KAMATI
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeiagiza Bodi ya Korosho
Tanzania, kuandika barua inayoeleza hatua walizochukua katika kurudisha
nyumba iliyouzwa kwa Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka (CCM).
Akitoa agizo hilo, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kamati yake haijaridhishwa na namna nyumba hiyo ilivyouzwa.
Zitto
aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha inapeleka barua yenye taarifa na lazima
iifikie kamati leo saa 6, ikieleza mchakato, taratibu na hatua
waliyofikia katika kushughulikia suala hilo.
Taarifa
ya CAG inaonesha nyumba ya Bodi ya Korosho iliyopo katikati ya jiji la
Dar es Salaam, iliuzwa kwa Koka kwa thamani ya Sh milioni 300 na
iliyokuwa Bodi ya Kilimo, ambayo kwa sasa haipo.
Pia,
Zitto aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha wanatafuta hati za nyumba na
viwanja vyake na kila hatua wanayofuatilia watoe taarifa kwa kamati.
Aidha,
PAC imeitaka Bodi ya Korosho kuhakikisha mapato ya nje yanayopatikana
kutokana na kuuza korosho, wayatumie kuongeza thamani ya zao hilo
ikiwamo kufufua viwanda.
No comments:
Post a Comment