Pages

Tuesday, January 27, 2015

POLISI HAWAWEZI KULINDA RAIA KWA FEDHA



IGP, Ernest Mangu

ULINZI wa nchi yetu kamwe hauwezi kufunga-manishwa na fedha bali uzalendo. Hata askari washindi hawaingii vitani na vitita vya fedha mifukoni bali mioyo iliyojaa mapenzi kwa nchi yao. Hii ni tafakuri yangu.
Picha za askari waliouawa kwenye shambulio la ‘kigaidi’ Ikwiriri mkoani Pwani hivi karibuni zilinirudisha darasani ambako nilifundishwa kuwa picha huongea zaidi ya maneno 1,000.

Sababu za mauaji hayo ukilinganisha na picha za polisi waliouawa zinatofautiana; hii ni kwa mujibu wa elimu yangu. Haiwezi kuwa sawa, nia ya kuiba silaha kituoni ikaambana na kuwacharanga mapanga polisi ambao kwa tafsiri walishasalimu amri kabla ya kuuawa.



Najivika uhusika; niliyetaka kumuibia nimeshampiga panga mbili kichwani, yuko chini anavuja damu kwa nini nisichukue nilichokitaka na kuondoka? Kinachonisukuma kumkata panga tena na tena mwilini ni kitu gani? Bila shaka ni hasira au chuki.

Sitaki kuendeleza tafsiri hiyo hapo juu kwa sababu inaeleweka kwa wenye akili. Badala yake najikita katika kufikiri; jamii imefika mahali pa kuwaficha wauaji mpaka zawadi ya fedha itangazwe? Kwamba, tuna watu ambao wako tayari kuiuza amani yetu kwa fedha?

Nani ametufikisha kwenye ushenzi huu? Kwamba tuwe tayari kuwaficha wauaji, watu wanaopora silaha, wanaohatarisha usalama wa taifa letu mpaka tulipwe fedha! Hiki ni kiwango cha juu cha uasi wa taifa.
Ndiyo maana sikubaliani na falsafa ya mkuu wa jeshi la polisi nchini, Ernest Mangu ya kutangaza dau la kuwalipa wanaofanikisha upatikanaji wa wahalifu wakiwemo wanaowaua kinyama polisi wenye dhamana ya kulinda raia na mali.

Nikiulizwa nini kifanyike kwa usalama wa taifa letu? Nitaanza kusema: “polisi hawawezi kulinda raia kwa fedha.” Kinachotakiwa kufanyika ni kuifanya dola yetu kuwa ndugu wa jamii. Naamini msingi wa amani uko hapa.

Raia wa kawaida hawezi kumficha aliyemcharanga mapanga ndugu yake mpaka asubiri kulipwa milioni 20. Ukiona hilo linatokea basi mantiki yake ni kuwa mtu huyo alishauvua udugu na kujiungamanisha na wauaji.

Ikiwa ni hivi jeshi la polisi limeshawahi kujiuliza kwa nini askari wake wanauawa kikatili? Mipango ya kuvamia vituo vya polisi inafanyika wapi?Hao wavamizi wa vituo wanaishi wapi na ndugu zao ni akinani? Je, wanapomaliza kufanya unyama kama huo wa Ikwiriri wanaelekea wapi, nani anayewapikia chakula baada ya kufanya ushenzi huo?

Hizo silaha wanazopora wanazihifadhi wapi?  Wanatumia usafiri gani, wanapita barabara gani na wapi wanapolala watu hao? Je, wametengeneza dunia mpya siyo hii ya raia wa kawaida?Nafikiri majibu ya maswali hayo yanatoa taswira kuwa uhusiano baina ya polisi na raia ni jambo la kushughulikiwa haraka iwezekanavyo. Wazo hili ninalo yapata mwaka sasa lakini nimekwama kulifikisha kwa wakuu wa polisi kwa sababu hawako tayari kulipokea.

Hata hivyo, sitasita kupigia kelele lau kwenye karatasi kwa sababu nauona uasi mkubwa usoni. Maana sijui hizi silaha zinazoibwa kila siku zinapelekwa wapi, zitatumikaje na nani atakuwa shabaha ya magaidi.
Nasisitiza taifa haliwezi kulindwa kwa fedha.

Wananchi hawapaswi kuhongwa ili walinde usalama wao; huu ni utamaduni mbaya usiopaswa kujengwa kwenye taifa hili. Nimeshauri mara nyingi na leo nitashauri tena;  tuwafundishe raia uzalendo kwa nchi yao, tuwaelimishe namna ya kujilinda kabla ya kulindwa.

Kama hilo halitoshi, tulifanye jeshi la polisi kuwa ndugu wa raia. Tukifanya hivyo hakuna haja ya kuwahonga wananchi ili wawafichue wahalifu na wanaoua polisi wetu na kupora silaha. Nachochea tu!

No comments:

Post a Comment