
chache zaidi huku za vyama vya upinzani zikipanda.
“Hata hivyo muda uliobaki chochote kinaweza kutokea na
kubadilisha hali ya hewa,” alisema.
Kwa upande wake, Dk Benson Bana kutoka Idara ya Sayansi ya
Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema Watanzania wameichoka CCM
kwa sasa.
“Vijana wengi wanaamini kuwa Chadema ndiyo inaweza kuwa
tumaini na mbadala wao kwa CCM, walijipanga na matukio ya ufisadi yakawabeba
ndiyo sababu ya kutoa ushindani kwenye Serikali za Mitaa,” alisema Dk Bana.
Awali, Dk Bana alisema kuwa Ukawa wana uwezo wa kuendesha
Serikali bila hofu yoyote ya kuyumbishwa kutokana na msingi wa Katiba, sheria
na kanuni zinazoendesha Taifa.
“Nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na Ukawa siyo muungano
wa kwanza kujaribu hatua hiyo, Kenya upinzani wameingia kwa muundo kama huo na
nchi inaongozwa,” alisema.
“Wangeongeza idadi kubwa ya wafuasi kwa sababu Watanzania
wamechoshwa na CCM na wanatamani kuona dhamana ya kura yao kupitia nguvu ya
chama kimoja,” alisema.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina
Mlama alisema hakuna tafiti zinazoweza kuonyesha nafasi ya Ukawa kuchukua
Serikali, lakini wameonyesha juhudi za kuleta ushindani.
“Ukawa wamethubutu, wamejaribu hivyo tunatakiwa kusubiri
sanduku la kura kwa sababu wananchi wenyewe ndiyo watakuwa na majibu kama
watakuwa tayari kwa pamoja kuleta mabadiliko ya kimfumo,” alisema Profesa
Mlama.
Matokeo ya CCM yashuka
Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka
2004 yanaonyesha kuwa CCM ilipata asilimia 88.4, huku vyama vya upinzani
vikiambulia asilimia 11.6.
Mwaka 2009, CCM kilivuna kura nyingi zaidi kwa kupata
asilimia 93.70 baada ya kujiongezea asilimia 5.3 kutoka kura za awali. Hata
hivyo, mambo hayakuwa mazuri kwa vyama vya upinzani kwani vilijikuta vikipata
asilimia 6.30.
Kwa upande mwingine takwimu za matokeo ya CCM katika chaguzi
mbalimbali zinaonyesha kushuka tangu mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete
anaingia madarakani.
Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Rais Kikwete
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kitaifa, alipata asilimia 80.28 dhidi ya vyama
vya upinzani vilivyokuwa vimepata asilimia 19.72.
Uchaguzi uliofuata CCM iliporomoko kwenye kiti cha urais
hadi asilimia 61.17 huku vyama vya upinzani kwa pamoja vikiambulia asilimia
38.30.
Ripoti ya Twaweza
Ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Twaweza kuhusu maoni na
matakwa ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa iliyotolewa Novemba mwaka huu,
ilieleza kuwa kama Watanzania wangepiga kura mwaka huu CCM ingepata asilimia
54.
Kwa mujibu wa utafiti huo, imani ya wapenzi wa CCM juu ya
wagombea wao watarajiwa inashuka kila mwaka. Mwaka 2012, Edward Lowassa alipata
asilimia nane, 2013 (20) na 2014 (17).
Mizengo Pinda mwaka 2012 alipata 23, mwaka 2013 na 2014
alipata asilimia 14. John Magufuli mwaka 2012 alipata asilimia 8, 2013 (6) na
2014 asilimia tano.
No comments:
Post a Comment