Kiungo wa klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani Junior Malanda,
20, amefariki dunia katika ajali ya gari.
Malanda, aliyekuwa akiichezea timu ya taifa ya Ubelgiji ya
chini ya umri wa miaka 21, amecheza mechi 15 msimu huu katika Bundesliga na
mechi za Europa League ikiwemo dhidi ya Everton.
Mkurugenzi wa michezo wa Wolfsburg Klaus Allofs amesema
katika taarifa: "Tumesikitishwa sana, na hatuamini kilichotokea, hatuna
hata maneno ya kusema.
"Hatuamini hayuko nasi tena. Sala zetu katika kipindi
hiki kigumu tunazielekeza kwa familia yake."
Allofs ameongeza: "Alikuwa chachu katika timu na mwenye
furaha. Junior alikuwa mchezaji kandanda mzuri sana na ambaye ndio kwanza
alikuwa akichipukia."
Malanda alihusishwa na kuhamia Fulham na Crystal Palace
wakati alipoondoka Zulte Waregem mwaka 2013, lakini badala yake alijiunga na
Wolfsburg.
Mchezo wake wa mwisho ulikuwa dhidi ya Cologne waliposhinda
2-1 mwezi Disemba.
Polisi wa Wolfsburg wamesema Malanda alikuwa abiria katika
gari lililopata ajali katika barabara kuu karibu na mji wa Bielefeld.
Alikuwa akielekea kuungana na wachezaji wenzake kabla ya
kusafiri kwenda Afrika Kusini katika kambi ya mazoezi.
No comments:
Post a Comment