Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na mwaka
mpya, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda
huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo
mbalimbali ya starehe ambapo uzoefu unaonyesha baadhi ya watu hupenda kutumia
fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu hasa wa kujipatia vipato na
mali.Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, katika mikoa yote limejipanga
vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha
kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kipindi hiki cha
sikukuu na pale ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka. Ulinzi
umeimarishwa kwenye maeneo yote ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe
na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Hata
hivyo, watu wote watakaoenda maeneo ya beach wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka
kuzama kwenye maji.
Aidha, tunawakumbusha wananchi kuwa makini katika suala zima
la usalama wa maisha na mali zao, hususani kuchukua hatua stahiki na za haraka
kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo
yao na sehemu mbalimbali za biashara, na watokapo kwenye makazi yao wasiache
nyumba wazi ama bila mtu na pale inapobidi watoe taarifa kwa majirani zao.
Wazazi wanakumbushwa kuwa makini na watoto kwa kutokuwaacha watembee peke yao,
ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao
ikiwemo kupotea. Aidha, wazazi waepuke kuwapeleka watoto kwenye kumbi za disko
toto ambazo siyo salama.
Vilevile, wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie usalama
katika kumbi zao, hawarusiwi kujaza watu kupita kiasi kwenye kumbi hizo,
hususani kumbi za disko toto. Aidha, wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo
mengine yenye mikusanyiko mikubwa ya watu wanakumbushwa kufunga vifaa maalum
vya kufuatilia mienendo ya watu wanoingia na kutoka katika maeneo hayo (CCTV
kamera).
Pia, Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao
watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo
kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.
Mwisho, tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za
mipango yoyote ya uhalifu watakayoiona ikiendelea mahali popote kwa kuwafichua
wahalifu hao ili hatua za kuzuia uhalifu huo ziweze kuchukuliwa mapema. Taarifa
zinaweza kutolewa kupitia namba ya simu 0754 78 55 57 au Simu za Makamanda wa
Polisi wa mikoa au katika kituo chochote cha Polisi.
No comments:
Post a Comment