Rais Uhuru Kenyatta amemwachisha kazi waziri wa usalama
Joseph Ole Lenku na kumpendekeza waziri mpya wa usalama Joseph Nkaiseri
kuchukua nafasi hio.
Wakati huohuo mkuu wa polisi nchini Kenya inspekta generali
David Kimaiyo amejiuzulu kutokana na shinikizo dhidi yake afanye hivyo kwa
kushindwa kukabiliana na utovu wa usalama nchini.
Rais Kenyatta alisema kuwa baada ya mazungumzo na Bwana
Kimaiyo alikubali 'kustaafu' mapema kutoka kwa majukumu yake kwa sababu za
kibinafsi.
Rais alitoa tangazo hilo wakati akihutubia taifa kufuatia
shambulizi la hapo jana dhidi ya wachimba migodi 36 waliouawa na Al Shabaab
mjini Mandera Kaskazini ya Kenya.
Aliyekuwa mkuu wa polisi David Kimaiyo
Rais pia alitangaza kuwa amekubali ombi la Generali wa
polisi David Kimaiyo kuachia wadhifa wake.
Kimaiyo na Ole Lenku wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo za
kuachia ngazi kufuatia kukithiri kwa utovu wa usalama nchini.
Hatua ya kuwatimua kutoka katika nyadhifa zao wawili hao
bila shaka litakuwa jambo la kuridhisha kwa wakenya wengi ambao wamekuwa
wakilalamikia utovu wa usalama na kuwataka waondoshwe ofisini.
Uteuzi wa Joseph Nkaisery kama waziri mpya wa usalama ni
jambo jipya kwani atakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka kwa upinzani kuwa ndani
ya serikali.
Alipokuwa anahutubia nchi,Rais Kenyatta aliwasihi wabunge
kuongeza mda wa vikao vyao vya leo ili kumhoji na kumkagua Nkaisery
aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya waziri mpya wa usalama na maswala ya ndani ili
wamuidhinishe.
No comments:
Post a Comment