Pages

Monday, January 19, 2015

Bomu lajeruhi watano banda la video


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai.
Watu watano akiwamo mtoto wa miaka 15, wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa  bomu la mkono lililotupwa kwenye  banda la kuonyeshea picha za video.
Bomu hilo linadaiwa kuwa ni la kutengenezwa kienyeji, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai.

Pamoja na shambulio hilo, watu wengine watatu wamefariki dunia  na wengine wanne  kujeruhiwa  katika matukio tofauti ya ajali na kuuawa.

Kamanda wa Polisi Mkoa  akizungumzia bomu alisema ni la kurushwa kwa mkono na kwamba  lilivurumishwa alhamisi saa  2 usiku, kwenye kibanda cha kutizamia picha za video kilichoko  kijiji cha Amboni na kujeruhi watizamaji watano.
 



Waliojeruhiwa ni  Hassan Abdallah (72), Rashid Ally (45), Mrisho Abdi (29) mtoto   Juma Mtoo (15) na Abdul Ismael (19) wote wakazi wa kijiji cha Amboni.
Kashai alisema wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Tanga, Bombo wakiwa na majeraha mbalimbali mwilini na kwamba  Ally Rashid  (25) mkazi wa kijiji hicho anashikiliwa kwa uchunguzi.

Rashid anahusishwa na bomu hilo linalodaiwa ni la kutengeneza kienyeji kwa mujibu wa Kamanda.

Wakizungumzia tukio la bomu hilo, baadhi ya wananchi  waliokuwa eneo la tukio walieleza kuwa waliona kitu chenye mwanga angani  kabla ya kutua kwenye banda ambalo  walikuwemo watu zaidi ya 30 wakifurahia picha za video.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kutokuwa na hofu ya  tukio hilo na kwamba hali ya usalama imedhibitiwa huku uchunguzi wa kina ukiendelea na kuhimiza ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo kukabiliana na uhalifu.

Katika tukio jingine, mtuhumiwa George Nambai, ameuawa na watu wenye hasira baada ya jaribio lake la kutaka kupora simu kushindwa.

Aliuawa baada ya  kushindwa kuiba badala yake wananchi wenye hasira walijitokeza  kumshambulia hadi kufa.

Kamanda Kashai  alisema aliuawa  juzi katika eneo la Central baada ya kumchoma  kitu  chenye ncha kali  ubavuni Mohamed  Abraham  ili  kumnyang’anya simu, hata hivyo mmiliki huyo wa simu naye  alifariki wakati  akipatiwa matibabu katika hospitali ya Bombo.

Kamanda Kashai alisema tukio jingine ajali ya gari lenye aina ya Isuzu iliyokuwa ikiendeshwa na Mngazija Shabani,  ilipinduka na kusababisha kifo cha abiria mmoja na kujeruhi wengine wanne.

Ajali hiyo ilitokea Shume wilayani Lushoto na aliyepoteza maisha ni Irene Emanuel (14) na  waliojeruhiwa  ni Irene Grayson (16), Rose Elieza (30), Eva Mbonea (28) na Emilia Elineema wote wakazi wa Mavumo Shume wilayani Lushoto. Ajali hiyo ilihusisha gari namba T 618 AHT.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment